Tanesco wasema maboreshaji mita za luku kukamilika Novemba

Na Nora Damian, Mtanzania Digital Dodoma

Shirika la Umeme (Tanesco) limesema maboresho yanayoendelea katika mfumo wa kulipia umeme kadiri mteja anavyotumia (Luku) yatakamilika Novemba 24 mwaka huu.

Shirika hilo linafanya maboresho hayo kwa lengo la kuhakikisha mfumo huo unaendana na viwango vya kimataifa na kuongeza usalama wa mita hizo.

Akizungumza Agosti 4,2024 Meneja Masoko wa Tanesco, Sylivester Matiku, amesema wameshapita katika mikoa na kanda mbalimbali na kwamba hivi sasa wako katika Kanda ya Dar es Salaam.

Matiku alikuwa akizungumza na Waandishi wa habari kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo kwenye Maonesho ya Wakulima na Wafugaji (Nanenane) yanayofanyika kitaifa jijini Dodoma.

“Katika uboreshaji wa mita kutakuwa na token ambazo zitakuwa na namba moja mpaka tatu, namba moja mpaka mbili ni kwa ajili ya maboresho ya mita na namba tatu ni kwa ajili ya kuingiza umeme ambao umenunua.

“Tulikuwa na mita lakini zinaenda zinabadilika, tunataka wananchi wasipate shida waweze kuendana na hali halisi na hadi itakapofika Novemba 24 mwaka huu tutahakikisha kwamba watu wote wameshaingizwa kwenye uboreshaji wa mita,” amesema Matiku.

Amesema katika maonesho hayo pia wanatoa elimu kuhusu matumizi bora ya umeme kwa sababu wananchi wengi wana hofu kwa kudhani ni ghali na kuwataka kuacha dhana hiyo kwani kwa sasa vifaa vinavyotumia umeme vimeboreshwa na kutumia gharama ndogo.

“Nia ya serikali ni kuhakikisha kwamba tunapunguza uharibifu wa mazingira kwa kukata miti na kuhakikisha mvua zinapatikana kwenye vyanzo vya maji kwa sababu maji ni moja ya vyanzo vyetu vya umeme. Tunayo majiko ya kufundishia na tunawaambia wananchi wasione kutumia umeme ni ghali kama ilivyokuwa mwanzo bali teknolojia imeboreshwa, unaweza kupika hata maharage kwa kutumia gharama kidogo isiyozidi Sh 300,” amesema Matiku.

Related Posts