Dar es Salaam. Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi amesema atafuata taratibu na itifaki za nyadhifa za viongozi wa Serikali atakapoingia katika ofisi zao kuomba ushirikiano na ikishindikana atawalazimisha kushirikiana kupitia nguvu ya sheria.
Kinachompa nguvu ya kufanya hivyo ni kile alichofafanua kuwa, watumishi wa umma wanawajibika kwa wananchi kwa mujibu wa sheria, akitokea anayeifanya ofisi ya umma kama sebule ya nyumba yake atamlazimisha kuwajibika kupitia sheria.
Sababu ya majibu hayo ya Mwabukusi ni swali aliloulizwa baada ya kuukwaa urais wa TLS, iwapo atashirikiana na viongozi wa Serikali ambao kwa namna fulani ameonekana akipishana nao mitazamo na pengine hana uhusiano mzuri na wao.
Mwabukusi amechaguliwa kuwa Rais wa TLS Agosti 2, 2024, katika mkutano mkuu uliofanyika jijini Dodoma akiwashinda wagombea wenzake watano ni Sweetbert Nkuba, Paul Kaunda, Emmanuel Muga, Revocatus Kuuli na Ibrahim Bendera.
Hata hivyo, Nkuba ameahidi kukata rufaa mahakamani dhidi ya matokeo ya uchaguzi huo kwa kile alichodai, kulikuwa na kasoro lukuki na haamini ushindi wa Mwabukusi.
Mwabukusi amesema hayo jana Jumamosi usiku Agosti 3, 2024, alipohojiwa katika kipindi cha runinga cha Medani za Siasa kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha Star TV.
Amesema uhusiano kati ya TLS na Serikali upo kisheria na kanuni, hivyo atakapoingia ofisini hatafanya kazi kama Mwabukusi bali kwa msingi ya chama hicho.
“Yeyote atakayefuatwa, atafuatwa kwa itifaki za nafasi yake, sehemu ya kuomba tutaomba, sehemu ya kuchukua haki yetu tutaichukua bila kupepesa macho na sehemu ya kukemea tutakemea,” ameeleza.
Amesisitiza atakapomfuata yeyote katika ofisi hizo na asionyeshe ushirikiano atamlazimisha kulitekeleza hilo kisheria.
Kwa mujibu wa Mwabukusi, TLS haihitaji msaada wa yeyote kwa sasa, badala yake ni ushirikiano kutoka kwa wadau wake ambao Serikali ni miongoni mwao.
Alipoulizwa iwapo ana ugomvi na kiongozi yeyote serikalini, amekana akisema maadui zake alishawaweka bayana tangu siku za awali.
“Naamini sina ugomvi na kiongozi yeyote, sina ugomvi na taasisi yoyote, maadui wangu ni wezi wa mali za umma, wala rushwa na watu wasioamini katika utawala wa sheria na Katiba,” amesema.
Hata hivyo, kiongozi huyo mpya wa mawakili atakayeongoza kwa miaka mitatu hadi 2027 amesema kumekuwa na tafsiri hasi juu ya msimamo na ukosoaji wake wa mienendo mibaya ya Serikali, akisisitiza hatakoma kufanya hivyo.
“Kuna desturi na tabia zilizojengeka hasa za watu kutokuwa wa kweli katika nafsi. Sehemu ya kulia mtu anacheka, sehemu ya kukosoa anapongeza alafu atakuja kulaumu miaka 10 baadaye.
“Kwa mtazamo wangu yeyote anayefanya kosa anapaswa kuambiwa bila kupepesa macho na bahati mbaya wengi wanatafsiri tabia hiyo kama kukosa adabu,” amesema Mwabukusi.
Ameeleza hakuna mahali watakapofichana au kupakana mafuta kwa mgongo wa chupa, panapohitajika kukosoana watakosoana.
Majibu yake hayo, yametokana na swali aliloulizwa kuwa, ameonekana mtu mwenye jazba mara nyingi, haoni kama inaweza kuyumbisha uongozi wake.
Mwabukusi aliambatanisha majibu yake na ufafanuzi juu ya kamati ya maadili iliyokata jina lake wakati wa mchakato wa kuwania urais, akisema kisasi chake kiliishia kwenye kukata rufaa na Mahakama ilimtendea haki.
“Sina ugomvi binafsi na mtu yeyote na sitarajii kuwa na kisasi na kama kuna niliyemkosea niombe radhi ili tuijenge TLS yetu,” amesema Mwabukusi.
Alipoulizwa kuhusu malalamiko ya Nkuba, Mwabukusi amesema haoni kama kinacholalamikiwa na wakili huyo ni sawa, kwa kuwa uchaguzi ulikuwa wazi na kila kilichofanyika mawakala na wagombea walikuwepo kukiona.
Kuhusu madai ya karatasi zilizookotwa, amesema kwa mujibu wa taarifa katika karatasi hizo yeye ndiye aliyepigiwa kura, hivyo kama zimeokotwa maana yake ni hasara yake.
Kwa maneno mengine, amesema kwa karatasi zinazodaiwa kuokotwa maana yake zilikuwa kura zake na pengine zingehesabiwa angepata ushindi wa kura nyingi zaidi.
