Mwenyekiti chama cha wawekezaji wa utalii ajiuzulu

Unguja. Mwenyekiti wa Chama cha Wawekezaji wa Utalii Zanzibar (Zati), Rahim Bhaloo, amejiuzulu nafasi hiyo ikiwa ni miezi mitatu kabla ya kumaliza muda wake wa uongozi wa miaka mitatu. 

Bhaloo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar (ZCT), akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatatu Agosti 5, 2024, ametaja sababu moja tu iliyomfanya ajiuzulu kuwa ni kusumbuliwa na masuala ya kifamilia. 

Amesema; “Ninahisi siwezi sasa kuendelea kutumia nguvu zangu na mali pia kwa ajili ya kazi hii.”

Hivyo, amesema umefika wakati wa kujiweka pembeni na kuuachia uongozi mpya nao ulete mawazo mapya ya kusaidia kukiendeleza chama hicho kwa viwango vya juu zaidi.

“Nimekipeleka chama katika kiwango ambacho kinatambulika na kuthaminiwa na wadau, na sasa ni wakati wa nguvu mpya kuingia,” amesema. 

Wakati wa uongozi wake, Bhaloo anasifiwa kwa kuongeza idadi ya wanachama kutoka 18 waliokuwapo wakati huo na kufikia 500 waliopo sasa.

 Pia anasifiwa kwa kuhakikisha kunakuwa na usimamizi thabiti wa fedha.

Kujiuzulu kwake kunakuja wakati tasnia hiyo inaanza kulazimika kutekeleza ulipaji wa ada ya lazima ya bima ya Dola za Marekani 44 (takriban Sh118,360) kuanzia Septemba Mosi mwaka huu.

Ada hiyo ilitangazwa hivi karibuni na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Saada Mkuya Salum, kwamba utaratibu huu mpya unalenga kuimarisha huduma kwa wageni Zanzibar.

“Bima hiyo itashughulikia mambo mbalimbali ambayo yamekuwa yakiwasumbua wageni kama vile afya, upotevu wa mizigo, ajali, uokoaji wa dharura, upotevu wa hati za kusafiria na hata kurejeshwa kwa mabaki ya watalii wanapofariki,” alisema Dk Mkuya.

Bima hiyo itatolewa na Shirika la Bima la Zanzibar, taasisi inayomilikiwa na Serikali, na haitazingatia iwapo mtu ana sera nyingine ya usafiri kutoka kwingineko.

Kabla ya hapo, bima ya usafiri haikuwa ya lazima nchini Tanzania na nchi nyingine za Afrika Mashariki. Hata hivyo, tangazo hilo limezua wasiwasi katika sekta ya utalii, ambayo ni msingi wa uchumi wa Zanzibar.

Waendeshaji watalii wamehofia kwamba gharama ya ziada inaweza kufanya kisiwa hicho kuwa mahali pa gharama kubwa zaidi.

“Pamoja na nia njema ya Serikali katika kuongeza uzoefu wa wageni katika kisiwa hicho, hii inaweza kuwafukuza wageni wetu kwa sababu ya mlolongo wa mahitaji ambayo wanapaswa kutii,” amesema Sued Ali mwendeshaji watalii.

Wakizungumzia kujiuzulu kwa mwenyekiti huyo baadhi ya wadau wa utalii wamesema: “alipoifikisha taasisi ni mbali kwa hiyo pengo lake linaweza kuoneka lakini huwezi kulazimisha kama ameona kuna jambo halipo sawa akiendelea kuhudumu katika nafasi hiyo,  tumtakie kila la kheri.”

Related Posts