UKIWA shabiki wa Yanga leo una jambo moja tu la kufanya kama ni siku ya kuabudu basi nenda kwanza kamshukuru Mungu, kisha ukitoka kaivae uzi wa klabu hiyo, weka fedha mfukoni na usisahau tiketi yako na ukiona vipi beba na vuvuzela kwena kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kitachoendelea huko unakijua.
Ndio, si unajua kwamba Wananchi huwa hawana jambo dogo…unaambiwa kuanzia saa 3:00 asubuhi mageti ya Kwa Mkapa yatakuwa wazi kuwapokea wageni ambao ni mashabiki wa Yanga watakaokuwa wamejitokeza ili kuhitimisha Kilele cha Wiki ya Mwananchi waliyoipa kauli mbio ya Nyie Hamuogopi!
Kauli hii ya Yanga inakuja kama kuwatisha wapinzani watakaokutana nao katika michuano mbalimbali ya msimu mopya, ikitambia mziki wa kikosi chao kilichosajiliwa kibabe kikiongezwa nyota wachache tu lakini wenye moto hasa ambao mapema tu washachukua Kombe moja la mapema kule Afrika Kusini.
Wananachi wanasisitiza Kilele cha Wiki ya Mwananchi ni Funga Kazi kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa mashindano ikianza Ngao ya Jamii kisha Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho na michuano ya CAF.
Pale Benjamin Mkapa kulikuwa na Tamasha la Simba Day lililofanyika jana, lakini Yanga ilishakuwa imejipanga sawasawa kuhakikisha hakuna kinachoharibu mpango wao kuelekea Kilele cha Wiki ya Mwananchi.
Saa sita usiku wa kuamkia leo, Yanga ikavamia uwanjani hapo baada ya kuweka kila kitu chao jana mapema kwenye Uwanja wa Uhuru na kazi ya kuupamba kwa haraka Kwa Mkapa ikaanza kwa kikosi kazi cha watu wasiopungua 150.
Kikosi kazi hicho kimepewa masharti mawili tu, kuhakikisha uwanja unapendeza kwa rangi za Yanga lakini kusionekane mapambo yoyote ya watani wao, Simba uwanjani hapo.
Umesikia ile nyimbo mpya ya Yanga iliyotengenezwa na msanii Harmonize? Basi jamaa atakuwa ndani ya nyumba na ratiba siku hiyo inaonyesha kutakuwa na burudani za kumwaga.
Ukiacha Harmonize wasanii wengine waliothibitiashwa kuburudisha ni pamoja na Christian Bella, Marioo, Chobis Twins, Pado, Billnass na Meja Kunta ambaye amesajiliwa rasmi kuwa msanii maalum wa muziki wa singeli kufuatia Dulla Makabila aliyejaribu kukimbilia Simba.
Konde Boy ameachia ngoma mpya iitwayo Yanga Dobi Dobi, huku wasanii wengineo hao wakiachia zao kusindikiza tamasha hilo funga kazi.
Ukiacha wasanii hao pia DJ Ally B kama KAWAIDA ataendelea kuwapa burudani ya kuimba na kupiga muziki kama ilivyokuwa matamasha yaliyopita.
Mbali na wasanii hao mabosi wa juu wa Yanga hadi jana walikuwa wanapambana na Diamond Platinumz ambaye kama mambo yatakwenda atakuwa sehemu ya watakaotoa burudani kwenye shoo hiyo na hii inaweza kuwa rekodi ya aina yake ya kukutanisha mafahari mawili tamashaani, yaani Mondi na Konde Boy Kwa Mkapa.
Mashabiki wa Yanga ni kama wamechukizwa na kejeli za watani wao Simba ambao walikuwa wanadai kwamba, wao kwenye mambo ya kuwahi supu wako fasta lakini ishu ya kununua tiketi aah…wazitooo!
Kejeli hizo zikawaibua Yanga ambao jana mapema tu tiketi zote zilikluwa zimeunzwa ambapo zile za VVIP zilizokuwa zikiuzwa Sh 600,000, Royal (Sh 300,000), VIP A (50,000), VIP B (30,000), VIP C (15,000)
Machungwa 10,000 na Mzunguko Sh 5,000 zote zilikuwa zimeuzika fasta tofauti na ilivyokuwa awali.
Baada ya kumalizika kwa tiketi hizo, Yanga jana waliamkia kwenye supu mara walipomaliza kukimbilia na kufanya jogging ili kujiweka freshi kwa ajili ya leo kuujaza uwanjani (full house) bila zengwe mapema!
