Dar es Salaam. Licha ya Serikali kulifungia Kanisa la Christian Life (CLC), lililoongozwa na Dominique Dibwe maarufu kama ‘Kiboko ya Wachawi’, imebainika kiongozi huyo wa dini anaendelea kutoa huduma hiyo, huku akiomba mamilioni ya fedha kwa waumini wake.
Tofauti na awali, Dibwe ambaye ni raia wa Jamhuri ya Demokrasi ya Congo (DRC) kwa sasa anatoa huduma ya maombezi na kile anachokiita uponyaji kwa njia ya simu, akiomba kulipwa mamilioni hayo kwa waumini wenye matatizo.
Kwa sababu hiyo hiyo ya kutoza fedha kuanzia Sh500,000 kwa waumini wake ili awape huduma ya uponyaji wa kiroho, ndiyo iliyoifanya Serikali ilifutie usajili wa kanisa lake, Julai 25, 2024.
Katika barua ya kufutwa usajili wa kanisa hilo iliyotolewa na Msajili wa Jumuiya za Kiraia, Emmanuel Kihampa ilieleza vitendo hivyo vinakiuka matakwa ya kifungu cha 17 cha Sheria ya Jumuiya, Sura ya 337 kama ilivyofanyiwa marekebisho na Sheria ya Mabadiliko ya Sheria mbalimbali Namba 3 ya Mwaka 2019.
Mbali na kutoza fedha, sababu nyingine za kufutwa usajili wa kanisa hilo zilizotajwa katika barua hiyo ni kutoa mafundisho yenye kuleta taharuki katika jamii na mahubiri ambayo ni kinyume cha maadili, mila, desturi na utamaduni wa Kitanzania.
Nyingine ni kutoa mahubiri yanayodhalilisha watu madhabahuni, kutoa mahubiri chonganishi na kuhamasisha waumini wa kanisa lake kuua watu kwa dhana au tuhuma za uchawi au ushirikina.
Hata hivyo, Mwananchi imethibitisha kuwa Dibwe ameshaondoka nchini kurudi kwao DRC tangu Julai 29, 2024 baada ya kanisa lake kufutiwa usajili.
Akizungumza Agosti mosi mwaka huu, na Mwananchi kwa njia ya simu kuhusu alipo Kiboko ya Wachawi, Msemaji Mkuu wa Idara ya Uhamiaji Tanzania, Paul Mselle amesema uwepo wa kiongozi huyo nchini umekoma baada ya kufutwa usajili wa kanisa lake.
Hata hivyo, wakati haya yakiendelea, video ya mchungaji huyo ilionekana juzi kwenye mitandao ya kijamii akimuomba Rais Samia Suluhu Hassan arejee nchini, akidai hana makosa bali amesingiziwa.
“Nafikiri… namuomba Mama Samia (Rais) kilio cha mwanao Kiboko ya Wachawi kinaweza kufika mahali ulipo, natamani kurudi Tanzania niungane na mke wangu na watoto wangu, pia watu wa Mungu ambao Mungu aliniinua kwa ajili yao,” amesema.
“Watu wamenisingizia vitu vingi, wamenijengea hoja ya masuala ya kutoza viingilio, masuala ya uchonganishi vitu ambavyo mimi sijawahi kushtakiwa na mtu yoyote.”
Msemaji Mkuu wa Idara ya Uhamiaji, Mselle amesema: “Kibali alichokuwa nacho kilikuwa kinaisha Septemba mwaka huu, (bila kutaja tarehe) kilikuwa kwa ajili ya uendeshaji wa kanisa, sasa Serikali ilipofuta kibali cha kanisa lake alitakiwa kuondoka nchini, kwani shughuli iliyomfanya awepo nchini ilikuwa imeondolewa.”
Kutokana na kufungiwa kwa kiongozi huyo wa dini, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda amewataka viongozi wengine wa dini kufuata utaratibu kuondoa migongano isiyo ya lazima.
“Watu wafuate utaratibu kuondoa migongano na mivutano isiyo ya lazima, kanisa hilo si la kwanza kufungiwa na mamlaka husika na yalipofungiwa hali ilikuwa shwari, mpaka sasa hakuna malalamiko yoyote yaliyoletwa kwangu,”amesema Mapunda.
