Tabora. Baadhi ya wanawake waliopata huduma ya kujifungua kwenye Zahanati ya Isevya iliyopo Manispaa ya Tabora wameiomba Serikali kujenga uzio mrefu kuzunguka zahanati hiyo ili kukomesha watu wasio na maadili wanaowachungulia.
Wanawake hao wanasema wakati wa wakijifungua kuna baadhi ya watu wenye rika la vijana huwachungulia kupitia mwanya uliopo kutokana na eneo la hospitali kutokuwa na uzio hivyo kuwa na ugumu katika udhibiti wa mwingiliano wa watu.
Akizungumza na Mwananchi, Lucy Seleman mkazi wa Kata ya Isevya alisema wapo watu hao ambao siyo wastaarabu wamekuwa wakiwachungulia wanawake wanaojifungulia kwenye zahanati hiyo jambo ambalo ni la aibu.
“Baadhi ya vijana wa kata hii ya Isevya Manispaa ya Tabora wamekuwa wana tabia za kuchungulia wanawake wanapokua wanajifungua kwenye zahani yetu. Hili ni jambo baya na liko kinyume na maadili yetu, hivyo tunaiomba Serikali itujengee uzio mkubwa kuzunguka zahani yetu ili kukomesha matendo haya,” amesema.
Mkazi mwingine wa Kata hiyo, Zuhura Ismail aakiwa katika maandalizi ya kujifungua mtoto wake mwenye miezi nane sasa, alichunguliwa na vijana hao aliowaelezea kuwa hawana maadili.
“Mimi nina watoto wanne mpaka sasa, miezi nane iliyopita nilienda kujifungua katika zahanati yetu ya Isevya, wakati nangojea muda ufike wa kujifungua nikaona vijana dirishani wakichungulia kwenye chumba ambacho wazazi huwa tunajifungulia, kwa kweli nilijisikia vibaya hivyo tunaiomba serikali upatikane uzio ili eneo lile lijitegemee” alisema
Alipotafutwa mmoja kati ya wauguzi wa Zahanati hiyo ambaye hakuwa tayari majina yake yawekwe wazi alisema changamoto hiyo ipo na wamelifikisha kwenye mamlaka husika kwa ajili ya kufanyiwa kazi baada ya malalamiko kuwa mengi.
Alipotafutwa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Tabora Ramadhan Kapera ili kuzungumzia changamoto hiyo alisema serikali tayari imeshaanza kuchukua hatua ambapo Sh20 milioni zimetengwa kwaajili ya kujenga uzio katika eneo la zahanati hiyo ili kuepusha mwingiliano uliopo baina ya wagonjwa na wapita njia.
“Ni kweli tumekuwa tukipata malalamiko ya baadhi ya watu kupita ilipo zahanati ya yetu ya Kata ya Isevya na kuwachungulia wanawake wanapokuwa kwenye hali yao ya kujifungua, hili halikubaliki katika jamii lakini tayari tumeshatenga milioni 20 kwaajili ya kujenga uzio ambao utasaidia kuondoa kero hiyo kwa akina mama wetu,” amesema Kapera.