Kwa Mkapa mambo yameanza kunoga

NYOMI ya mashabiki wa Yanga ikiwa imefurika nje, walioingia ndani wanaendelea na burudani ya muziki, huku mhamasishaji wa tamasha la wiki la Mwananchi, Dakota akiifanya kazi yake vyema.

Ndani ya Uwanja wa Benjamin Mkapa, mashabiki wanaendelea kuingia, huku zikipigwa nyimbo za wasanii mbalimbali Dakota akiwa anawahamisha.

Yanga leo inafanya tamasha lao, linalotumika kutambulisha kikosi chao cha msimu mpya, kuwapa nafasi mashabiki wao kuwatambua mastaa wapya na waliosalia kikosini.

Makamu wa Rais wa Yanga, Arafati Haji hakuwa nyuma kushuka chini kwenda kuwapungia mkono mashabiki na hawakusita kumwitikia kwa sauti za shangwe.

Kiongozi huyo amezunguka uwanja mzima akiwapungia mashabiki mkono, akiwa sambamba na Dakota anayewahamasisha wamsalimie kwa kumpungia mikono.

Amesikika akiwaambia “Wananchi makamu wa Rais Arafati Haji anapita basi tumpungie mikono kwa pamoja ,maana hao ndio wanatupa heshima ya kutamba na ubingwa.”

Yanga inafanya tamasha la sita tangu mwaka 2019 linaloenda na burudani mbalimbali ikiwamo utambulisho wa kikosi kipya na jezi mpya za msimu wa 2024-2025 kabla ya kumaliza kwa mechi ya kirafiki ambapo safari hii mabingwa hao wa Tanzania wanavaama na Mabingwa wa Kombe la Kagame 2024, Red Arrows ya Zambia.

Related Posts