City inahitaji pointi za mapema Championship

WAKATI Mbeya City ikianza kambi yake kwa ajili ya msimu ujao, uongozi umeeleza muelekeo wa timu hiyo ukisisitiza utajipanga ndani na nje ya uwanja kukusanya pointi za mapema.

Timu hiyo inajiandaa na Championship kwa msimu wa pili mfululizo baada ya kushuka daraja 2022/23 na imeanza kambi yake huko Isyesye jijini humo kujiandaa na msimu mpya wa 2024/25.

Mtendaji Mkuu wa timu hiyo, Ally Nnunduma alisema kutokana na msimu uliopita kupoteza muelekeo dakika za mwisho, hawataki kujirudia tena na badala yake watakusanya pointi za mapema.

Alisema kinachowapa nguvu ni muunganiko wa ndani na nje ya uwanja kwa mashabiki na wadau namna wanavyoipa sapoti timu hiyo na kuahidi kuwa Ligi Kuu ndiyo kilio chao.

“Mashabiki wamekuwa pamoja na timu yao, wadau nao wanaendelea kutoa sapoti kwa lengo la kuirejesha City Ligi Kuu, tutajipanga kukusanya pointi mapema bila kumdharau mpinzani,” alisema Nnunduma.

Kigogo huyo aliongeza kwa sasa wapo katika mazungumzo na kampuni mbili ambazo zimeonyesha nia ya kuwekeza kikosini humo na baada ya makubaliano wataweka wazi kila kitu.

Mmoja wa mashabiki wa timu hiyo, Dickson Charles alisema hadi sasa wanaridhishwa na mwenendo wa City kwa namna uongozi unavyowashirikisha kila hatua na hali hiyo inaongeza ufanisi.

“Kwa kipindi cha nyuma timu ilionekana kuwa ya mtu mmoja, lakini kwa sasa tumeona ushirikishwaji, sisi mashabiki ndio tunaumia na kufurahia matokeo yoyote, tutapambana irudi Ligi Kuu,” alisema Charles.

Related Posts