Beirut. Zikiwa zimepita siku nne tangu kifo cha mkuu wa Hamas, Ismail Haniyeh kitokee, hali ya usalama katika ukanda huo si shwari huku Marekani ikiwataka raia wake kuondoka.
Tovuti ya BBC leo Jumapili Agosti 4, 2024 imeripoti kuwa: “Ubalozi wa Marekani mjini Beirut umewataka raia wake kuondoka Lebanon kwa haraka, huku mvutano ukiwa unaoongezeka Mashariki ya Kati.”
Lebanon ni miongoni mwa nchi zilizopakana na Israel ambayo ipo katika mvutano na Hamas na nchi zinazoiunga mkono Palestina.
Taarifa ya Marekani iliambatana na iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, David Lammy ambaye alisema hali ya kikanda, “inaweza kuzorota zaidi.”
Iran imeapa kulipiza kisasi dhidi ya Israeli kufuatia kifo cha mkuu wa Hamas, pia mauaji yake yalikuja saa chache baada ya Israel kumuua kamanda wa Hezbollah, Fuad Shukr huko Beirut.
Inahofiwa kuwa, Hezbollah yenye makao yake nchini Lebanon, kundi linaloungwa mkono na Iran, linaweza kulipiza kisasi jambo litakaloongeza mvutano.
Jana Jumamosi, Hezbollah ilirusha makombora katika mji wa Beit Hillel kaskazini mwa Israel japokuwa yalidaiwa kudhibitiwa.
Picha zilizotumwa kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha mfumo wa ulinzi wa anga wa ‘Iron Dome’ wa Israel ukizuia roketi hizo. Hakujawa na ripoti za majeruhi.
Israel imepakana na Lebanon upande wa kaskazini, mpaka huo ulitambuliwa na Umoja wa Mataifa mwaka 2000 kama mpaka rasmi kati ya nchi hizo mbili baada ya Israel kujiondoa kutoka kusini mwa Lebanon.