Hai. Watu wawili wamefariki dunia, akiwamo Mchungaji wa Usharika wa Kimashuku, Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Kantate Munis (42) baada ya gari walilokuwa wakisafiria kugongana na basi kubwa la abiria.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu Agosti 5, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema ajali hiyo ilitokea jana Jumapili Agosti 4, 2024 eneo la Kimashuku, Kata ya Mnadani wilayani Hai, Mkoa wa Kilimanjaro, wakati gari ya mchungaji huyo akikatiza barabara upande wa kulia kuingia kanisani kwake.
Kamanda Maigwa amewataja waliofariki dunia mbali ya Mchungaji Munis ni Laban Kweka (50) ambaye ni mzee wa kanisa hilo, wote walifia eneo la ajali.
“Ni kweli jana kulitokea ajali iliyohusisha gari dogo na basi la abiria lililokuwa likitokea Dodoma kuja Moshi mjini, lilipofika eneo la Kimashuku, Mailisita liligongana na gari dogo na kusababisha watu wawili kufariki dunia na majeruhi,” amesema kamanda huyo.
Mwananchi imezungumza na msaidizi wa Mkuu wa Jimbo la Hai, Dayosisi ya Kaskazini ya KKKT, Mchungaji Dominick Mushi aliyesema ajali hiyo imetokea wakati mchungaji huyo akiingia usharikani Kimashuku.
Amesema Mchungaji Munis alikuwa akitokea kwenye uimbaji wa kikanda Bomang’ombe wilayani Hai na alipofika eneo la Kimashuku ndipo alipopata ajali hiyo.
“Jana tulikuwa kwenye uimbaji wa kikanda, tulipomaliza ndipo mchungaji akatoka kurudi usharikani ambako ndipo anaishi nyumba za usharika na wakati amefika Kimashuku akiingia usharikani akapata ajali.
“Mchungaji alikuwa anaingia usharikani Kimashuku na basi lilikuwa linayapita magari mengine ndipo likaigonga gari ya mchungaji kwa ubavuni na kusereresha hadi kwenye miti,” amesema na kuongeza kuwa gari hilo lilikuwa na watu saba, wengine watano wamepata majeraha.
Mushi amesema majeruhi hao ambao ni mama na watoto wake wamepelekwa Hospitali ya Mawenzi na wengine wawili wamelazwa Hospitali ya Wilaya ya Hai wakiendelea na matibabu.
Mwili wa Mchungaji Munis umehifadhiwa Hospitali ya Rufaa ya KCMC, huku wa mzee wa Kanisa ukihifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Hai kusubiri taratibu za maziko.
Endelea kufuatilia Mwananchi.