MSIMU wa tatu wa mbio za mabadiliko ya Tabia Nchi kwa mwaka 2024, Climate Change Marathon 2024 zinatarajiwa kufanyika wilayani Pangani kwa mara ya kwanza zikihusisha washiriki kutoka ndani na nje ya Tanzania zikilenga kukusanya fedha zitakazotumika kugawa majiko ya gesi ya kupikia kwa wanawake.
Wanufaika katika mbio hizo ambao ni wanawake kutoka katika wilaya za Pangani na Handeni mkoani Tanga hususani waliopo katika Kijiji cha Msomera waliohamia kutoka Hifadhi ya Taifa Ngorongoro zikiandaliwa na taasisi ya Tree of Hope ikishirikiana na Asasi ya Muungano wa Jinsia na Mabadiliko ya Tabia Nchi.
Akizungumza Mkurugenzi wa Tree of Hope, Fortunata Manyeresa alisema mbio hizo zitafanyika Septemba 28 zikitanguliwa na bonanza la michezo mbalimbali ambapo pia washiriki watapata fursa ya kutembelea Mbunga ya za wanyama Saadani huku zaidi ya kaya 50 zikitarajiwa kunufaika mpango huo.
“Mbio za mabadiliko ya tabianchi kwa mwaka 2024 zinalenga kukusanya fedha kwa ajili ya kuhamasisha jamii kutumia nishati mbadala ili kuwasaidia wanawake katika wilaya za Pangani na Handeni waliopo Kijiji cha Msomera na tunategemea zaidi ya kaya 50 zitanufaika, mpango huu unalenga pia kupunguza uchafuzi wa mazingira tunatarajia kwamba tukio hili litaongeza uelewa kwa jamii juu ya athari za mabadiliko ya tabia nchi” alisema Manyeresa.
Mbio hizo itajumuisha mbio za kilomita 21 hadi 2.5 na washindi watavuna kati ya Sh 250,000-500,000 na Katibu wa Chama cha Riadha Mkoa wa Tanga, Hassan Mwagomba alisema chama kimetoa baraka zote, huku akiwakaribisha wadau wengine kushirikiana na kuunga mkono jitihada mbalimbali za serikali katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi kwa jamii pamoja na utunzaji wa mazingira.