Anavyoendelea kupiga mamilioni
Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kiongozi huyo wa kiroho huko huko alipo anaendelea kutoa huduma za uponyaji, akiomba kulipwa hadi Sh10 milioni.
Mwandishi wa habari hii amepiga simu kwa kiongozi huyo akijifanya mgonjwa kupindukia na kuomba msaada wa matibabu ya kiroho, lakini aliishia kuombwa Sh10 milioni, ili ugonjwa wake upone.
Kinachoshangaza zaidi, Dibwe ameomba kiasi hicho cha fedha kipatikane ndani ya saa 24, akimtishia mwandishi (aliyejifanya mgonjwa) asipoipata ndani ya muda huo angepoteza uhai.
“Nakuona ukienda kufa ndani ya saa 24, maana kuna vitu vinakutembea kutoka kwenye moyo hadi tumboni na namuona mwanamke mmoja ameenda kwa mganga kutoa uhai wako na usipopata huduma hiyo haraka utakufa. Una Sh10 milioni hapo ili upone,” amesema Dibwe kwa njia ya simu.
Dakika chache baadaye mwandishi huyo alimpigia simu tena Kiboko ya Wachawi kumweleza amepata Sh300,000 badala ya Sh10 milioni, lakini kiongozi huyo aligoma akisema kazi ya kuutibu ugonjwa huo ni ngumu na kiasi hicho cha fedha hakitoshi.
Ukiachana na huduma za kiroho, Mwananchi ina taarifa za uhakika za kuendelea kwa ibada katika kanisa hilo, ingawa zinafanywa kwa siri na zinahusisha waumini wanaojulikana.
Sambamba na ibada, waumini hao wanakutana kuelezana kinachoendelea juu ya mchakato wa kurejesha huduma kanisani hapo.
“Huduma zipo, wachungaji wanaendelea kuhudumia, lakini tatizo hujui ni nani unayemuhudumia, unaweza kuona unamsaidia kumbe unamuingiza matatizoni,” amesema mmoja wa viongozi alipozungumza na Mwananchi.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, tayari wameshakata rufaa kwa ajili ya kurejesha huduma za kanisa lao, lakini majibu yanatarajiwa kupatikana ndani ya miezi mitatu (Oktoba mwaka huu).
Ingawa Serikali imefuta usajili wa kanisa hilo, kuna matumaini ya kuendelea kuwepo kutoka miongoni mwa waumini wake.
Hata hivyo, matumaini hayo hayabebwi na imani walizonazo waumini, bali wengine wamelazimika kubaki kanisani hapo Buza kwa Lulenge kwa kukosa nauli za kurejea kwao.
Mkazi wa Chamwino jijini Dodoma, Rose Stephen ni miongoni mwa waumini hao, anayedai anashinda ibadani kusubiri mchungaji huyo arejee.
“Tunaamini kanisa litafunguliwa, hii ni changamoto ya muda tu, tumeshaambiwa ibada itakuwepo, kanisa lilifungwa wakati tupo ndani na hapa mimi nalala chumba cha kukodi, wapo wanaolipa Sh2,000 na wengine Sh3,000,” amesema.
Rose amesema wanalala mchana kanisani hapo kusubiri hatima yao, huku waumini wengine kutoka mataifa mengine wanalala madhabahuni nyakati za usiku na mchana wakiomba.
Muumini kutoka DRC ambaye hushinda kanisani bila kutaja jina lake, amesema hawezi kuondoka kwa sababu ameshalipa fedha kuonana na mchungaji na hana nauli ya kurudi kwao.
“Siwezi kuondoka nitasubiri kwa sababu hela niliikopa kuja kumaliza tatizo langu,” amesema.
Hata hivyo, baadhi ya mashuhuda waliiambia Mwananchi kuwa, wafuasi wa mchungaji huyo hufanya ibada kila asubuhi kuomba kanisa lifunguliwe, huku wakiwalaani wanaowaita wapinzani waliofanikisha huduma hiyo kufungwa.
Wapo waumini wanaohusisha kufungwa kwa kanisa hilo na kile wanachokiita fitina za kidini, kama anavyoeleza mkazi wa Moshi mkoani Kilimanjaro, Samwel Mmbando.
