PUMZI YA MOTO:Kampuni zetu za kimataifa ziwaunge mkono wasanii

RAIS Samia Suluhu Hassan amekuwa mstari wa mbele kuunga mkono wasanii wetu ili waweze kutoboa kimataifa.

Ziara yake ya Korea Kusini aliyofuatana na wasanii wa maigizo ni mfano halisi wa upendo wa mama kwa wanawe wasanii.

Lakini iko haja ya taasisi nyingine za serikali anazoziongoza ziongeze juhudi katika kumuunga mkono katika harakati hizi.

Nitatolea mfano Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), ambayo ndiyo — national carrier — yaani ndiyo mbeba bendera wa taifa.

Ukipanda ndege za ATC ni vyema ukajiona umepanda ndege ya kampuni ya nyumbani na sio ya nchi za mbali huko. Kampuni nyingine za ndege huweka kazi za sanaa za wasanii wao kama kiburudisho kwa abiria, hasa kwa safari ndefu.

Nasi kampuni yetu inaweza kututangaza katika hili. Ni vyema nyimbo za wanamuziki wa Tanzania na filamu za waigizaji wa Tanzania zipewe nafasi.

Isiwe kazi zote za sanaa utakazokutana nazo ni zile za ng’ambo, hasa za Kimarekani. Kwa wale ambao hamjanielewa, ni hivi, kwenye ndege kila abiria huwa na skrini yake ya TV inayokaa nyuma ya kiti cha mbele yake.

Skrini hii ni maalumu kwa ajili ya abiria kukuburudisha kutokana na urefu wa safari. Hebu fikiria safari ya kutoka Dubai hadi Dar es Salaam, saa tano hewani.

Bila kuwa na kitu cha kukuburudisha unaweza kuchoshwa sana na safari. Skini hiyo ndani yake huwekwa vitu mbalimbali kwa mfano filamu, muziki, makala, vipindi vya TV mbalimbali na kadhalika.

Abiria huchagua anachokipenda na kukiangalia njia nzima na kuburudika. Ndege za kampuni nyingine hasa zile kubwa kabisa utakuta wameweka kazi za wasanii mbalimbali duniani, lakini bila kusahau kazi za wasanii wa nchi husika.

Sasa ATC kwa vile ni kampuni yetu inapaswa kutilia mkazo jambo hilo. Tunawategemea waongeze nguvu katika kuweka kazi za wasanii wetu ili kuzitangaza kwa sababu ndege hizi zinatumiwa na watu wa mataifa mbalimbali.

Kuweka kazi za wasanii wa Ulaya na Marekani siyo mbaya kwa sababu wao ni ‘brand’ ya dunia, lakini za wasanii wa kwetu ni vyema zikapewa nafasi kubwa pia.

Kama chakula wanaweka cha kwetu basi na kazi za wasanii wetu inawezekana pia hasa katika kipindi hiki ambacho mama anaupiga mwingi kwa wasanii.

Taasisi zetu ikiwamo ATC zisikubali kuishia kutoa pesa kwa ajili ya kuwalipa wasanii wa nje na kuwaacha wa ndani. Hili ni eneo ambalo wanaweza kufanya vyema zaidi pia. Wanafanya kazi nzuri sana, huduma nzuri na hata wahudumu ni wazuri sana mashaallah, na wanapendeza sana kwa mavazi yao.

Tukishindwa katika hili, itakuwa ni aibu kubwa kuwa na vyombo vya kitaifa ambavyo havijivunii fahari ya taifa.

Sote tunajua kwamba kampuni yetu imetoka mbali na inapitia changamoto, lakini hiyo ndiyo biashara. Na biashara hutaka uwekezaji na huo ni mowajawapo wa uwekezaji.

Biashara ya ndege inataka huduma nzuri sana kwa wateja, ikiwemo burudani. ATC inatakiwa iwekeze pia eneo hilo kwa sababu ni muhimu sana na liko ndani ya uwezo wao.

Kwa taasisi zinazofanya kazi na wageni wa kimataifa na zinaona filamu zetu hazina kiwango cha kuburudisha wateja wao, ni vyema wasaidie katika utayarishaji wake ili kupata kazi bora zenye viwango. Wasanii wetu wasipoungwa mkono na taasisi zetu hawawezi kufika mbali hata kama mama atawachukua wote na kuwapeleka HOLYWOOD.

Mama anafanya mengi lakini anatuhitaji kila mmoja wetu tumsaidie kazi ili kulifanikisha lengo ambalo ni maendeleo ya nchi yetu.

Related Posts