Mabosi wapya Iringa wamepania sana

UONGOZI mpya wa Chama cha Soka la Wanawake Mkoa wa Iringa umesema baada ya kukamilika kwa uchaguzi, shughuli iliyobaki ni kupiga kazi kuhakikisha mpira unachezwa wilaya zote.

Uchaguzi wa chama hicho ulifanyika mwishoni mwa wiki iliyopita na kuwapata viongozi wake watakaokiongoza kwa miaka minne ijayo huku matarajio ya wengi ikiwa ni kuona mabadiliko.

Waliochaguliwa ni Rehema Omary (Mwenyekiti), Amina Karuma (Mjumbe mkutano Mkuu) na Hapiness Ndunguru na Subira Mgimba wakipenya wajumbe kamati tendaji.

Akizungumza na Mwanaspoti baada ya kushinda nafasi ya Mwenyekiti, Rehema alisema uchaguzi ulienda vyema na viongozi waliopatikana walipita kwa haki na kwa sasa ni kuchapa kazi.

Alisema kwa sasa kamati inatarajia kuketi mapema wiki hii kujadili uelekeo mpya, lakini ajenda kubwa itakuwa ni kupanga namna soka la Wanawake litakavyochezwa katika Wilaya zote za Mkoa wa Iringa.

“Uchaguzi uliisha salama, wagombea wote kila mmoja alikuwa na nia ya kuongoza hivyo tunaenda kushirikiana kwa pamoja kusimamia soka la Wanawake kuchezwa maeneo yote ya Iringa,” alisema Rehema.

Katibu Mkuu wa Chama cha Soka mkoani Iringa (IRFA), Adinani Chorobi alisema kutokana na viongozi wote kuwa wapya wanatarajia mabadiliko na utekekezaji wa ahadi zao kusimamia soka kwa Wanawake.

“Sisi upande wetu tutawapa ushirikiano na tuna imani na walioshinda kwa sababu wengi sura ni mpya, tunatarajia mabadiliko hasa soka la Wanawake kuchezwa,” alisema Chorobi.

Related Posts