Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesisitiza umuhimu wa kuongeza thamani ya rasilimali za kilimo na madini ndani ya nchi. Akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa CCM Ifakara, wilayani Ifakara, mkoani Morogoro, siku ya Jumatatu, Agosti 5, 2024, Rais Samia alieleza kuwa wawekezaji wanapanua viwanda ili kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na madini hapa nchini.
“Ndugu zangu, tumekubaliana kwamba rasilimali zilizopo nchini ziwe za mazao ya kilimo au madini lazima yaongezwe thamani hapahapa nchini. Na ndiyo maana wawekezaji hawa wanatanua viwanda ili kuongeza thamani hapa,” alisema Rais Samia. Pia, alibainisha kuwa eneo la Ifakara lina wawekezaji wakubwa wa madini ambao wanahimizwa kuanzisha viwanda vya kuongeza thamani ya madini wanayochimba ili kutoa ajira kwa Watanzania.
Rais Samia aliongeza kuwa uongezaji wa thamani wa viwanda unahitaji nishati na umeme wa uhakika. “Tunajua kwamba uwekaji wa thamani wa viwanda unahitaji nishati, unahitaji umeme na ndiyo maana jana nilipita kuangalia kazi iliyofanyika kwenye kituo cha kupoza umeme cha Ifakara,” aliongeza.
Kauli ya Rais Samia imekuja wakati nchi ikiwa kwenye harakati za kuboresha sekta za kilimo na madini kwa kuhakikisha rasilimali zinatumika ipasavyo na kuleta manufaa kwa wananchi. Rais alihimiza umuhimu wa kuendelea kuboresha miundombinu ya nishati ili kuunga mkono juhudi za kuongeza thamani na kutoa ajira zaidi kwa Watanzania.
#KonceptTvUpdates