Msemaji mmoja wa jeshi la Uganda Meja Kiconco Tabaro, amesema maafisa hao waliwasili nchini humo kupitia mpaka wa Ishasha wilayani Kanungu kusini magharibi mwa Uganda.
Maafisa hao 98 waliwasili wakiwa na bunduki 43 pamoja na risasi na kupokonywa silaha hizo mara moja.
Maafisa wa polisi wakimbia M23 na makundi mengi ya wapiganaji
Tabaro ameongeza kuwa maafisa hao wa polisi walikuwa wanakimbia mapigano na kundi la M23 na makundi mengine ya wapiganaji pamoja na jeshi la Kongo.
Msemaji huyo wa jeshi pia amesema kuna vurugu nyingi na pia njaa katika eneo hilo la mapigano.
Takriban wakimbizi 2500 wa Kongo wamekimbilia Uganda siku nne zilizopita
Tabaro amesema katika muda wa siku nne zilizopita, takriban wakimbizi wengine 2,500 waliwasili nchini Uganda wakikimbia vurugu zinazoendelea nchini Kongo na kwamba suala linalochangia zaidi hali hiyo ni ongezeko la ghasia na ukosefu wa usalama.
Wanawake wajawazito, wale wanaonyonyesha pamoja na watoto ni miongoni mwa wakimbizi hao.
Kundi la M23 limekuwa likiendesha uasi mpya nchini Kongo tangu mwaka 2022. Ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyoonekana mwezi uliopita na shirika la habari la Reuters, imesema jeshi la Uganda limetoa msaada kwa kundi hilo la waasi linaloongozwa na Watutsi, madai yaliokanushwa na Uganda.
Umoja wa Mataifa waishtumu Rwanda kwa kulifadhili kundi la M23
Kwa muda mrefu, Umoja wa Mataifa umeishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi hao ambao mara kwa mara wamekuwa wakikamata sehemu kubwa za eneo la mashariki mwa Kongo lenye utajiri mkubwa wa madini, madai ambayo Rwanda imeyakanusha.
Soma pia:Waasi wa M23 wanaudhibiti mji mkubwa nchini DRC
Juhudi za jeshi la Kongo kuwarudisha nyuma waasi hao zimeimarika katika muda wa mwaka mmoja uliopita kwa kutumia droni na ndege, ingawa waasi bado wanaongeza maeneo ambayo yako chini ya udhibiti wao.
Mnamo mwezi Juni, M23iliuteka mji wa Kanyabayonga, ambalo limekuwa eneo la kimkakati linalotumika kama lango la kuyafikia maeneo mengine ya mashariki mwa Kongo ya jimbo la Kivu Kaskazini.
Umoja wa Mataifa wakadiria raia milioni 7.2 wamekimbia makazi yao Kongo
Kulingana na makadirio ya Umoja wa Mataifa, mapigano katika eneo la Kivu Kaskazini yamesababisha watu milioni 1.7 kuyakimbia makazi yao na kuifikisha idadi kamili ya raia wa Kongo waliokimbia migogoro mingi kufikia rekodi ya milioni 7.2.