Uingereza kuendelea kufadhili miradi ya Ukimwi nchini

Moshi.Balozi wa Uingereza nchini Tanzania,  David Concar amesema nchi yake itaendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali ya Tanzania katika kupambana na ugonjwa wa Ukimwi, ili kutimiza malengo  ya kimataifa ya muda wa kati na mrefu,  kuona hakuna maambukizi mapya, unyanyapaa na vifo vinavyohusiana  na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU).

Balozi Concar amesema hayo wakati wa mapokezi ya wapanda Mlima Kilimanjaro 71 walioshiriki kampeni ya kila mwaka ya GGM Kili Challenge mjini Moshi, Kilimanjaro, inayoandaliwa na kampuni ya dhahabu ya Geita Gold Mining kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Kupambana na Ukimwi (Tacaids).

 “Njia kuu ambayo Uingereza inafanya  ni  kuwa mmoja wa wachangiaji wakubwa wa Mfuko wa Kimataifa wa kupambana na Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria, kwa miaka mitatu kuanzia mwaka 2024 hadi 2026, Uingereza itatoa pauni bilioni moja kwa mfuko huo ambao kwa jumla utatoa dola milioni 602 kwa Tanzania.

 “Nitoe  pongezi kwa AngloGold Ashanti na Bodi ya Wadhamini ya Geita Gold Mining Limited, Kilimanjaro Challenge dhidi ya HIV/AIDS pamoja na Tacaids kwa kuifanya Kili Challenge kuwa tukio la kila mwaka  la  kupendeza likileta ujumbe wa nguvu kwa wanaoishi na VVU,” amesema.

Akizungumza katika hafla hiyo, mwakilishi kutoka Geita Gold Mining, Mhandisi Nzuamkende amesema kampeni hiyo inayofanyika  kwa mwaka wa 22, inalenga kukusanya fedha kuchangia jitihada za Serikali ya Tanzania kufikia malengo ya sifuri tatu (maambukizi mapya -sifuri, unyanyapaa-sifuri na vifo vinavyohusiana na Ukimwi-sifuri).

 “Tunapokusanyika hapa ili kusherehekea mafanikio yenu, ninatoa shukrani zangu za dhati kwa kila mmoja wenu kwa kukabiliana na hofu zenu na kushinda mojawapo ya milima mirefu zaidi na yenye changamoto duniani.

 “Juhudi zenu kwenye miteremko ya Mlima Kilimanjaro na kwenye njia tambarare za baiskeli, hazijadhihirisha tu nguvu ya uamuzi na umoja, lakini pia zimeleta athari kubwa katika dhamira yetu ya pamoja ya kupambana na VVU na Ukimwi, mmetuonyesha hakuna changamoto isiyoweza kuzuilika tunapokutana kwa sababu moja na kwa hilo, nawapongeza nyote,” amesema.

Aidha, amewashukuru  wafadhili na washiriki  wote kutokana na michango yao inayoendelea kufanikisha kampeni hiyo hadi kuufanya  Mfuko wa Kili Challenge Against HIV/AIDS Trust kuwa  mfuko wa kimataifa, unaohusisha wapanda mlima na waendesha baiskeli kutoka mabara yote na zaidi ya nchi 20. 

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tacaids, Dk Jerome Kamwela amesema Tanzania inafanya vizuri kuelekea malengo ya kimataifa ya muda mrefu na wa kati ambayo ni kufikia 95 tatu kufikia mwaka 2025 ambazo tawimu za karibuni zinaonyesha kuna watu milioni 1.7 wanaishi na VVU.

Amesema 95 ya kwanza ni kuona watu hao wanatambuliwa na kujua hali zao ambapo sasa imefika asilimia 83, huku 95 ya pili ni wale wanaoishi na VVU watumie dawa za kufubaza makali ya Ukimwi (ARV) ambapo Tanzania imevuka lengo kwa kufikisha asilimia 98 na 95 ya tatu ni kwa wale wanaotumia ARV wawe wamefubaza virusi na kuelezakuwa utafiti wa mwisho unaonyesha maambukizi mapya yamepungua.

 Baadhi ya washiriki wenye umri mdogo waliopanda Mlima Kilimanjaro ni Regina Baraka na Baraka Erasto, kutoka kituo cha Moyo wa Huruma cha mkoani Geita, kilichoanzishwa kupitia mfuko wa Kili Challenge.

Watoto hao wameelezwa kufurahishwa kwa uzoefu walioupata kwa mara ya kwanza wakipanda mlima huo, hivyo kutoa hamasa kwa vijana wadogo wenye umri kama wao kujitokeza kushiriki kampeni hiyo, ili kuleta mabadiliko kwa wenye VVU.

Related Posts