Kibaha. Mmiliki wa kampuni ya mabasi ya Sauli, Solomon Mwalabhila amefariki dunia kwa ajali ya gari iliyotokea Mlandizi mkoani Pwani.
Akizungumza na kwa njia ya simu na Mwananchi Digital leo Agosti 4, 2024 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Pius Lutumo amesema Mwalabhila amefariki leo baada ya gari lake kugongwa kwa nyuma na lori la mchanga.
“Ndiyo hilo tukio limetokea leo saa 12:30 asubuhi maeneo ya Mlandizi alikuwa anatoka Dar es Salaam kuelekea mikoani gari lake likagongwa na lori la mchanga kwa nyuma na akapoteza maisha papohapo,” amesema.
Lutumo amesema ndani ya gari marehemu Mwalabhila alikuwa na mtoto wake, Midrick Solomon mbaye amepata majeraha madogomadogo maeneo mbalimbali ya mwili wake.
“Huwa ana kawaida ya kusafiri na mtoto wake huyo kila anaposafiri hivyo wakati anapata ajali walikuwa wote” amesema.
Amesema wanamtafuta dereva wa lori la mchanga aliyesababisha ajali hiyo, Ramadhani Mkusa mkazi wa Zegereni Kibaha ambaye ametoroka.
“Tunamtafuta dereva huyo na mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali ya Mlandizi Kibaha,”amesema.