Mbeya. Umoja wa Wasafirishaji na Wafanyabiashara katika Stendi Kuu ya mabasi mkoani Mbeya, umesema kifo cha aliyekuwa Mkurugenzi wa Kampuni ya mabasi ya Sauli, Solomon Mwalabila ni pigo kutokana na mageuzi aliyofanya katika sekta ya usafirishaji na kusaidia jamii.
Sauli alikutwa na mauti jana Jumapili, Agosti 4 baada ya gari alilokuwa akisafiria kugongwa kwa nyuma na lori la mchanga katika maeneo ya Mlandizi mkoani Pwani na anatarajiwa kuzikwa kijiji cha Godima wilayani Chunya mkoani Mbeya.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Agosti 5, 2024 Makamu Mwenyekiti wa Umoja huo, Noah Mwashela amesema Sauli atakumbukwa kwa mchango wake katika sekta ya usafirishaji ikiwamo kuajiri vijana na kuwaondoa katika makundi maovu ya kihalifu.
Amesema kifo chake kimewapa simanzi na mshtuko mkubwa, kwani licha ya utajiri aliokuwa nao, alikuwa mtu mwenye kuguswa na matatizo ya watu na kutoa mchango wake wa hali na mali.
“Kupitia magari yake vijana wengi walipata ajira na wengine kufanya kazi kwa muda vibarua na kujiingizia kipato, hali ambayo ilileta mabadiliko kwao badala ya kuwa kwenye makundi maovu walikuwa wakifanya kazi.
“Mara ya mwisho kuongea naye ilikuwa kama wiki mbili nyuma, akaeleza namna anavyopambania magari yake yarejee kazini na ninadhani safari yake ya Dar es Salaam ilikuwa ni kushughulikia hilo, lakini ndio hivyo hatunaye tena,” amesema.
Amesema pamoja na mageuzi kwenye eneo la ajira, lakini marehemu alikuwa mtu wa kushiriki katika shughuli za kijamii na muda mwingine kujitolea misaada mbalimbali pale alipoweza.
“Nakumbuka misiba kama minne ikiwamo mmoja wa mtu wa Kilosa (Morogoro) alijitolea sana kuanzia usafiri, jeneza na kutoa Sh300, 000, lakini hata matatizo mengine alijitolea sana hata kama hayupo alifanya namna na kusaidia” amesema Mwashela.
Kwa upande wake Mwenyekiti mstaafu wa umoja huo, Salum Kilowoko amesema Sauli atakumbukwa kwa ushirikiano aliokuwa nao na kwamba ahadi yake ilikuwa ni kurejesha magari yake mapema mwezi huu, lakini mapenzi ya Mungu yameamua hivyo.
Amesema marehemu alikuwa mtu wa tofauti licha ya utajiri aliokuwa nao lakini alitoa mchango kubwa na kwamba kifo chake ni pigo kwa maendeleo ya mtu mmoja mmoja.
“Alitengeneza umoja na ushirikiano alikuwa mtu mwenye kushiriki shughuli nyingi za kijamii na kutoa pesa yake ili kusaidia utatuzi wa changamoto, sisi tumekuwa naye kwa ukaribu mno na alibadilisha hata matajiri wengine katika kuweka umoja,” amesema Kilowoko.
Mmoja wa waliokuwa wafanyakazi wake katika mabasi, John Agustine amesema jina la Sauli hawezi kusahaulika kirahisi kutokana na mchango mkubwa alioutoa kwa vijana akieleza kuwa mchango wake utakumbukwa.
“Nimefanya naye kazi miaka mitatu, alikuwa mtu wa karibu na sisi, anasikiliza kwanza na hakuwa na haraka ya kuamua mambo, kwa ujumla tumepata pigo na tunaenda kuanza maisha mapya,” amesema Augustine.
Dada wa marehemu, Ericka Mwalabila amesema hadi sasa mwili wa marehemu upo Dar es Salaam wakiendelea kushughulikia kwa ajili ya kusafirisha kuupelekwa kijiji cha Godima wilayani Chunya mkoani Mbeya kwa mazishi.
“Bado ratiba hazijakamilika kwa kuwa mwili bado upo Dar es Salaam, tunaendelea kuhangaikia kusafirisha na maziko yatakuwa Chunya kijiji cha Godima, tukikamilisha taratibu zote tutawasiliana,” amesema Ericka