KUNA wakati huwa nacheka sana nikizisikia tambo za wanachama na mashabiki wa klabu za Simba na Yanga. Iwe ni katika vijiwe vya kahawa mitaani au ndani ya mitandao ya kijamii, huchekesha! Wanatambiana kuhusu nyota wa vikosi vyao. Iwe ni wale waliopo vikosini tayari ama wanaotajwa kusajiliwa kila msimu.
Hutambiana hadi uwezo wa wafadhili na wadhamini wao. Upande wa Yanga kipindi fulani walitambia sana fedha na Yusuf Manji. Hata hivyo, Manji alivyojiengua, waliishia maisha ya unyonge sana. Maisha kama yale waliyowahi kuishi Simba baada ya Mohammed Dewji kujiondoa Simba miaka ya 2000.
Hata hivyo, baadaye Mo Dewji akarudi na kuwapa jeuri upya. Msimbazi walikuwa wakiimba kila jina baya dhidi ya watani zao. Kisa fedha za Mo Dewji. Hata hivyo, kwa kuwa Mungu huwa hatupi viumbe wake. Leo Jangwani ni fulu kicheko. Wamepata uhai mpya.
Hii ni baada ya kampuni ya GSM kuina neema klabu hiyo. Wanachama na mashabiki wa klabu hiyo kwa sasa wananenepa! Sura zinang’aa kwa tabasamu kwa vile GSM kawaletea neema na kuwapa jeuri dhidi ya watani zao. Wasinenepe vipi wakati kila uchao wanasoma na kusikia taarifa kutoka kwenye vyombo vya habari juu ya bunduki flani ipo njiani kutua Yanga. Timu imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu misimu mitatu mfululizo. Imetwaa Kombe la Shirikisho misimu mitatu mfululizo.
Yanga imecheza Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa klabu ya kwanza ya Tanzania kufanya hivyo tangu michuano hiyo ilipoanza kuchezwa kwa mfumo wa sasa mwaka 2004.
Imesajili wachezaji wenye viwango vya hali ya juu na waliokuja kulipa kisasi cha mabao matano iliyowahi kupewa na Simba mwaka 2012. Ndio. Novemba 5 mwaka jana, Simba ilipigwa 5-1 na hata ziliporudiana tena Aprili mwaka huu ikalala tena 2-1.
Wiki iliyopita ilikuwa Afrika Kusini kucheza mechi ya kuwania Kombe la Toyota dhidi ya Kaizer Chiefs ya huko, baada yaa wali kucheza mchezo na timu ya Ligi Kuu ya Ujerumani, FC Augusburg na TX Galaxy ya Afrika Kusini. Mechi hizo hazijaja kwa bahati mbaya. Ni uhusiano mzuri alionao GSM na Wasauzi. Kiasi Simba wameishiwa pozi, japo wanajitutumua. Bado wana Mo Dewji.
Kitu cha kustaajabisha ni, haya ni maisha ya muda mrefu kwa wanachama na mashabiki wa klabu hizi. Wamekuwa wakifurahia mafanikio ya klabu zao kwa mifuko ya watu. Wakati mwingine hata hawajui, fedha za wafadhili ama wadhamini wao huwa zinatolewa kwa mipango ipi? Kuna mikataba gani ambayo klabu zao zimeingia. Wanalevywa na tambo, ghafla wafadhili ama wadhamini wakitimka wanaachwa njiapanda. Hawajui wawasaidie vipi viongozi wao kuzisukuma klabu zao. Hata inapotokea migomo baridi ya wachezaji wao kushinikiza kulipwa posho na mishahara yao baada ya kuzinguliwa, wanachama na mashabiki huishia kuwaka tu na kulaumu wachezaji au viongozi. Hawatoi mawazo wala michango ya kutatua tatizo.
Utamaduni huu upo miaka mingi na umeendelea kubaki kama ulivyo kwa sababu wanachama na mashabiki wa klabu hizo, hawajui jukumu lao na hawajui kama wao ndio wenye klabu na sio viongozi.
Kibaya ni, mifumo ya klabu hizo imeshindwa kubadilika tangu zilipoanzishwa. Kumbuka Yanga iliasisiwa mwaka 1935, ikiwa na maana kwa sasa ina miaka 89. Si midogo hata kidogo, lakini haina hata uwanja wa mazoezi, achilia mbali kumiliki wa kucheza mechi. Simba nayo ilizaliwa 1936, ikiwa na maana kwa sasa ina Miaka 88. Ni umri mkubwa kwelikweli, lakini ina uwanja wa mazoezi tu, pale Bunju. Hauwezi kuutumia kwa mechi zozote za ligi kulinganisha na Azam FC iliyozaliwa 2004 ina uwanja unaotumika hadi kwa mechi za kimataifa.
