Ajira 26,755 serikalini: Mbinu bora ya kuomba, kufanikiwa

Dar es Salaam. Wakati Serikali ya Tanzania ikitangaza ajira 26,755 ndani ya kipindi cha miezi miwili, wataalamu wa masuala ya rasilimali watu wameeleza mbinu za kuomba ajira hizo na kuingia kwenye usaili.

Baadhi ya mbinu hizo, wakati wa usaili ni lazima muombaji wa ajira aonyeshe anakwenda kuongeza ubunifu na kuleta matokeo na si uhitaji wa kazi, mshahara na maisha mazuri.

Kwa upande wa viambatanisho, waombaji wa nafasi hizo wanapaswa kuhakikisha taarifa zao kwenye vyeti vya kuzaliwa, taaluma na kitambulisho cha Taifa (Nida) zinaendana.

Kwenye ajira zilizotangazwa hivi karibuni na Serikali, ifahamike sekta ya elimu na afya ndizo kada zilizobeba namba kubwa ya ajira, huku nyingine kama wataalamu wa kilimo, udereva, uhasibu, manunuzi na maofisa ustawi wa jamii nao nafasi zao zikitangazwa.

Kwa kada ya afya, Julai 7, 2024 Serikali kupitia kwa Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kwa niaba ya Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa ilitangaza nafasi 9,483 mpya za ajira katika sekta hiyo

Kama hiyo haitoshi, Julai 21, 2024 Serikali ilitangaza nafasi nyingine 11,015 za sekta ya elimu, ikiwa ni baada ya kuwapo kwa ahadi kadhaa za kuajiri walimu 12,000 katika mwaka wa fedha 2024/25.

Nafasi zilizotangazwa zilielekezwa kwenye masomo ya kemia, fizikia na biolojia katika ngazi ya ualimu daraja la IIIB na IIIC, huku wale wa hisabati wakiwa zaidi ya 1,325.

Mbali na hizo, Agosti 3, 2024 Serikali ilitangaza ajira nyingine 6,257 za kada mbalimbali.

Kada zilizoguswa zaidi ni ununuzi, udereva, ofisa kilimo, wasaidizi wa kumbukumbu, uhasibu, waandishi waendesha maoni, maofisa maendeleo ya jamii na wasaidizi wa hesabu ndizo zenye nafasi nyingi za ajira na mwisho wa maombi ni Agosti 16, 2024.

Cha kuzingatia unapoomba ajira hizi

Meneja rasilimali watu, Harold Harold akizungumza na Mwananchi amesema wakati wa uombaji wa nafasi hizo ni muhimu muombaji kuwa timamu kiakili.

Jambo lingine muhimu, amesema mtu anayeomba kazi ahakikishe ana uelewa wa kutosha juu ya eneo analotaka kwenda kulifanyia kazi, ili kutobabaika anapoitwa kwenye usaili.

“Kwenye viambatanisho vyako, hakikisha jina lililopo kwenye kitambulisho cha Taifa (Nida) ndilo ambalo lipo kwenye vyeti vyako vyote kwa sababu vikipishana ni dhahiri itatafsiriwa hao ni watu wawili tofauti,” amesema.

Endapo nafasi ya ajira iliyotangazwa inahitaji mtu mwenye uzoefu na asiye na uzoefu akaomba, Harold amesema hawezi kupata.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali watu, Grace Adrian amesema mtu anapoomba ajira za Serikali ahakikishe ameweka taarifa zake zote zinazohitajika kwenye mfumo wa uombaji wa ajira serikalini (Ajira portal).

Mfumo huo amesema hakuna mtu anayeweza kuingilia na kurubuni watu, hivyo ni muhimu kuweka taarifa sahihi.

Grace amesema kwenye usaili njia mbili hutumika, ikiwemo ya mazungumzo na maandishi.

“Unaanza na maandishi, ukifaulu unakwenda kwenye mazungumzo, ukifanya vizuri kwenye maandishi ukateleza kidogo kwenye mazungumzo unabaki kwenye mfumo nafasi nyingine zikitoka unaitwa, hivyo ni muhimu uijue kazi unayokwenda kuiomba na kuielezea,” amesema na kuongeza;

“Tatizo kubwa la vijana wanaoomba ajira ni ujasiri na kukosa maarifa ya kile wanachokiomba, kama unaomba ajira ya udereva sheria za usalama barabarani lazima uzifahamu na ujue kuendesha gari, kama utakwenda ukiamini utapendelewa ni ngumu kwa sababu maswali yatakayotolewa hayasahihishwi na mtu mmoja, hivyo ni ngumu kupenya kwa ujanja ujanja,” ameeleza.

Zingatia haya kwenye usaili

Mtaalamu wa Rasilimali watu, Paul Mngongo akizungumzia eneo la usaili amesema ni tatizo kubwa, kwani vijana wengi wanaoitwa hawaendani na matakwa ya waajiri kwenye eneo la ujuzi.

“Kwenye eneo hili huwa mameneja rasilimali watu hawapewi kuzungumza, ila wanakutana na tatizo kubwa sana…watu ilipo sokoni haiendani na mahitaji, unataka mtu mbunifu na mwenye matokeo, lakini aliyepo anayetaka kazi, mshahara na maisha mzuri,” amesema.

Mngongo amesema ni muhimu vijana kwenda kwenye usaili wakiwa na mtazamo wa kuonyesha matokeo kwenye taasisi na si kuhitaji kazi, kwani ubunifu wenye matokeo ndio hutafutwa katika dunia ya sasa.

Amesisitiza dunia ya sasa huitaji mtu wenye ubunifu na matokeo, uwezekano wa kulipwa fedha nyingi upo.

“Ukiangalia utofauti wa ajira za Serikali na binafsi ni kwamba Serikali inatoa huduma na sekta binafsi inataka faida, lakini sasa kutokana na dunia ilivyo kila mfanyakazi anapaswa kuwa mbunifu kuleta matokeo hata serikalini,”

 Masharti ya jumla kwa waombaji

Katika nafasi hizo za ajira zilizotangazwa na Serikali, waombaji wanapaswa kuwa raia wa Tanzania wenye umri usiozidi miaka 45.

“Waombaji wenye ulemavu wanahamasishwa kutuma maombi na wanapaswa kuainisha kwenye mfumo wa kuombea ajira ulemavu walionao kwa ajili ya taarifa kwa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma,” taarifa ya Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma imebainisha.

Mahitaji mengine ni waombaji kuambatanisha cheti cha kuzaliwa kilichothibitishwa na mwanasheria/wakili.

Pia waombaji ambao tayari ni watumishi wa umma na wamejipatia sifa za kuingilia katika kada tofauti na walizonazo, wametakiwa kupitisha barua zao za maombi ya nafasi za kazi kwa waajiri wao na waajiri wajiridhishe ipasavyo.

Waombaji waambatishe maelezo binafsi yanayojitosheleza yenye anwani na namba za simu za kuaminika pamoja na majina ya wadhamini watatu wa kuaminika.

Vilevile maombi yote yaambatane na vyeti vya taaluma, maelezo, nakala za vyeti vilivyothibitishwa na mwanasheria/wakili ambavyo ni vyeti vya kuzaliwa, kidato cha nne, kidato cha sita kwa wale waliofikia kiwango hicho, vyeti vya kuhitimu mafunzo mbalimbali na vyeti vya kitaaluma kulingana na sifa husika.

Related Posts