TANESCO yatumia Maonesho ya Nane Nane kutoa elimu kwa wananchi

Meneja wa Masoko wa TANESCO Sylvester Matiku akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusiana na utendaji wake katika kuhudumia wananchi kwenye Maonesho ya Kilimo Kitaifa Nane Nane yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.
Na Chalila Kibuda ,Michuzi TV Dodoma
SHIRIKA  la Umeme Tanzania (TANESCO) limesema kuwa wananchi watumie fursa ya Maonesho ya Kilimo Nane Nane kupata elimu kuhusiana na utendaji wa Shirika katika miradi mbalimbali inayotekelezwa nchini yenye lengo kuboresha upatikanaji wa Umeme.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 4,2024 katika viwanja vya Maonesho Kilimo Kitaifa Nane Nane yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, Meneja Masoko wa TANESCO Sylvester Matiku amesema wameshiriki katika maonesho hayo wakiwa kama taasisi muhimu katika kuchochea ukuaji wa uchumi katika sekta ya kilimo kwani uzalishaji katika uchakataji na usindikaji wa mazao unahitaji Umeme.
“Wananchi wakitumia Maonesho haya katika kupata elimu juu utendaji wa Shirika la TANESCO kuwa mabalozi katika wa kutoa elimu juu ya matumizi Sahihi ya kutumia Nishati ya Umeme”amesema Matiku.
Amesema Shirika kwa sasa lina Mradi mkubwa wa Bwawa la Nyerere ambapo wananchi wanapaswa kujifunza faida ya Bwawa hilo ambalo limekamilika kwa asilimia 98.33.

Aidha matiku ameongeza kuwa wanaendelea na maboresho ya mita za Luku na zoezi hilo wanatarajia kulikamilisha Novemba mwaka huu hivyo amewataka wananchi kuhakikisha wanafanyia marekebisho mita zao ili waendelee kutumia huduma bora zinazotolewa na Shirika.

Matiku amesema kuwa kutokana na maboresho katika kutumia teknolojia kumesaidia kupunguza matumizi ya umeme kwani sasa hivi vifaa vya kutumia umeme vimeboreshwa zikiwemo Balbu zinazotumia umeme kidogo.
“Tunaomba wananchi waje kwa wingi wajifunze pia kujilinda(usalama) wakati wa kutumia umeme.
Aidha amesema wananchi watumie Mawasiliano ya Tehama ya kujihudumia wakiwa popote pindi wanapopata changamoto.
Amesema Serikali inawekeza kwenye uzalishaji wa umeme ili uwe wakutosha nchini lakini pia hata kuuza nchi jirani ili pia kuchochea ukuaji wa uchumi.
Matiku amesema nchi ina umeme wa kutosha na lengo la Serikali ni kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa na huduma hiyo.
Meneja Masoko ametoa rai kwa wananchi pindi wanapoona umeme umeshawafikia kwenye maeneo yao wachangamkie fursa ya kuunganisha katika nyumba zao.
Hata hivyo amesema nia ya Serikali kuona kila mwananchi anafikiwa na huduma ya Umeme kwa ustawi wa uchumi wa Taifa.

Related Posts