Unguja. Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), Hemed Suleiman Abdulla amekemea tabia ya baadhi ya makada wanaotangaza nafasi mbalimbali za kugombea kabla ya muda wake, huku wakijua kufanya hivyo ni kinyume na Katiba.
Hemed ambaye pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, amemuagiza Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana CCM (UVCCM), Mohammed Ali Kawaida kuwachukulia hatua wote wanaokwenda kinyume na maadili ya chama hicho.
Amesema hayo leo Jumapili Agosti 4, 2024 wakati akifungua kongamano la vijana la kuonyesha mafanikio, fursa na maendeleo ndani ya miaka mitatu ya Rais Samia Suluhu Hassan na Rais Hussen Mwinyi, lililofanyika katika ukumbi wa umoja ni nguvu mkoani Pemba.
“Wale wote wanaofanya hivyo wanatakiwa kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa kuwa wanakwenda kinyume na katiba na sheria za chama kwa kuwa wanakiletea sifa mbaya,” amesema.
Amesema chama kipo tayari kuhakikisha malengo ya vijana yanatimia, hasa katika kukipigania Chama cha Mapinduzi (CCM).
Pia, amesema uwepo wa makongamano ya kitaaluma ndani ya chama ni uimarishaji wa chama na kuunga mkono jitihada zinazofanywa na viongozi wa chama katika kutekeleza majukumu yao.
Mjumbe huyo amesema, jeshi la CCM ni vijana wanaohitaji kupewa taaluma juu ya kazi mbalimbali zinazofanywa na Serikali kwa lengo la kuwa mabalozi wazuri wa kuyatangaza yanayofanyika.
Onyo kama hilo limewahi kutolewa kwa nyakati tofauti na Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa chama hicho, Amos Makalla.
Viongozi hao wamekuwa wakiwaonya wale walioanza kampeni mapema za udiwani na ubunge kutokufanya hivyo na kuwaacha waliochaguliwa kuendelea kutekeleza majukumu yao ipasavyo na wasubiri wakati ufike.
“Tuwape nafasi waliochaguliwa wafanye kazi zao hadi muda sahihi utakapofika, msidhani chama kipo kimya, nyendo zako zinaratibiwa, kumbukumbu zako zitawekwa kwamba wewe umeanza kampeni mapema,” alisema Makalla, Mei 7, 2024 katika mahojiano maalumu na Mwananchi.
“…Niwatoe hofu CCM ipo makini inafuatilia, inapokea taarifa mbalimbali kutoka kwenye kata, majimbo kuhusu wanaojipitisha.”
Awali, Kawaida amesema kufanyika kwa kongamano hilo itakuwa fursa kwa vijana kuona namna gani wanazifikia fursa zilizopo kwa maslahi yao.
Kawaida amesema Serikali zote mbili zimetenga fedha kwa ajili ya kuwawezesha vijana, ili kuhakikisha wanawekeza katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo zitakazowakwamua kiuchumi.
Awali, mbunge wa Vijana Mkoa wa Kusini Pemba, Munira Mohammed Mustafa amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imetenga Sh16 bilioni kwa ajili ya vijana kujiendeleza kiuchumi na kujenga vyuo vya mafunzo ya amali katika wilaya zote.
Hivyo, amewataka vijana kuchangamkia fursa hiyo kwa kujiunga kwenye vikundi kuendesha shughuli mbalimbali za ujasiriamali.