Wananchi wafurika kwa Mkapa | Mwanaspoti

BALAA katika uwanja wa Benjamin Mkapa, kwani mashabiki wa timu ya Yanga wamejitokeza kwa wingi jambo lililosababisha foleni kubwa.

Muonekano wa nje ya uwanja kwa sasa unaonyesha idadi kubwa ya mashabiki waliovalia jezi nyeusi,njano na kijani wakiwa wamepanga mistari ya kuingia ndani ya dimba hilo iliyofika mpaka barabarani.

Ikiwa bado ni saa sita kabla ya mechi hiyo kuanza itakayo wakutanisha Yanga na Red Arrows Mabingwa wa Zambia  msimu uliopita.

Wananchi wamejihimu mapema kutaka kushuhudia kikosi chao kipya cha msimu wa 2024-2025 kitakachotambulishwa leo baada ya kuishuhudia tu kupitia runinga ikicheza mechi za kirafiki za kimataifa ikiwa kambini Afrika Kusini.

Yanga ikiwa huko ilicheza mechi tatu ikianza na FC Augsburg ya Ujerumani na kuchapwa mabao 2-1 kabla ya kuizima TS Galaxy ya Afrika Kusini ikiwa ni michezo ya michuano maalumu ya Kombe la Kimataifa la Mpumalanga kabla ya kuinyoosha Kaizer Chiefs kwa mabao 4-0 katika mechi nyingine ya michuano maalumu ya Kombe la Toyota na kuondoka nalo kibabe.

Kuanzia saa 2:00 usiku Yanga itacheza mechi nyingine maalumu kuhitimisha Kilele cha Wiki ya Mwananchi dhidi ya Red Arrows ya Zambia na mapema tayari Kwa Mkapa kumechangamka kwa mashabiki lukuki kujitokea, huku utaratibu wa siku ya leo ukiwa angalau kulinganisha na ule wa jana wa tamasha la Simba Day.

Hadi sasa hakuna vurugu wala changamoto kubwa zinazowazuia mashabiki kuingia uwanjani ambapo hali ya usalama iko vizuri kutokana na walinda usalama wakiwamo askari Polisi kuweka utaratibu mzuri unaotoa nafasi kwa mashabiki kuingia uwanjani bila bughudha tofauti na jana Wanasimba walipofikia hatua ya kuvunja uzio ili kugombea kuingia uwanjani na kuilazimisha menejimenti tya Mkapa kurekebisha tatizo baadae kwa kuongeza mageti zaidi ya kuingilia uwanjani.

Related Posts