Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imemhukumu Abdallah Ally Abdallah, kifungo cha miaka minne jela, baada ya kupatikana na hatia ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi zenye uzito wa kilo 6.12.
Abdallah, mkazi wa Mpapa visiwani Zanzibar, alidaiwa kukutwa na dawa hizo katika Bandari ya Dar es Salaam, sehemu wanapokaa abiria wanaosafiri kwenda Zanzibar.
Hukumu hiyo imetolewa leo Jumatatu Agosti 5, 2024 na Hakimu Mkazi Mkuu, Anna Magutu baada Mahakama kumtia hatiani.
Akisoma hukumu, Hakimu Magutu amesema mshtakiwa ametiwa hatiani kama alivyoshtakiwa, baada ya upande wa mashtaka kuwasilisha mashahidi saba na vielelezo kadhaa kuthibitisha shtaka.
“Baada ya kupitia ushahidi wa upande wa mashtaka, Mahakama imekukuta na hatia na kwamba utatumikia kifungo cha miaka minne gerezani. Una haki ya kukata rufaa, iwapo hujaridhika na uamuzi huu,” amesema Hakimu Magutu.
Kabla ya hukumu hiyo, mshtakiwa alipopewa nafasi ya kujitetea aliomba apunguziwe adhabu.
Hata hivyo, Hakimu Magutu ametupilia mbali ombi hilo na kumhukumu kifungo cha miaka minne gerezani.
Awali, wakili wa Serikali Mwandamizi, Monica Ndakidemi aliomba Mahakama itoa adhabu kali kwa mshtakiwa huyo, ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia ya kusafirisha dawa za kulevya wakati wanajua dawa hizo ni hatari.
Katika kesi ya msingi, Abdallah alidaiwa kutenda kosa hilo Januari 17, 2023 katika Bandari ya Dar es Salaam, iliyopo Wilaya ya Ilala.
Ilidaiwa siku ya tukio, mshtakiwa akiwa amekaa sehemu wanapokaa abiria wanaosafiri kwenda Zanzibar, alikutwa na dawa hizo za kulevya aina ya bangi zenye uzito wa kilo 6.12 zikiwa ndani ya begi.