Shughuli imekwisha, tukutane ‘Nane Nane’

UKISIKIA funga kazi, basi ilikuwa jana wakati Yanga ilipohitimisha Kilele cha Wiki ya Mwananchi, saa 24 tu tangu Simba kufanya tamasha la Simba Day na kutambilisha mashine mpya za msimu wa 2024-2025m, huku mashabiki wa timu hiyo baada ya kuona vikosi vyote kutamba wakisema ‘Tukutane Nane Nane’.

Simba na Yanga zinatarajiwa kuvaana Alhamisi hii kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa katika pambano la nusu fainali ya Ngao ya Jamii, ikiwa Dabi ya Kariakoo ya kwanza msimu huu, huku kila upande ukiwa umeimarisha vikosi ilivyonavyo ambapo wikiendi hii zilikiwasha katika matamasha yao maarufu.

Katika mechi ya msimu uliopita, Simba iliitambia Yanga katika Ngao ya Jamii kwa kuifunga penalti 3-1 baada ya muda wa kawaida kumalizika kwa suluhu, lakini ilipigwa nje ndani katika Ligi Kuu, ikianza kwa kuchapwa 5-1 kabla ya kufungwa tena 2-1 na kujikuta ikimaliza nafasi ya tatu nyuma ya Yanga na Azam.

Hivyo, mashabiki wa klabu hiyo wanaona ni muda muafaka wa kukutana na wenzao Alhamisi kumaliza ubishi, kwani kila moja ikiamini ina kikosi bora kitakachofunika Kwa Mkapa kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu Bara Agosti 16. Washindi wa mechi hiyo ya Simba na Yanga ataumana na yule wa mechi kati ya Azam na Coastal Union zitakazocheza pia Agosti 8 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Unguja.

Sasa wakati mashabiki wa klabu hizo wakianza kuchimbana biti mapema kabla ya timu hizo kukutana Agosti 8, kilichofanywa jana na Yanga Kwa Mkapa ni kama kujibu mapigo kwa watani, wao baada ya Wananchi kujihimu mapema na kupata burudani ya kuhitimisha Kilele cha Wiki ya Mwananchi.

Mashabiki wa klabu hiyo walioujaza Kwa Mkapa baada ya kushindwa kuhimili kejeli za Simba baada ya kuweka rekodi kwa kumalizan tiketi za tamasha la Siomba Day siku tatu kabla ya kufanyika kwake.

Nyomi la Wananchi wakiwa na jezi mpya na zile za zamahi walijitokeza mapema Kwa Mkapa na kuanza kuingia uwanjani tangu saa 4 asubuhi, huku wengine wakibarizi nje, kuvuta muda licha ya burudani za muziki na michezo ya utangulizi ikiendelea ndani kunogesha tamasha hilo la sita tangu lilipoasisiwa mwaka 2019.

Tofauti na ilivyokuwa juzi wakati wa tamasha la Simba Day, jana mashabiki waliofurika Kwa Mkapa walipata wasaa wa kuingia uwanjani bila bughudha yoyote aui msongamano kutokana na kuwepo kwa utaratibu mzuri uliosimamiwa na wana usalama wakiwamo askari polisi tangu mapema.

Hali hiyo ilifanya mashabiki na wapenzi hao wa Yanga kuingia uwanjani kwa utatatibu wa kuachiana nafasi bila kusukumana na jambo hilo liliwafanya wafurahie na kueleza wanafurahia hali hiyo.

Wakati zimesalia saa chache kabla ya kikosi cha Yanga kutambulishwa kwa mashabiki katika sherehe za kuhitimisha Kilele cha Wiki ya Mwananchi, mashabiki wa klabu hiyo mapema tu wameanza kumtaja straika mpya wa timu hiyo, Prince Dube wakidai ndiye usajili uliowakuna zaidi.

Mashabiki hao wamesema Dube ndiye aliyebeba kwa sasa matumaini yao katika eneo la mbele na hasa wakati huu wanaenda kuvaana na Simba katika Ngao ya Jamii siku ya Agosti 8 kabla ya kuanza kazi kwenye michuano ya kimataifa  ya Ligi ya Mabingwa Afrika pamoja na Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho.

Nyota huyo amejiunga na Yanga msimu huu baada ya kuachana na matajiri wa Azam FC, huku mashabiki wa kikosi hicho wakipongeza viongozi kwa kukamilisha usajili huo wakisema wamelamba dume.

Mmoja wa shabiki wa timu hiyo aliyehudhuria kilele hicho cha Wiki ya Mwananchi, aliyejitambulisha kwa jina la Nurath Athuman amesema, usajili wa Dube ni silaha tosha ya kuwapa ubingwa msimu ujao.

“Msimu huu tumefanya usajili mzuri sana ila kwangu wa Dube umenipa jeuri ya kutamba mtaani, naamini msimu ujao tunabeba tena mataji yote ya ndani,” alisema Nurath.

Kwa upande wa shabiki mwingine aliyejitambulisha kwa jina la John JR alisema, hakuna asiyejua uwezo wa Dube hivyo mashabiki wa timu pinzani wajipange kwa maumivu mengine.