Baada ya kukosa tamasha moja lililopita, Haji Manara ‘Bugatti’, anarudi kazini kunogesha tamasha hilo ikielezwa amejiandaa vilivyo kuhakikisha anafanya utambulisho wa kibabe kwa mastaa wa kikosi hicho.
Manara anatarajiwa kuteka shoo hiyo katika utambulisho wa mastaa wa Yanga wakiwemo wale saba wapya ambao ni; Abubakar Khomeny, beki Chadrack Boka, viungo Clatous Chama, Duke Abuya, Aziz Adambwile na washambuliaji Jean Baleke na Prince Dube.
Taarifa kutoka ndani ya Yanga zinasema timu hiyo mara itapoingia itakuwa kwenye vazi maalum nje ya suti mlizozoea na baada ya hapo itaingia uwanjani kusalimia mashabiki kwa kuzunguka ikiwa na mavazi mengine.
Haitaishia hapo, timu hiyo itakapoingia kujaribu Uwanja itakuwa kwenye vazi lingine na baadaye kuvaa vazi lingine wakati wa kupasha misuli.
Hata itakapocheza mechi itavaa jezi za nyumbani kwenye kipindi cha kwanza lakini kipindi cha pili itavaa uzi wa ugenini zikiwa zote mpya.
Simba jana wao walijipima dhidi ya APR ya Rwanda, ambao ni mshindi wa pili wa michuano ya Kombe la Kagame 2024 iliyofanyika jijini Dar es Salaam na leo sasa itakuwa ni zamu ya Yanga kuvaana na mabingwa wenyewe wa michuano hiyo, Red Arrows ya Zambia.
Mabingwa hao wa Zambia walishiriki Kagame kama waalikwa na kufanya kweli kwa kubeba ubingwa ikiwa ni mara ya kwanza kwa timu waalikwa nje ya CECAFA kunyakua taji kwa kushindwa kwa pebnalti 10-9 baada ya dakika 120 kumalizika kwa sare ya 1-1.
Mchezo wa Yanga dhidi ya Arrows umepangwa kuanza saa 2:00 usiku ambapo mashabiki wa Mabingwa hao wa Tanzania, watakiona kwa mara ya kwanza kikosi chao cha msimu ujao kikicheza Kwa Mkapa mara baada ya kuwashuhudia tu kuputia runinga ilipokuwa ikiliamsha kule Sauzi.
Ikiwa Afrika Kusini Yanga ilicheza na FC Augsburg ya Ujerumani na kulala 2-1, kisha kuzichapa TS Galaxy na Kaizer Chiefs kwa bao moja kila moja na kubeba ubingwa wa Kombe la Toyota kutoka huko.
Mabosi wa Yanga jana walikuwa wanasubiri kupata uhakika wa maombi yao ya kumualika Makamu wa Rais Dk Phillip Mpango kuwa mgeni rasmi wa tamasha hilo na kama atakuja basi itakuwa mara yake ya kwanza kuhudhuria mechi ya timu hiyo ambayo inaelezwa ndio anayoishabikia.
Mbali na kigogo huyo, lakini shoo hiyo itakayoshindikizwa pia na michezo kadhaa ya kirafiki, inatarajiwa kuhudhuiriwa na viongozi mbalimbali wa klabu hiyo, viongozi wa kiserikali na wanasiasa sambamba na mastaa mbalimbali ambao ni Wananchi na tamasha linawahusu ikiwa ni majibu kwa watani wao Simba waliolifanya tamasha la Simba Day jana kwenye uwanja huo huo.
Wananchi wana kiu ya kutaka kuona kitu gani kitajiri katika tamasha hilo, kwa maana ya kuanzia sapraizi ya watoa burudani, viongozi na hata wachezaji ambao watavaana na Wazambia wakiwa na kumbukumbu nzuri ya msimu uliopita kulifunga tamasha kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.
Katika mchezo huo, Mzambia Kennedy Musonda ndiye aliyefunga bao hilo pekee na kuwapa burudani mashabiki, huku majina ya Maxi Nzengeli, Pacome Zouzoua, Yao Kouassi, Skudu Makudubela, Gift Fred, Hafiz Konkoni na wengine waliotua klabuni kwa mara ya kwanza waliiteka shoo kwa kushangiliwa na mashabiki siku hiyo.