Straika wa Mali atua Coastal Union

DAUDI ELIBAHATI: TIMU ya Coastal Union imekamilisha uhamisho wa mshambuliaji raia wa Mali, Amara Bagayoko kutoka Klabu ya ASKO de Kara ya Togo.

Mshambuliaji huyo msimu uliopita akiwa na ASKO de Kara, Bagayoko alikuwa mfungaji bora wa Ligi ya Togo baada ya kufunga jumla ya mabao 19, huku akichezea timu mbalimbali za FC Nouadhibou ya Mauritania, Al-Hala SC ya Bahrain na Djoliba AC Bamako ya kwao Mali.

Mwanaspoti linafahamu kwamba Bagayoko mwenye miaka 25, amesaini mkataba wa miaka miwili wa kukichezea kikosi hicho cha jijini Tanga ambacho kinajiandaa kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza tangu kiliposhiriki michuano ya kimataifa mwaka 1989.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Coastal Union, Abbas Elsabri alisema lengo lao ni kutengeneza timu imara itakayoleta ushindani.

“Lengo letu ni kutengeneza timu imara itakayoleta ushindani msimu ujao kwa sababu kama ambavyo unafahamu tuna mashindano ya ndani na ya kimataifa,” alisema.

Kuhusu maandalizi ya timu hiyo yanayoendelea kisiwani Pemba, Elsabri alisema, wachezaji wote wako katika ari kubwa kwa ajili ya mchezo wao wa nusu fainali ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC, utakaopigwa Agosti 8 mwaka huu kwenye Uwanja wa New Amaan Complex Zanzibar.

“Kambi yetu itaendelea hapa Pemba hadi siku ya mwisho ya mchezo wetu na Azam FC, hivyo hatuna ratiba ya kurudi jijini Tanga kwa sasa, kikosi chetu kimejipanga vizuri kuhakikisha kinafanya vizuri licha ya kutambua ugumu uliopo mbele yetu,” alisema.

Related Posts