Namna mastaa hawa wanavyoibeba Simba Dk 90

Simba imefanya yao kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa katika tamasha la Simba Day lililoenda kwa jina la Ubaya Ubwela lililofanika Jumamosi na wana Msimbazi wakapata burudani ya aina yake, huku wakishuhudia soka tamu kwa dakika 90 kutoka kwa kikosi hicho kinachojitafuta kwa sasa baada ya misimu mitatu mibovu.

Ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya APR katika mchezo wa kirafiki unaweza usiwe ishu sana, lakini kubwa zaidi ni viwango vya wachezaji wao wapya na wale waliokuwepo tangu msimu uliopita kuonyesha kuwa Simba ya Kocha Fadlu Davids ina watu na kama Wanasimba wataivumilia inaweza kuwapa raha isiyomithilika.

Simba iliyokuwa imeweka kambi katika jiji la Ismailia, Misri kwa takribani wiki tatu kuanzia Julai 8-23 ikijiandaa na msimu wa 2024-2025 na kucheza mechi tatu za kirafiki za ndani.

Katika mechi hizo tatu Simba ilishinda zote, huku nyota wapya wakifanya balaa akiwemo Jean Charles Ahoua, Joshua Mutale, Steven Mukwala na Valentino Mashaka na mashabiki wakawa na hamu kubwa ya kuiona timu hiyo Kwa Mkapa katika kilele cha Simba Day lililoshindikizwa na pambano la kirafiki dhidi ya APR na Ubaya Ubwela ukawanyoosha kwa mabao 2-0.

Wafungaji wa mabao ya mechi hiyo walikuwa ni Debora Mavambo na Edwin Balua katika kipinid cha pili, baada ya kuingia uwanjani kutoka benchi, kwani  kipindi cha kwanza kilimalizika kwa matokeo ya 0-0, lakini kuna kazi nzito ilifanywa na nyota wa kikosi hicho kama Joshua Mutale, Jean Charles Ahoua, Awesu Awesu na Steven Mukwala aliyekosa penalti dakika ya 44 kwa mkwaju wake kula nguzo na kurudia uwanjani.

Hapa kuna uchambuzi wa namna nyota wa Simba walichokifanya katika mchezo huo uliowapa mwanga Wanasimba kuelekea msimu wa 2024-2025 huku wakiwa na kibarua cha mechi ya nusu fainali ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga, Agosti 8, mwaka huu.

Kumbuka katika utambulisho wa kikosi, kipa Aishi Manula hakutajwa wala hakuwepo katika picha ya kikosi cha msimu wa 2024-2025, baadaye Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema walimsahau lakini bado ni mchezaji wao akiwa na mkataba wa mwaka mmoja.

Katika wachezaji 29 waliotambulishwa, Kiungo Yusuf Kagoma na kipa Ayoub Lakred hawakucheza kutokana na kutakuwa fiti wakiuguza majeraha.

Ally Salim alianza kikosi cha kwanza, akacheza kwa takribabani dakika 33, akatolewa baada ya kuonekana kuumia. Katika muda wake huo, alikuwa mtulivu golini ingawa kuna kosa moja alilifanya ilibaki kidogo aruhusu bao baada ya mpira mrefu aliorudishiwa kumpita lakini akauwahi usiingie golini.

Mussa Camara aliingia baada ya kutolewa Ally Salim. Camara ambaye ni usajili mpya kikosini hapo akitokea Horoya AC ya Guinea, ana utulivu na ni mzuri katika utumiaji miguu yake kuuchezea mpira. Alipokuwa golini, alipata shambulizi moja tu ambalo halikuwa la hatari sana. Alitolewa dakika ya 88 baada ya kucheza kwa takribani dakika 55. Akaingia Hussein Abel.

Hussein Abel ni miongoni mwa makipa wanne waliotambulishwa mbele ya mashabiki wa Simba kuelekea msimu ujao. Mwingine ni Ayoub Lakred ambaye hakucheza kabisa kutokana na kuuguza majeraha. Abel alimalizia mchezo ambapo kwa muda aliocheza alionyesha bado anahitaji kuaminiwa golini katika msimu wake wa pili kikosini hapo baada ya kuonyesha utulivu.

Shomari Kapombe alitumia dakika 45 za kwanza kudhihirisha Simba walifanya jambo sahihi kumuongezea mkataba wa kuendeleza kuitumikia timu hiyo kwani ni yuleyule katika kupiga krosi, kukaba na kupandisha mashambulizi alifanya kwa usahihi mkubwa. Ameonyesha ukongwe wake ambao vijana wanaocheza nafasi yake wanaweza kuendelea kujifunza.

