Ongezeko magonjwa ya zinaa tishio la ugumba

Morogoro/Dar. Wataalamu wa afya wameonya kuwa jamii inapaswa kuenenda na ngono salama, kwa kuwa ongezeko la magonjwa ya zinaa nchini LInatishia usalama wa afya ya uzazi hasa kwa vijana, kwani yanachochea tatizo la ugumba.

Wakitaja athari kwa mwanamke, wamesema huziba mirija ya uzazi, huku magonjwa kama kisonono yakiathiri njia ya kupitisha mbegu kwa mwanaume na uzalishaji na ubora wa mbegu.

Matumizi ya kinga ‘kondom’ yametajwa kuwa mwarobaini wa tatizo hilo, huku wakitaja kupungua kwa matumizi ya mipira hiyo ya kike na kiume miongoni mwa jamii.

Ripoti ya Mei 21 2024 iliyotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) inaashiria ongezeko la magonjwa ya zinaa maeneo mengi, huku kukiwa na changamoto za maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) na homa ya ini katika afya ya jamii na kusababisha vifo vya watu milioni 2.5 kila mwaka.

Daktari bingwa wa magonjwa ya kinamama kutoka Hospitali ya misheni Ifakara, mkoani Morogoro, Elias Kweyamba amesema magonjwa ya zinaa yana athari hasi katika afya ya uzazi akisisitiza ni muhimu kutibiwa mapema ili kupunguza athari hizo.

“Magonjwa ya zinaa kama kisonono yanaathiri njia ya kupitisha mbegu ya mwanaume, lakini pia yanaweza kuathiri uzalishaji na ubora wa mbegu hivyo kumfanya mwanaume kupata tatizo la ugumba,” amesema na kuongeza;

“Kwa mwanamke wale vijidudu huenda kuathiri mirija, sehemu ambayo mbegu ya kiume na yai la kike vinakutana ndipo atengenezwe mtoto. Sasa mtu anapopata magonjwa ya zinaa hupata maambukizi kwenye mirija ya uzazi na kuna uwezekano wa mirija kuziba.”amesema Dk Kweyamba kwenye semina ya waandishi wa habari iliyoandaliwa na Chama cha Uzazi na Malezi Bora Tanzania (Umati)

Akizungumzia athari za ugonjwa wa kaswende amesema si rahisi kusababisha makovu na badala yake husababisha mimba kutoka kwa sababu huathiri ukuaji wa mtoto, viungo vyake hadi moyo wa mtoto.

“Mtoto anapokuwa tumboni anapata athari, anaweza kuzaliwa na changamoto ya moyo, kaswende huchochea baadhi ya kemikali kwenye mfumo wa mama inayosababisha mimba itoke kama ilivyo VVU, maambukizi yoyote kuna kemikali huzalishwa na zinaingilia mfumo wa ukuaji wa mtoto, vichocheo vinavyoshikilia ujauzito, hivyo unaweza kutoka,” amefafanua.

Akizungumza na Mwananchi Mei mwaka jana,  Mkuu wa kitengo maalumu kinachoshughulikia matatizo ya uzazi Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini KCMC,  Dk Thomas Kakumbi alisema tatizo la ugumba linazidi kuongezeka nchini,  kwani hospitali hiyo inapokea wagonjwa kati ya 25 hadi 30 kwa wiki wakiwamo wanaume wakiwa na tatizo hilo.

Nchini Tanzania ongezeko la maambukizi ya magonjwa ya ngono na homa ya ini, yameifanya Wizara ya Afya kuboresha Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi na kuja na Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi, Magonjwa ya Ngono na Homa ya Ini (NASHCoP).

Takwimu za Wizara ya Afya zinaonyesha idadi ya waliopimwa na kubainika kuwa na kaswende pekee ilipanda kutoka 16,015 mwaka 2017 hadi 26,592 mwaka 2019. Kaswende iligundulika zaidi kwa wajawazito waliopimwa na kupata matibabu na idadi yao iliongezeka kutoka 10,049 hadi 18,298 katika kipindi hicho.

Takwimu za matibabu ya kaswende miongoni mwa wanawake waliogunduliwa wanaohudhuria kliniki, ilikuwa asilimia 17.3, 22.4 na 25 katika mikoa ya Tanga, Dodoma na Dar es Salaam na 100 katika mikoa ya Kagera, Geita, Mara na Simiyu.

Pamoja na magonjwa ya zinaa, Dk Kweyamba ametaja uhamishaji wa bakteria wa kutoka mdomoni kwenda njia ya uke kupitia mate na bakteria wa njia ya haja kubwa kwenda ukeni limekuwa miongoni mwa matatizo yanayosababisha ugumba kwa mwanamke.

Akifafanua zaidi amesema kwenye mirija ya uzazi ndiko mbegu ya kiume na yai vinakutana na kutengeneza mtoto, “Kama umeziba mtoto hatapatikana, utafanya vyovyote uwezavyo hutapata mimba sababu mirija imeziba. Sababu ni  maambukizi ya bakteria hao walitoka sehemu ya nyuma kuja ya mbele na hii ni mojawapo ya PID nyingi kwa sasa.”

Mtaalamu wa Afya ya Jamii, Dk Ali Mzige amesema magonjwa yote ya zinaa yana uwezekano wa kuchangia ugumba kutokana na athari ya magonjwa hayo yasipotibiwa ipasavyo.

“Inashauriwa kila ugonjwa wa zinaa anayeugua atibiwe yeye na mwenza wake, pamoja na kwamba yapo magonjwa ya zinaa zaidi ya 30 yakiwamo kisonono, kaswende, pangusa na klamedia ni muhimu kutibu kwa wakati, japokuwa mengine ni ngumu kuonyesha dalili mapema,” amesema.

Dk Mzige amesema korodani za mwanaume zikiathirika hushindwa kutengeneza mbegu za kiume na kupata na madhara yake ni kupata kovu linalosababisha mbegu za kiume kushindwa kutoka.

Hata hivyo amesema kaswende ni mbaya zaidi kwani husambaa mwili mzima na kufika mpaka kwenye ubongo na mara nyingi athari zake ni kumletea mgonjwa matatizo ya afya ya akili.

“Wengine wanaweza kupata magonjwa ya zinaa kama kisonono kwenye koo na kaswende kwenye ulimi, haya magonjwa mengine ya zinaa baadaye yanaleta saratani hasa ya njia ya haja kubwa au ya uke na nyakati zingine mtoto kuzaliwa na matatizo ya macho,” amesema.

Kauli ya wataalamu hao, inakwenda sambamba na ripoti ya utekelezaji wa mikakati ya sekta ya afya duniani juu ya maambukizi ya VVU, homa ya ini na magonjwa ya ngono ya mwaka 2022–2030 ya WHO inayoonyesha ongezeko la magonjwa ya zinaa hususan nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Ripoti hiyo inaonyesha magonjwa manne ya zinaa yanayotibika yaani kaswende, kisonono, klamidia na trichomoniasis, husababisha zaidi ya maambukizi milioni moja kila siku duniani.

Related Posts