Hata hivyo, ameahidi kufanya kazi na wagombea wote akidokeza walikuwa na ajenda nzuri zinazohitajika kutekelezwa.
Amesema pamoja na pongezi mbalimbali alizozipokea kutoka kwa mashindani wengine, bado hajapokea kutoka kwa Nkuba.
Asisitiza kifungu cha nne
Kifungu cha nne ndiyo nguzo ya uongozi wake, akisema ndicho kinachoeleza haki za wanachama, utawala wa sheria, uwekezaji na masuala ya ulinzi wa mawakili wanapokuwa katika majukumu yao.
Ameeleza mambo hayo yanagusa idara mbalimbali za Serikali huku akisisitiza umuhimu wa kujenga hali ya kuaminiana kati ya Serikali na mawakili.
“Tutakuwa tukienda kufanya mazungumzo katika hali ya kuelewana kwanza ndivyo utaratibu ulivyo.
“Kifungu cha nne hakina maana yoyote ya kuleta vurugu isipokuwa ndiyo msingi wa TLS, nje ya kifungu cha nne ndipo zilipo vurugu lakini ndani yake hakuna tatizo,” amesema.
Anahofia kilichomtokea Lissu
Pamoja na kuonyesha kukerwa na hatua ya Rais wa zamani wa Chama hicho, Tundu Lissu kupigiwa risasi Septemba 7, 2017, Mwabukusi amesema hababaishwi na vitisho hivyo.
Lissu alishambuliwa kwa risasi zaidi ya 20 na baadhi kumpata mwilini siku hiyo mchana akiwa kwenye magesho ya nyumbani kwake Area D, jijini Dodoma akitoka kuhudhuria vikao vya Bunge.
Kipindi hicho Lissu alikuwa rais wa TLS, alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma kwa matibabu ya awali na usiku huohuo alipelekwa Hospitali ya Nairobi, Kenya kisha Januari 2018 alipelekwa Ubelgiji. Hakuweza kuendelea na uongozi wake wa urais.
“Siwezi kubabaishwa sitaruhusu hofu iyumbishe maisha yangu kwa sababu, hakuna binadamu aliyeumba uhai. Kuna makaburi mengi tunapita huko barabarani sio kwamba wote walikosoa Serikali ukifika wakati umefika tu tutakwenda,” amesema.
Hata hivyo, amesema atakapoingia ofisini ataangalia ulipoishia uongozi uliopita kuhusu kutafuta haki ya Lissu, naye ataendeleza kuanzia hapo.
Kuhusu matukio ya utekaji, Mwabukusi amemtaka Rais Samia Suluhu Hassan aunde Tume ya Kijaji itakayochunguza vitendo hivyo.
Amesema kuna madai kwamba watu hao wanajiteka wenyewe, tume hiyo ndiyo itakayokuja na jawabu.
Amehusisha hilo na kutoonekana kwa takriban wiki tatu kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda akifafanua kisheria wananchi wake walipaswa kuarifiwa.
“Makonda ni Mtanzania na mtumishi wa umma na anapofanya kazi ana wasaidizi wake. Kitendo cha kiongozi kukaa kimya bila kuwaambiwa wananchi ni kutowajibika kwa hali ya juu.
“Makonda ni kiongozi wa watu, kama yupo mahali amepumzika watoke hadharani watwambie, kunyamaza ni kinyume na utawala bora,” ameeleza.
Lakini, amesema uamuzi wa kumuulizia au kupigania kujua alipo ataufanya iwapo baraza la uongozi la TLS litaazimia hivyo.
Hata hivyo, Katibu Tawala Mkoa wa Arusa (RAS), Missaile Musa amesema Makonda yuko likizo.
Udhalilishaji kwa mawakili
Kuhusu vitendo vya udhalilishwaji wa mawakili, amesema kuna haja ya kujenga maelewano na taasisi husika kwa sababu wakili si mhalifu, bali ni mtu anayemuhudumia mtu anayehitaji msaada wa kisheria.
Kadhalika, Mwabukusi amesema kuna haja ya kupunguza nguvu waliyopewa majaji, kwa kuwa mara nyingi wanazitumia vibaya dhidi ya mawakili.
“Wakili anapotetea na kuwasilisha maoni ya mteja wake jaji asiwe na kofia mbili wakati huo huo anasikiliza kesi huku ana mamlaka ya kumsimamisha wakili uwakili,” amesema Mwabukusi.
Amesema kunahitajika kuheshimiana kwamba Mahakama ifahamu bila mawakili haiwezi kufanya kazi kwa weledi na mawakili waelewe bila uwepo wa Mahakama uwepo wao ni bure.
Mambo mengine aliyozungumzia ni kutengeneza utaratibu utakaowezesha mawakili kufanya mikutano itakayofikiwa na wote.
Kwa upande wa mawakili matapeli na makanjanja, Mwabukusi amesema atasimamia kwa kushirikiana na mamlaka mbalimbali kuwadhibiti kwa kuwa uwepo wao unaathiri hata uchumi wa nchi, akisema hawalipi kodi.