NYOTA wa kimataifa wa Tanzania anayekipiga Al Nassr ya Saudi Arabia, Clara Luvanga amesema anatamani kuchukua Tuzo ya Kiatu cha Ufungaji Bora msimu huu wa Ligi Kuu Soka Wanawake nchini humo.
Msimu uliopita straika huyo alimaliza na mabao 11 akiwa kwenye nne bora za wafungaji nyuma ya Ibtissam Jraidi wa Al Ahli aliyefunga mabao 17 na kuibuka kinara.
Akizungumza na Mwanaspoti, Clara alisema malengo yake makubwa msimu huu ni kuisaidia timu hiyo kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Wanawake Saudi Arabia kisha kuchukua kiatu cha ufungaji bora.
Alisema msimu uliopita aliikosa tuzo hiyo kwenye mechi za mwisho ambazo ziliamua kiatu kwenda kwa Ibtissam.
“Msimu uliopita nilikuwa bora, natamani huu uwe zaidi ya uliopita, naamini nitafunga mabao mengi zaidi niisaidie timu yangu na niibuke mfungaji bora,” alisema Clara.
Msimu huu tayari Al Nassr imecheza mechi moja ya kirafiki dhidi ya PFC Femenino ya Hispania na kupata ushindi wa mabao 7-2 huku Clara akiweka kambani mabao matano.