Morogoro. Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina moja la Semeni (21), amefariki dunia baada ya kuzama kwenye Mto Ngerengere, mkoani hapa.
Akizungumza na Mwananchi Digital jana akiwa eneo la tukio, shuhuda Alphonsi Ernesto amesema Semeni alizama maji jana Jumamosi Agosti 3, 2024, wakati akiogelea.
Amedai licha ya marafiki zake kumuonya asithubutu kuogelea kwa kuwa si mzoefu, lakini Semeni alikaidi ushauri huo na kwenda kuogelea ambapo alizama na kupoteza maisha.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa mashuhuda, tukio hilo lilitokea Saa 11 jioni katika eneo linalojulikana kwa jina la Yespa, Kata ya Kihonda, baada ya Semeni na wenzake kumaliza kibarua cha kukata majani kwa ajili ya kulisha mifugo.
Imeelezwa walipokuwa wakinawa mtoni, ndipo Semeni alizama wakati akijaribu kuogelea na mwili wake umepatikana leo Jumapili Agosti 4, 2024 saa 8:00 mchana, baada ya juhudi za uokoaji zilizodumu kwa takriban saa nane.
Ofisa wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wa Mkoa wa Morogoro, Fadhili Makala amesema juhudi za uokoaji zilianza baada ya kupata taarifa ya kuzama kwa Semeni kutoka kwa mashuhuda wa tukio hilo.
“Tumefika hapa baadhi ya watu wakawa wanalihusisha tukio hili na imani za kishirikina wakati wa uokoaji, jambo ambalo si jema,” amesema Makala.
Hata hivyo, tukio hilo limeibua wasiwasi juu ya usalama wa eneo hilo, ambalo lina historia ya vifo vya watu kuzama.
Mashuhuda, akiwemo Alphonsi Ernesto amesema licha ya marafiki kumwonya, Semeni alisisitiza kuogelea na alipoingia mtoni, alionekana kusukumwa na nguvu isiyojulikana hadi alipozama.
Naye Abdala Mtolange, mmoja wa waokoaji, amesema changamoto ya kuupata mwili wa marehemu, zilihusisha mbinu za kiasili ili kuuona.
“Tulikuja huku kufanya kazi, tumeenda shambani tumefyeka muda wa jioni wakati tunarudi, tukaja kunawa hapa, lakini kaka alienda kule akanawa baadaye akatuambia anataka kuoga, tukamwambia asioge kwanza mpaka tuwaulize wenyeji wa hapa kina kikoje.” “Tukamwita mtu mmoja tukamuhoji, lakini kabla hatujamaliza kuzungumza na yule mwenyeji, tukashtukia mwenzetu amerukia kwenye maji akaanza kuogelea na alipofika kati pana kina kirefu tukaona kama kuna kitu kinamvuta nyuma, akarudi juu akaanza kutuita tumsaidie tukaita na watu wengine wamsaidie wakajaa, wakapiga simu ‘fire’ wakaja hapa lakini hawakufanikiwa kumuona mpaka leo,” amesimulia shuhuda Alphonsi Ernesto.
Lakini Mwenyekiti wa eneo hilo, Zakia Yusuph amethibitisha kuwa sio mara ya kwanza tukio la watu kuzama katika eneo hilo, huku Diwani wa Kihonda, Hamisi Kilongo akitoa wito kwa wananchi kuacha kuogelea mtoni hapo.
Kilongo ameahidi mipango ya kuweka uzio au nyavu ili kuzuia matukio kama haya.