Dk Nchimbi, wenzake kujikita kanda ya ziwa kwa siku 14

Kigoma. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amewasili Kigoma kuanza ziara ya siku tatu ikiwa ni mwendelezo wa ziara zake za kukagua uhai wa chama na utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020-2025.

Dk Nchimbi ameanza ziara yake leo Jumapili Agosti 4, 2024 na anatarajiwa kuendelea na ziara hiyo ya siku 14 hadi Agosti 18, 2024 katika mikoa ya Kigoma, Kagera, Geita, Mwanza na Mara.

Dk Nchimbi amewasili Kigoma saa 2 asubuhi akipokewa na makada wa chama hicho na anatarajiwa kufanya mkutano wa hadhara baadaye saa 10 jioni.

Kabla ya mkutano huo, Katibu Mkuu na timu yake watakuwa na kikao cha ndani na viongozi wa CCM Mkoa wa Kigoma na watazungumza changamoto zao za uendeshaji wa chama pamoja na utekelezaji wa ilani ya uchaguzi.

Kesho Jumatatu Agosti 5, 2024, Dk Nchimbi ataendelea na ziara yake katika Wilaya ya Kasulu ambako atahitimisha ziara yake katika mkoa huo Agosti 6, 2024 kabla ya kuelekea mkoani Kagera kuendelea na ziara yake.

Dk Nchimbi alianza ziara Julai 28, 2024 katika mikoa ya Mtwara na Lindi aliyoihitimisha Julai 31, 2024 akiwa amefanya mikutano ya hadhara, kusikiliza kero za wananchi na kutembelea kaburi la Rais wa awamu ya tatu, hayati Benjamin Mkapa lililopo katika Kijiji cha Lupaso, Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara.

Ziara ya Dk Nchimbi inafanyika ikiwa imepita miezi sita tangu aliyekuwa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Paul Makonda alipotembelea mkoa huo, Februari 3, 2024 na kusikiliza kero za wananchi waliojitokeza.

Katika ziara yake, Dk Nchimbi ameambatana na wajumbe wa sekretarieti ya CCM akiwamo Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla, Katibu wa Organaizesheni, Issa Gavu Haji na Katibu wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Rabia Abdallah Himid.

Mkoa wa Kigoma unaopatikana Magharibi mwa Tanzania, unakabiliwa na changamoto ya miundombinu ya barabara katika baadhi ya maeneo pamoja na ukosefu wa masoko kwa baadhi ya mazao ya kilimo kama vile michikichi.

“Tumefurahia ujio wa Katibu Mkuu wa CCM, tutamweleza kero zetu. Sisi wananchi tuna kero nyingi ikiwamo barabara za hapa mjini, ni mbovu,” amesema Mariam Hilalio, mkazi wa Kigoma mjini.

Related Posts