Kelvin Kijili ni usajili mpya, aliingia wakati Kipindi cha pili kinaanza akichukua nafasi ya Kapombe. Kasi yake katika kupandisha mashambulizi ni silaha anayoitumia, ndiye aliyesababisha bao la pili baada ya kumkimbiza mlinzi wa APR hadi karibu na boksi, akafanyiwa faulo iliyotumiwa vizuri na Edwin Balua kufunga.

Mohamed Hussein huu ukiwa ni msimu wake wa 11 ndani ya Simba, ndiye nahodha wa kikosi hicho kwa sasa, kutokea mbavu ya kushoto ameendelea kuwa bora katika kuzuia na kushambulia, dakika zake 66 zilitosha kukonga nyoyo za Wanasimba.

Valentine Nouma aliingia baada ya kutoka kwa Mohamed Hussein, wawili hao wanacheza nafasi moja. Nouma ni usajili mpya na katika dakika takribani 26 alizocheza ameonyesha kuna kitu ndani yake. Muda mchache tu baada ya kuingia, alipata fursa ya kupiga shuti lililolenga lango lakini kipa wa APR akawa imara na kudaka.

Che Malone wanamuita Ukuta wa Yeriko, huu ni msimu wake wa pili ndani ya Simba, alicheza kwa dakika 70 na kulinda vizuri eneo lao la ulinzi, alifanya washambuliaji wa APR wasilete hatari yoyote langoni mwao kwani alikuwa akinusa haraka hizo hatari na kuzizuia.

Hussein Kazi huu ni msimu wake wa pili, aliingia dakika ya 70 baada ya kutoka Che Malone, bado anaendelea kupambania namba yake ndani ya Simba, alizitumia vizuri dakika zake 20 kulinda wasiruhusu bao.

Chamou Karaboue alicheza vizuri sana beki huyu ambaye ni usajili mpya akishirikiana na Che Malone. Dakika zake 70 zilimtosha kudhihirisha Simba haikufanya makosa kumsajili kwani amekuwa mtulivu akiwa na mpira, ubabe wake katika kukaba uliwatisha washambuliaji wa APR ambao walikuwa wakicheza mbali na eneo la hatari la Simba.

Che Malone na Chamou inaonekana ndiyo pacha itakayotumika katika ulinzi wa kati kikosini hapo baada ya msimu uliopita Che Malone kucheza na Henock Inonga Baka ambaye ameuzwa.

Abdulrazack Hamza naye usajili mpya, alicheza kwa dakika 20 sambamba na Hussein Kazi akichukua nafasi ya Chamou, alifanya faulo mbili zilizoonwa na mwamuzi Ramadhan Kayoko. Bado ana muda wa kuipambania nafasi kikosi cha kwanza.

David Kameta anafahamika kama ni beki wa kulia, lakini juzi alipoingia kuchukua nafasi ya Omary Omary alionekana kucheza eneo la kiungo mkabaji, alikuwa mtulivu kwa takribani dakika mbili alizocheza kufika tisini sambamba na zile tano za nyongeza.

Fabrice Ngoma alicheza kwa dakika 45, eneo la kiungo cha ukabaji alifanya kazi yake vizuri ingawa muda wake akiwa uwanjani wapinzani walikuwa wakifika sana golini kwa Simba.

Debora Fernandez ni usajili mpya, dakika moja tu tangu aingie uwanjani mwanzoni mwa Kipindi cha pili, aliachia shuti kali akiwa nje ya 18 na kufunga bao la kwanza. Kumbuka shuti hilo lilikuwa la kwanza ‘on target’ kupigwa na Simba katika mchezo huo.

Joshua Mutale wanamuita SGR, alianza winga ya kushoto, alikuwa akiingia ndani anapopokea mpira ikiwa ni katika kupeleka mashambulizi, wakati mwingine alihama kwenda winga ya kulia. Ana kasi ambayo kama mabeki wa timu pinzani wasipokuwa makini wanaweza kujikuta wakimchezea sana faulo kwani hata juzi yeye ndiye aliyesababisha penalti baada ya kukwatuliwa eneo la hatari. Dakika zake 66 zilimtosha.

Mzamiru Yassin katika eneo la kiungo alianza na Ngoma, alikuwa akihamisha mipira kutoka upande mmoja kwenda mwingine, naye hana mabadiliko sana na ilivyokuwa msimu uliopita, alitumika kwa dakika 45 akatolewa akiwa na kadi moja ya njano.

Awesu Awesu ni Kiungo mpya wa Simba akitokea KMC, alianza kikosi cha kwanza akicheza dakika 45 pekee. Awesu alianza winga ya kulia kuna wakati alipishana na Mutale akaenda winga ya kushoto.

Achana na hilo, pia akawa anapishana na Ahoua yeye akaenda kucheza namba 10, pia alicheza kiungo cha kati, hiyo yote ni kuonyesha kwamba ana uwezo wa kucheza popote katika eneo la Kiungo cha ushambuliaji.

