Abiria 45 wanusurika kifo basi likipinduka Mwanza

Mwanza. Abiria 45 waliokuwa wanasafiri na basi la Kampuni ya ‘Bunzali Mtoto Safaris’ wamenusurika kifo baada ya gari hilo kupinduka eneo la Buhongwa Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza.

Ajali ya basi hilo lililokuwa likitokea Stendi ya Mabasi Nyegezi jijini hapa kwenda Maswa mkoani Simiyu imetokea leo Jumapili Agosti 4, 2024, Saa 6:30 mchana.

Taarifa za awali zinadai hakuna kifo bali abiria sita kati ya 45 waliokuwemo wamepata michubuko na tayari wamepelekwa Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana kwa matibabu.

Dereva msaidizi katika basi hilo, Method Marko amesema lilipinduka wakati likisubiri kupakia abiria katika kituo cha Dampo Kata ya Buhongwa.

“Tulikuwa tunasubiria kupakia abiria dereva akawa anaiegesha pembeni hapo ndipo sijui lilimshinda na kupinduka. Hata hivyo, hakuna aliyepata majeraha makubwa,” amesema Marko.

Marko amesema abiria ambao hawajapata majeraha wamefaulishwa kwenye gari nyingine ili kuendelea na safari yao kwenda Maswa mkoani Shinyanga, huku waliopata michubuko wakiendelea na matibabu.

Shuhuda wa ajali hiyo, Sangi Chacha amesema akiendelea na biashara yake katika soko la Dampo alishuhudia basi hilo likipinduka upande, ndipo walipowahi na kuanza kuwanasua abiria waliokuwemo.

“Tunashukuru kwamba hakuna aliyepoteza maisha, tumewasaidia wote wako salama,” amesema Chacha.

Akizungumza na Mwananchi Digital, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa amesema maofisa wa Polisi tayari wamefika eneo la tukio.

“Ni kweli nina taarifa ya ajali hiyo kutokea na watu wangu wako eneo la tukio, nitatoa taarifa mara tu watakapokuwa wamenipatia ripoti ya uchunguzi uliofanyika, kwa hiyo unaweza kunirudi baadaye nikupe taarifa kamili,” amesema Kamanda Mutafungwa.

Mwananchi ilifika eneo la tukio na kushuhudia Mkuu wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Nyamagana, Virginia Sodoka akiwa na maofisa wa Polisi wakishirikiana na baadhi ya wananchi kulinasua basi hilo kwenye korongo la barabara ilipodondokea.

Jitihada za kulinasua basi hilo zilizodumu kwa dakika zisizopungua 20 zilifanikiwa.

Related Posts