Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amemtaja Theresia Mdee, mama mzazi wa Mbunge wa Viti Maalumu, Halima Mdee kuwa mlezi wa harakati na mtunzi wa imani ya kuitafuta haki katika Taifa.
Theresia alifariki dunia Jumanne Julai 30, 2024, katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, jijini Dodoma baada ya kuugua saratani ya shingo ya kizazi.
Mbowe alikuwa miongoni mwa waombolezaji waliofika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Kibangu Dar es Salaam leo Agosti 5, 2024 kwa ajili ya kumwaga marehemu aliyesafirishwa kwenda mkoani Kilimanjaro.
“Mimi binafsi na wenzangu katika harakati tulimwona mama Halima Mdee kama mlezi wa harakati na kama mtunzi wa imani yetu ya kuitafuta haki katika Taifa, tulimwona kama mama mlezi aliyetuzalia viongozi walio bora sana kwa wakati wote,” amesema.
Amewataka wanafamilia wa Mdee kumshukuru Mungu kwa maisha ya mama huyo.
“Mama ameimaliza safari yake na wakati wote msiba huu uwe funzo, tunapaswa kutafakari vipi kuishi katika maisha haya.”
“Kwa hiyo kila mmoja ana wajibu wa kutafakari safari yetu ya mwisho tunaiandaa vipi na tunaipanga vipi,” amesema.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema msiba huo umekuwa kengele ya kuwakumbusha waumini kujiandaa na safari ya mwisho.
“Mungu amemteua mtu mmoja kugonga kengele ili wengine tukusanyike tupate ujumbe wa Mungu na mtu huyo ni mama yetu aliyelala katika pendo la Roho Mtakatifu.”
“Kwa hiyo huko alikotumwa kugonga kengele, haya yote aliyosema Baba Padri hayamuhusu huyo aliyelala bali yanatuhusu sisi tuliokusanyika hapa ili tuyasikie na kuyaishi,” amesema.
Chalamila amesema atatoa mchango kwa parokia hiyo ili uwe kumbukumbu ya kazi alizofanya marehemu.
“Tunaamini mama amefanya makubwa kiimani na ni mwanafamilia kiimani katika parokia na jumuiya mbalimbali na sisi tutachangia pale ambapo wewe (paroko) utaonyesha mahitaji katika familia.”
“Mimi nitaanza kuwasilisha mchango wangu kwako na ufanye kile ambacho kitaleta alama na kumbukumbu zaidi ya maisha mema ya maisha yake,” amesema.
Naye mume wa marehemu, James Mdee amesema mkewe alimfundisha utoaji wa zaka kwa kanisa na watu wenye mahitaji.
“Ni kweli alikuwa amejijengea tabia, kila anapopata fedha za aina yoyote na kutenga asilimia 10 na kuleta zaka, lakini kwake yeye fungu hilo hakuwa akileta lote kanisani, bali pia kuwapatia wahitaji. Akitokea mtoto mwenye shida ya ada, alikuwa anampatia.
“Katika hilo na mimi alinifundisha, alinihimiza kutoa fungu la 10 na nikifanikiwa anasema kwamba mafanikio haya ni kwa sababu ya ile zaka uliyolipa.”
“Kwa hiyo katika hili tujifunze wote, kama unataka kulipa asilimia 10 mwisho wa mwezi au mwisho wa wiki, huenda ikifika mwisho wa mwezi ukawa hauna tena. Basi tujifunze kuweka kidogo kidogo kwa ajili ya zaka,” amesema.
Akieleza taaluma ya ualimu aliyokuwa nayo marehemu, Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Kijitonyama, Eliona Kimaro amesema mama Mdee amefundisha watu wengi katika utumishi wake akiwajengea msingi.
“Mama yetu alikuwa ni mama na mwalimu tena nimesikia mwalimu wa shule ya msingi, kimsingi Mwalimu wa shule ya msingi ana maana kuliko profesa wa chuo kikuu.”
“Hakuna profesa anaweza kufundisha chochote isipokuwa mwalimu wa msingi hajafundisha. Hata maghorofa yangeenda juu kiasi gani, lakini kama hakuna msingi, hakuna kinachoweza kusimama. Huyu mama ni zaidi ya profesa.
“Watu aliowatengeneza katika hizo shule ambazo amezunguka katika mikoa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wengine leo ni mapadri, maprofesa, madaktari bingwa na wengine ni viongozi wa kisiasa kama ndugu yetu mheshimiwa mkuu wa mkoa,” amesema.
Akitoa salamu za Bunge la Jamhuri ya Muungano, mjumbe wa kamati ya uongozi Vita Kawawa amewataka waombolezaji kuendeleza utamaduni wa marehemu ambao mume wake ameueleza.
“Sisi sote tuna huzuni lakini tunashukuru kwa maisha yake aliyofanya hapa duniani. Kwa kuwa alikuwa mwalimu, amefundisha watu wengi sana na wengine wako hapa,” amesema.
Mbali na viongozi hao, ibada hiyo pia ilihudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hassan Bomboko, viongozi wa siasa, ndugu jamaa na marafiki.