Edgar apewa mmoja Fountain Gate

ALIYEKUWA mshambuliaji wa KenGold, Edgar William amekamilisha uhamisho wa kujiunga na Fountain Gate kwa mkataba wa mwaka mmoja.

Nyota huyo ambaye ni mfungaji bora wa Ligi ya Championship msimu uliopita akifunga mabao 21, amekamilisha dili hilo baada ya awali kukwama kujiunga na kikosi cha Singida Black Stars kilichomuhitaji ili akakichezee kwa msimu ujao.

Akizungumza na Mwanaspoti, Edgar alisema ameamua kuanza maisha mapya na kikosi hicho huku akiomba sapoti ya mashabiki wake licha ya kuamua kuondoka timu ya KenGold baada ya kuipambania kuipandisha kucheza Ligi Kuu Bara msimu ujao.

“Nawapenda sana mashabiki na viongozi wangu wa KenGold kwa sapoti kubwa ambayo wamenipatia tangu msimu uliopita, kwangu watabaki katika mioyo yangu ila nimeamua kutafuta changamoto sehemu nyingine, lengo nimelitimiza kwao hivyo hawanidai.”

Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Fountain Gate, Mohamed Muya alisema, usajili wao ndio umeanza hivyo huku akiwataka wadau wa klabu hiyo kutegemea mambo makubwa msimu ujao, kutokana na wachezaji wakubwa na wazoefu waliojiunga na kikosi hicho.

Mbali na ufungaji bora wa Championship, Edgar ameshinda Tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi ya Championship msimu uliopita baada ya kuwashinda Casto Mhagama aliyecheza naye KenGold na Boban Zirintusa wa Biashara United aliyejiunga na Tusker ya Kenya.

Anashikilia rekodi nzuri katika Ligi ya Championship kwani licha ya kuibuka mchezaji bora na mfungaji bora, pia amepandisha timu mbili Ligi Kuu Bara akianza na KenGold aliyoipandisha msimu huu na Mbeya Kwanza imu wa 2021/2022.

Related Posts