Shabiki mwingine, Ally Hamis alisema, licha ya Dube kuonyesha uwezo mkubwa hadi sasa ila wachezaji wote waliosajiliwa ni wazuri na wanawapa matumaini makubwa msimu ujao.

Tangu nyota huyo asajiliwe na kikosi hicho, tayari amefunga mabao mawili akianza katika michuano ya Mpumalanga Premier International Cup 2024, wakati alipoifungia Yanga iliposhinda 1-0, dhidi ya TS Galaxy ya Afrika Kusini.

Bao lingine Dube alifunga wakati timu hiyo iliposhinda mabao 4-0, dhidi ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini katika mchezo wa kirafiki ambao uliipa Yanga ubingwa wa michuano ya Kombe la Toyota Cup 2024.

Yanga ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu Bara na Kombe la FA msimu uliopita, imenasa saini ya nyota wapya saba ambao mbali na Dube ambapo wengine ni Clatous Chama aliyetokea Simba, Jean Baleke (Al-Ittihad SCS Tripoli), Aziz Andambwile (Fountain Gate), Chadrack Boka (FC Lupopo), Khomeiny Abubakar, Duke Abuya (Singida Black Stars).

Dube amesajiliwa baada ya kuitumikia Azam kwa misimu minne mfululizo akiifungia zaidi ya mabao 30 katika michuano yote tangu alipojiunga nayo mwaka 2020 akitokea Highlander ya Zimbabwe, huku akiwa na kismati cha kuitungua Simba mara kadhaa alipokutana nao katika michuano tofauti.

Kikosi kipya cha Yanga chini ya kocha Miguel Gamondi kinaundwa na makipa watatu,  Diarra Djigui, Abubakar Khomeiny na Abutwalib Mshery huku mabeki wakiwa ni Boka, Yao Kouassi, Nickson KIbabage, Kibwana Shomary, Dickson Job, Ibrahim Bacca na Bakar Mwamnyeto.

Viungo ni Khalid Aucho, Aziz Andambwile, Mudathir Yahya, Jonas Mkude, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Abuya, Pacome Zouzoua, Stephane Aziz Ki, Denis Nkane, Maxi Nzengeli, Chama na Farid Mussa, huku washambuliaji wakiwa ni Dube, Baleke, Kennedy Musonda na Clement Mzize.

Makamu wa Rais wa Yanga ambaye hajaonekana kwenye shughuli nyingi za Yanga kwa siku za karibuni, jana aliingia mapema uwanjani, aliliamsha kwa mashabiki baada ya kushuka jukwaani na kuwapungia mikono mashabiki kuwasalimia ambao waliompokea kwa shangwe uwanja mzima.

Mshehereshaji, Dakota De Lavida, alilikuwa akichombeza kwa kuwahamasisha mashabiki waliojaza uwanjani kumshangalia Makamu wa Rais huyo wa Yanga ambayo juzi kati aliula kwa kuteuliwa kuwa Mjumbe wa Bodi ya Uzalishajki Mali ya Jeshi la Polisi (TPFCS).

Mgeni rasmi wa tamasha hilo la jana alikuwa ni Makamu wa Rais wa Jamhuri, Dk Philip Mpango kama ambavyo Mwanaspoti lililodokeza mapema katika gazeti la jana akijumuika na vigogo wa klabu hiyo na viongozi wengine wa kiserikali na wanasiasa walioshiriki tamasha hilo lililosindikizwa na burudani ya soka kutoka kwa Yanga dhidi ya Mabingwa wa Kombe la Kagame 2024, Red Arrows ya Zambia.

Kabla ya mechi hiyo na burudani ya muziki kutoka kwa wasanii kama Harmonize, Marioo, Meja Kunte, King Of The Melodies, Christian Bella na wengine, mapema ilipigwa mechi kati ya Nyota wa zamani wa Yanga na Supastaa mbalimbali wanaoishabikia Yanga wakiongozwa na kocha Salum Mboto ambapo Maveterani wa Yanga walishinda 2-1 baada ya kipindi cha kwanza kuisha kwa sare ya 1-1 kisha kupisha burudani kutoka kwa Christian Bella alipanda jukwaani na kupiga ngoma mpya ya kuifagulia Yanga akisindikizwa na weanenguaji zaidi ya 20 jukwaani kabla ya kuangusha ngoma nyingine ikiwamo Msaliti na Nakuhitaji zilizowapa mzuka mashabiki na kuzicheza wakiwa jukwaani. kabla ya Marioo naye kuliamsha.

Bilionea wa klabu hiyo, Ghalib Said Mohammed ‘GSM’ aliingia uwanjani kibabe akisindikizwa na msafara wa watu kibao, ikiwa ni muda mfupi tangu Mjumbe wa Baraza wa Wadhamini wa Yanga, Mama Fatma Karume na Rais wa Yanga, Injinia Said Hersi kutimba uwanjani hapo na kuamsha shangwe kwa WanaYanga.

Related Posts