Mmbando, mmoja wa waumini wanaolipa Sh2,000 kulala karibu na lilipo kanisa hilo, bado anaamini ataonana na mchungaji huyo licha ya kukosa Sh500,000.
Amesema alihamasishwa na matangazo kuwa, mahubiri na maombezi katika kanisa hilo hufanyika bure, lakini alipofika alitakiwa kulipa fedha ndiyo aonane na mchungaji huyo.
Mmoja wa mamalishe kanisani hapo, Doris James (si jina halisi) amesema wapo watenda kazi wa kiongozi huyo wanaendelea na ibada, lakini kwa siri na kwamba mke wa ‘Kiboko ya Wachawi’ ndiye anayeratibu yote.
“Tangu asubuhi hadi saa 10 jioni watenda kazi hao walikuwa kwenye ibada, lakini hawaruhusu watu wengine kuingia kwa sababu hawaamini, kama wanakufahamu watakuuzia vitendea kazi ikiwepo mafuta, maji, fulana na vitu vingine ambavyo wanasema mchungaji alishaviombea,” amesema.
Mmoja wa majirani wa mchungaji huyo, aliyejitambulisha kwa jina la Mwalongo, anaeleza alimfahamu Dibwe akiwa anaishi Buza, kabla ya kuhamia Kitonga na wakati huo hakuwa mchungaji, bali alikuwa muumini wa kawaida.
Wakati huo kwa mujibu wa Mwalongo, Dibwe alikuwa akijishughulisha na shughuli mbalimbali na hakuwa na nyumba.
“Mchungaji huyo alikuwa mtumishi wa kawaida kwenye kanisa hilo ambalo pia lilikuwa chini ya mchungaji mgeni kutoka Jamhuri ya Demokrasi ya Congo, baada ya muda walimpa cheo wakati huo mchungaji wa awali aliondoka kanisani hapo,” amesema.
Baada ya cheo hicho kanisani, amesema baadaye Dibwe alitafuta kiwanja Kitonga na kujenga nyumba yake ndogo ya vyumba viwili vya kulala na sebule na alihamia.
Steven John (si jina halisi), naye ni jirani yake wa Kitonga, amesema hakumfahamu kama mchungaji, bali jirani na walimwita kwa jina la Baba Ephrahim.
Kwa mujibu wa John, Dibwe hakuwa anajichanganya na watu, ni mkewe ndiye aliyekuwa anafanya hivyo na alikuwa sehemu ya vikundi vya wanawake.
Amesema Agosti, 2023, Kiboko ya Wachawi alihitaji Sh1 milioni kwa ajili ya kusajili kanisa lake na aliomba akopeshwe na kuahidi angeilipa hata kwa riba kubwa kiasi gani.
Ilikuwa ngumu kupata kiasi hicho, kwa kile anachoeleza John kuwa, uhalisia wa maisha yao ya wakati huo uliwapa ugumu wengi kuamini kama angeweza kurejesha.
Lakini mwanzoni mwa mwaka huu, amesema hali ilibadilika, kwani Dibwe alimwagiza mkewe akanunue kiwanja kwa ajili ya ujenzi na walikinunua kwa Sh7 milioni.
Hakuna aliyejua Dibwe anafanya kazi gani, lakini amesema walishangaa kuona nyumba inakamilika ndani ya miezi miwili na baadaye alianza kununua magari ya kifahari.
“Huku asilimia kubwa tunafahamiana pia na kazi tunazofanya tuliona wenzetu wamebadilika ghafla na hatukujua ni kazi gani wanafanya, maana tunamuona mkewe nyumbani lakini wamekuwa na mafanikio ya haraka,” amesema.
Baada ya kugundua watu hawafahamu, mmoja wa watu anashuhudia kuwa alisimamishwa na mchungaji huyo barabarani na kumueleza kuwa na matatizo na chanzo ni kaka zake watatu.
Kilichoshangaza zaidi, ni kijana mmoja aliyesema aliwahi kusimamishwa na Dibwe akitabiriwa kurogwa na kaka zake, ndiyo maana ana maisha magumu.
Katika utabiri huo, amesema aliambiwa asingepaswa kutembea kwa mguu, alitakiwa kuwa na gari.
“Hakujua kama nina gari nimeliacha nyumbani, hivyo aliponisimamisha aliniambia mimi si wa kutembea kwa miguu na kupanda daladala kinachotokea ni kaka zangu hawapendi maendeleo yangu, hivyo wananiroga,” amesema.
