KIPA wa Yanga, Djigui Diarra amesaini mkataba mpya wa miaka mitatu wa kuendelea kukitumikia kikosi hicho hadi mwaka 2027.
Hatua hiyo imejiri katika utambulisho wa wachezaji na benchi la ufundi la kikosi hicho kwa ajili ya msimu ujao ambapo Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said alitangaza kumuongezea mkataba mpya nyota huyo.
Diarra alijiunga na kikosi hicho Agosti, 2021 alitokea Klabu ya Stade Malien ya kwao Mali, huku akiwa ni miongoni mwa makipa bora kikosini humo.
Nyota huyo tangu ajiunge na Yanga ameisaidia kutwaa mataji mbalimbali ikiwemo Ligi Kuu Bara, Ngao ya Jamii huku akitwaa tuzo tofauti tofauti akiwa na kikosi hicho.
Kwa msimu uliopita, Diarra aliipa Yanga ubingwa wa Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho la FA huku akitwaa tuzo ya kipa bora wa FA msimu uliopita katika tuzo za TFF zilizofanyika Agosti Mosi mwaka huu jijini Dar es Salaam.