Awesu ni mzuri katika kukaba, alionyesha hilo mara kwa mara alipokuwa akipokonya mipira akiingia uvunguni mwa wapinzani.

Kibu Denis aliingia baada ya kutoka Mutale, hakuonyesha cheche zake hiyo inatokana na kutokuwepo katika maandalizi ya msimu na wenzake kule Misri, aliungana nao waliporejea Dar. Ana kazi ya kufanya kuingia kikosini.

Augustine Okejepha ni usajili mpya, alipoingia Kipindi cha pili kilipoanza akishirikiana na Debora Fernandes Mavambo waliifanya Simba kuwa hatari eneo la katikati, wapinzani wakiwa hawapandi sana mbele wanaishia kuchezewa mpira eneo lao.

Omary Omary ametokea Mashujaa, unaweza kusema hakuwa na siku nzuri juzi kwani alipoteza kirahisi pasi mbili zilizomfanya Kocha Fadlu Davids kumpa dakika 18 pekee kuanzia dakika ya 70 alipoingia kuchukua nafasi ya Ahoua na kutolewa dakika ya 88. Huyu ni Kiungo, asipokaza anaweza kuishia sana benchi.

Edwin Balua ndiye mfungaji wa bao la pili kwa Simba, aliingia Kipindi cha pili kilipoanza kuchukua nafasi ya Awesu. Bao lake halikunishangaza sana kwani yule Edwin Balua wa msimu uliopita, ameendelea palepale alipoishia.

Mabao ya faulo za moja kwa moja msimu uliopita aliwafunga Simba wakati anaitumikia Tanzania Prisons kabla ya kusajiliwa kikosini hapo dirisha dogo. Kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, alimtesa sana Ally Salim akichagua engo ya kwanza kuweka mpira nyavuni, akarudia tena wakati Simba ikicheza dhidi ya Namungo, kufunga kwa staili hiyohiyo.

Ameondoka Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’ ambaye alikuwa akiongoza kupiga faulo ndani ya Simba, sitashangaa kuona msimu huu Balua akipewa jukumu hilo kwani ni mtaalamu sana wa mipira hiyo.

Ladaki Chasambi naye alipata nafasi kidogo ya kuonyesha uwezo wake ingawa kwa takribani dakika saba alizocheza, ilionekana kawaida.

Jean Charles Ahoua alitumika kwa dakika 70, alipangwa kuanza namba 10, lakini alikuwa anashuka sana chini kuja kuchukua mipira na kuipeleka mbele. Ni mzuri kupiga mashuti na kusaidia mashambulizi.

Steven Mukwala dakika zake 57 alizitumia vizuri ingawa alikosa penalti ambayo aliipiga kiufundi sana, ikala nguzo na kurudia uwanjani.

Ukiachana na penalti, jamaa huyu ni straika kweli, alionyesha upambanaji uliodhihirisha kwamba kama hatakuwa na mabadiliko huko mbele, anaweza kuisaidia sana Simba.

Ubora wake upo katika kuwakimbia walinzi kwani alisamamishwa namba tisa, akawa hatulii katikati kutokana na kukabwa sana, akawa anatanua pembeni kuwavuta walinzi wa APR kitu ambacho kilikuwa kikiacha mianya iliyokuwa ikimfanya Mutale kupita kirahisi. Mawasiliano yao bora sambamba na Mutale yanaweza kuibeba Simba katika eneo la ushambuliaji.

Valentino Mashaka ndiye aliingia kuchukua nafasi ya Mukwala, lakini alitumia dakika 20 pekee akatika dakika ya 77, licha ya kupata muda mchache, lakini aliwasumbua sana walinzi wa APR hadi wakamchezea faulo ambayo pengine ndiyo ilimtoa nje baada ya kuonekana amepata maumivu.

Freddy Koublan ameletewa washindani katika eneo la ushambuliaji, uwepo wa Mashaka na Mukwala inaonyesha eneo hilo kuna kazi kwelikweli. Dakika zake takribani 13 alizocheza hakuonyesha makali sana.

Kocha Mkuu wa APR, Novic Darco, amesema: “Simba ni timu imara sana, wapo vizuri kifiziki wanafahamu namna ya kukaa kwenye nafasi kila wakati na kutumia nafasi. Simba hii imetupa mchezo mzuri sana.”

Kwa upande wa Kocha wa Simba, Fadlu Davids, amesema: “Mapumziko nilikaa na wachezaji wangu kuwapa mbinu za kwenda kufanya baada ya kipindi cha kwanza kuonekana tukicheza taratibu mpira hauendi sana mbele, kipindi cha pili tuliwaweka wapinzani kwenye matatizo baada ya kuwapa presha, tukashinda.”

Related Posts