Serikali kufungamanisha Reli ya Tazara, SGR kurahisisha usafirishaji

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali itafungamanisha Reli ya Kisasa ya SGR na Reli ya Tanzania Zambia (Tazara) kwa lengo la kurahisisha usafiri wa watu, bidhaa na mazao ili kuleta maendeleo.

Ametoa kauli hiyo leo Jumapili, Agosti 4, 2024, wakati akiwasalimia wananchi wa Round About ya Mikumi, mkoani Morogoro, ikiwa ni siku ya tatu ya ziara yake rasmi ya kikazi aliyoianza Agosti 2 na itakamilika Agosti 6, 2024.

Rais Samia amesema kuwa dhamira ya kuunganisha reli hizo ni kurahisisha usafiri wa bidhaa na watu, hasa kwa kuzingatia kwamba Mikumi ni eneo lenye uzalishaji mkubwa wa mpunga na miwa, hivyo mazao hayo yataweza kusafirishwa kwa urahisi zaidi.

Pia, Rais Samia ameahidi kuwa Serikali itaendelea kutoa ruzuku ya mbolea na inajipanga kutoa ruzuku ya mbegu, akisisitiza kuwa Mikumi ni eneo lenye wakulima hodari wa mpunga.

Sh7.2 bilioni kudhibiti mafuriko

Aidha, Rais amesema Serikali imetenga Sh7.2 bilioni kwa ajili ya utafiti na ujenzi wa mabwawa na kingo katika bonde la Lwembe, ili kudhibiti mafuriko na kuongeza uzalishaji wa mpunga na miwa mara mbili kwa mwaka.

Katika suala la utalii, Rais Samia amesema filamu ya The Royal Tour imeongeza idadi ya watalii nchini, ambapo katika Hifadhi ya Mikumi, wageni wameongezeka kutoka 54,021 mwaka 2019/20 hadi 138,844 mwaka 2023/24.

Ametoa wito kwa wananchi na wawekezaji kujenga hoteli nzuri, ili kuboresha huduma kwa watalii.

Maombi ya Mbunge wa Mikumi

Mbunge wa Mikumi, Dennis Londo, ameomba Serikali kujenga barabara ya lami kutoka Kilosa hadi Mikumi na kufungua geti jipya la watalii. Rais Samia alijibu kuwa barabara hiyo itazingatiwa katika ilani ya uchaguzi ijayo, huku akisisitiza kuwa barabara zote zitajengwa, ili kuunganisha wilaya na maeneo mengine kwa ajili ya kurahisisha usafiri na biashara.

Ziara ya Rais Samia mkoani Morogoro inalenga kukagua na kufungua miradi, pamoja na kufuatilia matumizi ya fedha za Serikali.

Leo, Rais Samia ametembelea Chuo Kikuu cha Mzumbe na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa tawi la chuo hicho la Morogoro na anatarajiwa kufungua Daraja la Ruaha, Barabara ya Kidatu-Ifakara, na kuweka jiwe la msingi kwa ujenzi wa Kiwanda cha Sukari cha Kilombero (K4), miongoni mwa shughuli nyingine atakazofanya.

Related Posts