Ishu ya Manula yagawa Simba SC, mashabiki wafunguka

SIMBA juzi ilifanya utambulisho wa kikosi kipya cha msimu wa 2024-2025 kwenye kilele cha tamasha la Simba Day, lakini kuna kitu kilijitokeza na kuzua sintofahamu, baada ya kipa namba moja wa timu hiyo, Aishi Manula kutotambulishwa rasmi kama ilivyozoeleka na kutajwa baadaye sana baada ya zoezi la upigaji wa picha.

Hata hivyo, Ofisa Habari wa Simba alitoa ufafanuzi kwamba Manula bado ni kipa wa timu hiyo na ilitokea kwa bahati mbaya kusahaulika kutajwa kwenye utambulisho, ila ni mchezaji halali na atakuwepo kwa msimu ujao, licha ya ukweli hajafanyiwa vipimo vya afya wala hakuwepo kambini jijini Ismailia, Misri.

Kitendo hicho kilichofanywa na Simba kwa Manula ambaye ni kipa namba moja wa timu ya taifa, Taifa Stars imewaibua wadau waliogawanyika, huku baadhi yao wakimtaka kipa huyo kujishusha kwa manufaa ya soka lake kwani wamebaini kuna tatizo baina yake na mabosi wa klabu hiyo.

Makipa wa zamani wa soka nchini, wamezungumza na Mwanaspoti na kusema, wanahisi kuna tatizo baina ya Manula na uongozi wa Simba na kinachoendelea ni kama kumkomoa naye anapaswa kuchutama ili mambo yaendelee la sivyo ataumia zaidi kwani bado ana mkataba na timu hiyo.

Wakongwe hao wamemtaka Manula anusuru kiwango chake kwa kujishusha, ili asitoke nje ya mstari kwani bado ni kipa tegemeo hata kama anawekewa mizengwe na mabosi wake aliokuwa nao kwa misimu saba iliyopita tangu ajiunge na timu hiyo mwaka 2017 akitokea Azam FC.

Kocha wa zamani wa makipa wa Simba, Idd Pazi ‘Father’ alimshauri Manula na meneja anayemsimamia, kumalizana na klabu hiyo kwa hekima vinginevyo, inaweza mchezaji anayeweza kutoka kwenye mstari wa kazi.

“Kuna kitu nimekisoma katika mtandao wa kijamii wa Instagram wa (jina kapuni) kuhusiana kumtafuta mwanasheria ili waende katika vyombo vya soka kama FIFA, watazidi kukoleza moto, kwani Manula ni mchezaji halali wa Simba na hawawezi kuwapangia matumizi na kama analipwa stahiki zake hana la kujitetea,” alisema Pazi na kuongeza; “Namshauri Manula ajishushe kwa afya ya kiwango chake, amtafute aliyekuwa mwenyekiti wa Simba, Hassan Dalali amsafishe kwa mashabiki pia amsaidie kulitatua hilo kwa busara.”

Pazi alisema kama waliotangulia kuitwa Tanzania One ndani ya Simba walitumia busara kumalizana na klabu hiyo, Manula pia afanye hivyo kwani changamoto haziwezi kukosekana katika kazi yoyote.

Kipa wa zamani wa Yanga, Benjamin Haule alisema; “Manula bado anahitajika na Taifa, hivyo kama kuna shida inabidi itatuliwe kwa hekima baina yake na Simba, kwani kwa utambulisho wa wachezaji kusahaulika ni kama hawana programu naye.”

Kipa mwingine wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Ivo Mapunda alisema Manula ajishushe kwa manufaa ya kibarua chake, akisisitiza hakuna mchezaji mkubwa dhidi ya klabu.

“Manula ajishushe, kama kuna jambo aliwakosea viongozi aombe radhi, Simba pia watumie busara kumuadhibu na wasimharibie maisha, nyuma yake ana watu wanaomtegemea, hivyo kibarua kikiota nyasi haitapendeza,” alisema Ivo na kuongeza;

“Ndani ya klabu kuna viongozi ambao wana hekima na busara, waliangalie hilo, yeye siyo wa kwanza kukumbana na hilo, liliwahi kunikuta nyakati za mwisho kuna viongozi walikuwa wanataka niendelee kusalia na wengine wakasema niondoke, mwisho wa yote nikaondoka.”

Akizungumza na waandishi mara baada ya tamasha la Simba Day, Ahmed Ally alisema taarifa hizo za mtandaoni kwamba Manula alikuwa akilazimisha kuondoka kwa mkopo kurudi Azam FC, hazina mashiko kwa vile klabu haiwezi kuruhusu kila mchezaji anayetaka kuondoka ajiondokee bila utaratibu.

“Aishi Manula ni mchezaji wa Simba ana mkataba wa mwaka mmoja na wenye uamuzi wa mwisho juu yake ni viongozi ndio wenye uamuzi wa nini cha kufanya kuhusu yeye, lakini hakuna klabu ambayo itakuwa kila mtu akiomba kuondoka inaruhusu, Aishi ana mkataba na Simba SC,” alisema Ahmed.

Sakata la Manula na Simba lilianza tangu baada ya Kariakoo Dabi ya Novemba 5 ambapo timu hiyo ilifungwa mabao 5-1 na kutajwa miongoni mwa waliotuhumiwa kuihujumu timu sambamba na beki Henock Inonga aliyetimkia FAR Rabat ya Morocco kwa sasa, licha ya ukweli alitokea majeruhi ya muda mrefu.

Balaa likaongezeka baada ya Simba kulambwa mabao 2-1 na Tanzania Prisons na kuanza kuwekwa benchi akimpisha Ayoub Lakred na tangu hapo hajaonekana tena akiwa na timu hiyo hata timu ilipoenda kambini Misri zikiwamo taarifa kwamba alishauomba uongozi umuache arudi Azam FC, lakini amegomewa.

Sio Manula wala menejimenti yake waliopatikana jana kutoa ufafanuzi wa kinachoendelea kwa sasa, kwani simu zao zilikuwa zikiita bila kupokewa.

Kwa sasa Simba ina makipa wanne; Lakred aliye majeruhi, Hussein Abel, Ally Salim na kipa mpya kutoka Guinea, Moussa Camara ‘Spider’ kutoka AC Horoya.

Related Posts