TASAC, ZMA zaafikiana kuimarisha ushirikiano usimamizi wa usafiri majini

Zanzibar. Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) na Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA) zimeafikiana kuingia makubaliano ya kushirikiana katika kusimamia masuala ya udhibiti na usimamizi wa usafiri majini.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya kufanyika kwa kikao Agosti 2, 2024 kwenye Ofisi za Mamlaka ya Usafiri Baharini, Visiwani Zanzibar chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Wizara ya Uchukuzi, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Zanzibar na Wizara ya Uchumi wa Buluu Zanzibar.

Katika kikao hicho, wajumbe walijadili changamoto katika usimamizi wa usafiri majini nchini na kuzitafutia ufumbuzi.

Hivyo, kikao hicho kilielekeza kuwa ndani ya wiki mbili, kukamilishwe na kusainiwa kwa hati ya makubaliano ya utekelezaji wa ushirikiano katika masuala hayo.

TASAC chini ya Mkurugenzi Mkuu, Mohamed Salum na ZMA chini ya Mkurugenzi Mkuu, Mtumwa Saidi wameahidi kutekeleza maelekezo hayo kama yalivyotolewa kwenye kikao hicho.

Mkutano huo ulihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Zanzibar, Dk Mngereza Mzee Miraji, Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Kapteni Hamad Hamad, Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Abdallah Mitawi na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk Ally Possi.

Related Posts