Najua kuna watu watasema Simba imehama mfumo wa wanachama kuwa kampuni, lakini nani mwenye hakika kama taratibu zote zimekamilika? Ili Simba iwe kampuni kamili zipo njia lazima ipite…juzi kati tuliambiwa mambo bado, ila klabu inaendeshwa kama kampuni. Mwanachama gani wa Simba amewahi kusimama kidete kutaka kujua mfumo huo umefikia wapi? Nani anayesumbuka kujua fedha zinazotumika ndani ya Simba kwa sasa, zinatoka wapi na kama zinatolewa na Mo Dewji kwa misingi ipi wakati bado mfumo haujakamilika pasee na hata ule mkwanja wa Sh20 Bilioni haujatoka? Timu ilikuwa kambini Misri. Nani aliyegharimia. Timu imesajili wachezaji 13 wapya wa ndani na wa kigeni. Nani anajua wanalipwa na nani na mishahara yao ipoje. Hakuna hata mwanachama mmoja anawaza hilo. Wanafurahia mafanikio. Siku timu ikifanya vibaya watamshambulia Murtaza Mangungu na Salim Abdallah Try Again na kumtusi MO Dewji. Juzi kati Yanga kilikaribiwa kuwaka. Kisa Juma Magoma na wenzake kufungua kesi iliyotolewa hukumu ya kutolitambua Baraza la Wadhamini. Hukumu iliyouweka rehani uongozi wa kina Hersi Said na wenzake. Ukimgusa Hersi, umeigusa GSM. Wajitoe! Kina Magoma na wenzake wataweza kumlipa Stephane Aziz KI, Pacome Zouzoua au Clatous Chama?
Kama Yanga isingekuwa na ujuaji mwingi wa wanachama na wazee wa klabu hiyo, huenda ingeshaachana na mfumo walionao sasa tangu miaka ya 1990 wakati George Mpondela ‘Castro’ na wenzake walipowashtukia wafadhili wenye asili ya Kiasia walioigeuza Yanga kitega uchumi chao.
Tarimba Abbas naye alifuata baadaye na kuanza kuibadilisha Yanga ili iendeshwe kisasa miaka ya mwanzoni mwa 2000, lakini si mnajua wanachama walivyomgeuka? Yanga ikabaki kama ilivyo na sasa ndo unasikia wanaanza mchakato kubadilisha mfumo kwa hisani ya GSM!
Miezi michache iliyopita baadhi ya wanachama waliokuwa sehemu ya uongozi wa klabu hiyo walijaribu kuhoji juu ya ushiriki wa GSM katika mambo ambayo hawajaingia naye kimkataba, si mnajua kilichotokea? Viongozi waligeukana na kusimamishana ili GSM asitimke klabuni. Wakihofia kurudi maisha ya umatonya!
Kwa umri ilizonazo Simba na Yanga na mtaji wa wanachama na mashabiki, klabu hizo zilipaswa ziwe mbali kimafanikio na kiuchumi, lakini zinajikaba zenyewe kwa vile wanachama na mashabiki wanachokitaka ni kuona timu zao zinabeba mataji ya nyumbani na pengine kufungana zenyewe ili wapate cha kutambiana mtaani basi!
Hawazishughulishi akili zao namna gani wazikwamue klabu zao ndiyo maana kwa miaka mingi zimekuwa zikiishia zikitegemea mifuko ya watu badala ya fedha zinazotengeneza kwa ukubwa na majina yao.
Nadhani inapaswa kuanzia sasa wanachama na hata mashabiki wa klabu hizo kuamka na kutambua, ni wao ndio watakaozikwamua Simba na Yanga na si watu wengine. Zipo njia nyingi zilishaainishwa!
Soka la sasa linaendeshwa kibiashara ambayo ni lazima klabu ziwe na mfumo ukaozifanya zikue na kusonga mbele. Simba imepiga hatua kubwa, lakini bado haiwezi kusema imefika ikutakako. Ni kweli inaendeshwa na Bodi ya Wakurugenzi, lakini wanachama wanajua chochote kuhusu mambo yanayoendelea klabuni kwao? Nafasi yao ni ipi katika kuisaidia klabu yao kwa mfumo huo wa hisa? Asilimia zinazotajwa kuwa ni zao, wanazijua na kuzishiriki kwa sasa? Kama hawajui wafanye nini? Nani wa kusaidia kuharakisha mchakato huo ili klabu yao iondoke mahali ilipo? Bila shaka ni mtihani kwao, pia ni somo kwa Yanga wakati wapo katika mchakato wa kutaka kuindesha kikampuni. Kila mpenda maendeleo ya soka anatamani klabu hizo ziondoke hapo zilipo. Ziwe na wanachama na mashabiki wanaojitoa kwa ajili ya kuzipeleka mbele.