Dar es Salaam. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimelaani kitendo cha kikatili na unyanyasaji wa kijinsia kilichoripotiwa kinachomuhusu msichana (jina halijafahamika), mkazi wa Yombo Dovya, Wilaya ya Temeke, Mkoa wa Dar es Salaam.
Pia kimemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kutoka hadharani na kuonyesha kuchukizwa na tukio hilo la udhalilishaji na ukatili.
Msichana huyo anadaiwa kubakwa na kuingiliwa kinyume na maumbile na vijana watano wanaodai kupitia video hiyo kuwa, wametumwa na afande wakimtuhumu (msichana) kutembea na mume wa mtu.
Kipande cha video kinachosambaa mitandaoni kinaonyesha jinsi vijana hao walivyotekeleza tukio hilo ambalo tayari Polisi na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na wenye Mahitaji Maalumu, Dk Dorothy Gwajima wamelilaani.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Agosti 5, 2024, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga amesema kituo hicho kama sehemu ya jamii imehuzunishwa na ukatili huo na kutaka wahusika wote na aliyewatuma wanakamatwa na kufikishwa mbele ya mkono wa sheria.
Henga amesema matukio kama hayo yakifumbiwa macho yatazidi kujitokeza zaidi katika jamii.
“Vyombo vyote vya ulinzi na usalama viungane katika kuwatambua na kuwakamata wahusika na wachukulie hatua,” amesema.
Pia ametoa wito kwa jamii kupaza sauti pamoja na kushirikiana na vyombo vya usalama kuhakikisha haki inapatikana na hatua kali zinachukuliwa dhidi ya waliohusika.
Amesema tukio hilo ni kosa la jinai la ubakaji wa kundi (gang rape), kwa mujibu wa Sheria ya Kanuni za Adhabu (Penal Code Cap 16) Kifungu kwa 131A, adhabu yake ni kifungo cha maisha.
“Mbali na ubakaji huo, pia kuna makosa mengine ya jinai kama kumwingilia mtu kinyume cha maumbile na kusambaza picha chafu mtandaoni ambalo ni kosa la kimtandao,” amesema.
Aidha, LHRC inampongeza Boniface Jacob, aliyekuwa Meya wa Ubungo, Dar es Salaarn, kwa kutoa taarifa hizo pamoja na Jeshi la Polisi na Waziri Gwajima kwa hatua za awali walizochukua.
“Tunakemea vikali wahusika wa kitendo hiki na tunawaasa wananchi kuacha kusambaza video hizo kwenye mitandao ya kijamii, ili kumlinda msichana huyo,” amesema.
Jana Jumapili, Agosti 4, 2024, Jacob katika ukurasa wake wa X alielezea tukio hilo na kuwaomba viongozi mbalimbali, akiwamo Rais Samia Suluhu Hassan na Inspekta Jenerali wa Polisi nchini (IGP), Camilius Wambura kuchukua hatua.
Mbali ya hao, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Stergomena Tax ameombwa kuingilia kati suala hilo.
Akitoa maoni katika andiko hilo la Jacob, Waziri Gwajima aliandika: “Salaam. Ahsante sana kuniTag. Nimesoma na kuwasilisha kwenye mamlaka yenye dhamana ya kuchunguza na kukamata ambayo ni Wizara ya Mambo ya Ndani. Watatoa taarifa kwa nafasi yao.”
“Aidha, kwa namna yoyote ile, taarifa hii inasikitisha na jambo kama hili halifai, ni la kulaaniwa na haliwezi kufumbiwa macho. Iwapo manusura au aliye karibu naye atasoma hizi taarifa wasiogope, watoe taarifa ili manusura apate msaada haraka, ikiwamo huduma za afya, kisaikolojia na usalama.”
Dakika chache baadaye, Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime alitoa taarifa kwa umma kuzungumzia tukio hilo, akisema wameanza kulifanyia kazi na kulaaniwa, kwa kuwa halikubaliki na ni kinyume cha sheria, maadili ya Mtanzania.
“Jeshi limetoa wito kwa wananchi wote waache kuendelea kusambaza video hiyo, kwani kwa kufanya hivyo ni kosa kisheria, lakini pia ni kitendo cha kuendelea kudhalilisha utu wa binadamu mwenzetu,” amesema Misime na kuongeza:
“Tunatoa wito kwa mwenye taarifa ya kuhakikisha mkono wa sheria unawafikia kwa haraka waliofanya ukatili huu asisite kutusaidia kwa kutupa taarifa au kumpatia kiongozi yoyote yule wanayemwamini kwamba taarifa ikimfikia watu hao watapatikana haraka iwezekanavyo.”