KAMA ulifikiria Singida Black Stars imekamilisha usajili, basi utakuwa unajidanganya kwani mabosi wa kikosi hicho kwa sasa wako mbioni kukamilisha uhamisho wa winga raia wa Niger, Victorien Adebayor kutoka AmaZulu FC ya Afrika Kusini.
Taarifa kutoka ndani ya timu hiyo, zililiambia Mwanaspoti kuwa, ni kweli mabosi wa Singida wanapambana kwa ajili ya kukamilisha dili hilo mapema, huku ikitaka kumtambulisha siku ya Singida Black Stars ‘Big Day’ itakayofanyika Agosti 10.
“Kama mambo yataenda sawa basi mchezaji huyo atajiunga na Singida kwa ajili ya kuichezea msimu ujao, Adebayor ni moja ya pendekezo la kocha mkuu, Patrick Aussems, hivyo tusubiri kuona kitakachojiri katika dili hilo,” kilisema chanzo chetu.
Nyota huyo ambaye mara kadhaa alihusishwa kujiunga na miamba wa soka nchini Simba, msimu uliopita alikuwa timu ya AS GNN ya kwao Niger aliyojiunga nayo Januari mwaka huu kwa mkopo akitokea AmaZulu ambayo huenda ikaachana naye kwa msimu ujao.
Ofisa Habari na Mawasiliano wa Singida Black Stars, Hussein Massanza alisema, bado hawajakamilisha usajili kwa asilimia zote, na hata wachezaji ambao wameonekana katika kikosi hicho wengine hawajasajiliwa isipokuwa wanafanya nao mazoezi tu.
“Wapo wachezaji wengine tutawatoa kwa mkopo ila hadi pale ambapo taratibu zitakapokamilika, kuna sapraizi kubwa inakuja hivyo mashabiki zetu watarajie mambo mazuri, kwa sasa kikosi chetu kimemaliza kambi yetu ya Arusha na kinarudi Singida,” alisema Massanza.