WAZIRI wa Kilimo, Hussein Bashe amemjibu Mbunge wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina kwamba Serikali itaendelea kulinda masilahi ya wakulima wa miwa katika Bonde la Kilombero ikiwemo haki ya kuendelea kupeleka miwa kiwandani. Anaripoti Mwandishi Wetu, Morogoro … (endelea).
Bashe amewaeleza wakulima hao wasiwe na wasiwasi na hilo ilihali Mpina akiongozwa na jopo la mawakili zaidi ya 100 amefungua kesi tatu ikiwamo ya wakulima 24 wa Bonde hilo wanaopinga mahakamani kifungu cha 86 cha sheria ya fedha namba sita ya mwaka 2024 ambayo imetoa kinga iliyokuwepo mara ya kwanza kwenye soko la sukari nchini na kuruhusu uagiza holela wa sukari nchini.
Wakili Edson Kilatu anayesimamia kesi ambayo inahusu wakulima 24 wanaotokea bonde la Kilombero wakiongozwa na George Mzigondevu, alidai marekebisho ya kifungu cha 14 cha sheria hiyo inayosimamia soko la sukari Tanzania inaenda kuwaweka wakulima wa miwa rehani, kupoteza soko la miwa, fursa za ajira na kuathiri uchumi wa Taifa.
Kesi hiyo imefunguliwa wiki iliyopita dhidi ya Bashe na mwanasheria mkuu wa serikali, Jaji Dk. Eliezer Feleshi.
Hata hivyo, leo Jumatatu Bashe akitoa taarifa ya wizara kwa Rais Samia Suluhu Hassan anaendelea na ziara mkoani Morogoro amewahakikishia wakulima hao ambao hawakuvuna miwa yao mwaka jana kwamba Serikali imekubaliana na mwekezaji kuanza kuvuna hiyo kabla ya kuendelea na ya msimu huu.
“Miwa haitolala, miwa itaanza kuvunwa ya mwaka jana na mtaendelea kupata haki ya kupeleka miwa kiwandani msiwe na wasiwasi serikali inalisimamia hilo,” amesema Bashe.
Akizungumzia changamoto z wakulima hao, Bashe amesema iliyobaki ni uwazi katika kupima kiwango cha sukari kwenye miwa ya wakulima hao.
“Wamekuwa wakilalamikiwa sana na wazalishaji. Hatua ya kwanza tumekubaliana na Kilombero sugar wanapopokea miwa yao, kuwepo na wawakilishi wa wakulima, Tari na bodi ya sukari ambao pia watakuwa na mtaalaam ambaye anathibitisha kiwango cha sukari ambacho mzalishaji amekisema ili wakulima wapate haki yao,” amesema.
Ameongeza kuwa sasa wakulima wanapata bei nzuri kidogo ya kuanzia 100,000 hadi 108,000 ikilinganishwa na sehemu nyingine.