John anasema kilichomtafakarisha kijana huyo aliyetabiriwa na Dibwe ni kwamba hakuwa na kaka bali ni dada pekee, hivyo alishangaa maelezo ya Kiboko ya Wachawi yametoka wapi.
Amesema maelezo hayo yalimtafakarisha, kwa kuwa hana kaka katika familia yake zaidi ya dada zake, hivyo alimtaka afike kwenye kanisa lake lililopo Buza k kufanyiwa maombi na kufanikiwa ili awe tajiri kama wengine.
Hata hivyo, kuna mkanganyiko wa kanisa lililofutiwa usajili na lile alilokuwa akihudumu Dibwe, ikielezwa kiongozi huyo hakuwa katika kanisa la CLC.
Hilo lilielezwa na muasisi na Askofu wa kanisa hilo lenye makao makuu yake Kawe, jijini Dar es Salaam, Peter Lukindo kupitia mtandao wa Istagramu, akifafanua Dibwe alishaondoka CLC tangu Januari 31, 2024.
Ameeleza Dibwe alikuwa mtumishi wa kawaida alipokuwa CLC, lakini baadaye aliomba kuondoka akaanzishe kanisa lake la Kitume la Catholic Apostolical Church (CAC).
“Tulishauriwa na Ofisi ya Uhamiaji Wilaya ya Temeke turudishe kibali chake cha makazi, nasi tulifanya hivyo kwa barua rasmi iliyopokelewa na Uhamiaji Makao Makuu na kugongewa muhuri wa kupokelewa Aprili 3, 2024,” amesema.
Amesema kibali cha Dimbwe kilikuwa kinaisha muda wake Julai 8, 2024 aliambatanisha na barua ambayo Kiboko ya Wachawi aliituma Januari 24, 2024 ya kujitoa kwenye kanisa hilo na kuanzisha kanisa lake.
Barua hiyo ilisomeka, “ninatoa shukurani kwako kwa kunipokea na kufanya kazi kazi ya Mungu nikiwa chini ya uongozi wako kwa muda wa mwaka mmoja na nusu. Kwa muda wote huu tumefanya kazi ya Mungu kwa ushirikiano mkubwa na sasa ninaomba niwe huru, ili niweze kuanzisha kanisa langu litakaloitwa Kanisa la Kitume.
“Ombi hili ninalileta kwako kwa kuwa nimekuwa na maono haya kwa muda mrefu na ninatumaini tutaendelea kushirikiana katika huduma kwa kuwa wote tuna imani moja.”
Kwa taarifa iliyopata Mwananchi baada ya kurudishwa kwa kibali chake, Kiboko ya Wachawi aliomba kibali upya na kupewa kwa miezi mitatu ambapo alilipia dola 6,000 za Marekani (zaidi ya Sh15 milioni).
Mmoja wa majirani zake aliyeomba hifadhi ya jina lake, amesema barua ya kufutwa usajili wa kanisa lake aliipata siku alipokuwa katika sherehe ya siku ya kuzaliwa kwa mtoto wake Ephrahim.
Kinachofanya jirani huyo ahisi hivyo ni kile alichoeleza, tangu ilipomalizika sherehe hiyo hakuwahi kumwona tena Dibwe nyumbani hapo.
Kilichoonekana siku moja baada ya kufutiwa usajili, alikuwa akiingia na kutoka nyumbani hapo na magari ya kifahari huku akisindikizwa na walinzi wake, akiwemo Mwarabu Fighter.
Viti na vifaa vingine, anasema vimeshuhudiwa vikishushwa nyumbani hapo na kwamba mkewe amekuwa akitangaza kuviuza maeneo mbalimbali.
Mke wa dalali aliyemuuzia kiwanja alikojenga nyumba ya ghorofa, (jina lake limehifadhiwa) amesema walidhani mchungaji huyo ni Mtanzania na aliuziwa kama raia wengine.
“Wakati tunamuuzia alisema yeye ni raia wa hapa na hata uuzaji wake ulisimamiwa na Serikali ya mtaa wa huku pamoja na mwenye kiwanja ambaye tulimuuzia awali, kwani alikuwa anahitaji mteja,” amesema.