Tabora. Baada ya baadhi ya wanawake waliopata huduma ya kujifungua katika Zahanati ya Isevya iliyopo Manispaa ya Tabora na kulalamika kuchunguliwa na watu wasio na maadili, hatua zimeanza kuchukuliwa.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu Agosti 5, 2024 kuhusiana na hilo, Meya wa Manispaa ya Tabora, Ramadhan Kapera amesema ujenzi wa uzio wa zahanati hiyo utaanza Septemba 2024 na fedha zimeshapatikana.
“Baada ya uwepo wa matendo hayo yasiyo na utu kwa vijana kwenye Kata ya Isevya, kuwachungulia wanawake wanapojifungua, tulianza kuchukua hatua kwa kutenga Sh20 milioni kwa ajili ya kujenga uzio mkubwa utakaozunguka zahanati hiyo, ili tukomeshe tabia hizo,” amesema Kapera.
Amesema tayari Baraza la Madiwani na manispaa wameridhia fedha hizo zielekezwe kwenye ujenzi wa uzio huo na zilizobaki ziingizwe kwenye akaunti ya benki ya zahanati hiyo ili ujenzi uanze mara moja.
“Malengo yetu mengine ni kuondoa muingiliano uliokuwepo baina ya wakazi wa Isevya na wagonjwa wanaofika kupata huduma katika zahanati hiyo na ukikamilika utaondoa adha, hasa kwa wajawazito,” amesema.
Kapera amesema tangu zahanati hiyo ijengwe zaidi ya miaka 20 iliyopita, haikuwahi kuwa na uzio na malalamiko ya wajawazito kuchunguliwa wakati wakijifungua yalianza kusikika miezi saba iliyopita.
“Sasa hatua zimeanza kuchukuliwa kwa kuhakikikisha ujenzi wa uzio huo unakamilika, ili kulinda utu wa wanawake hao,” amesema meya huyo.
Akizungumza na Mwananchi Digital akiwa kwenye zahanati hiyo, Mwanaidi Mussa, mkazi wa Isevya amepongeza hatua hiyo ya Serikali, lakini ameiomba ujenzi wake uharakishwe.
Amesema wajawazito wanaofika kujifungua kwenye zahanati hiyo wanajikuta wakidhalilika kutokana na kuchunguliwa na watu kupitia madirishani hususan vijana.
“Binafsi sijawahi kukumbwa na kadhia hiyo, ila wapo marafiki zangu wamewahi kuchunguliwa walipokuwa wanajifungua, kwa kuwa Serikali imesema ujenzi utaanza mwezi wa tisa, basi kazi hiyo imalizike haraka,” amesema Mussa.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi mkoani hapa limesema mpaka sasa halijapata kesi yoyote kuhusiana na changamoto hiyo na endapo watapata watazifanyia kazi kwa haraka.
Akizungumza na Mwananchi kwa simu leo Jumatatu Agosti 5, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora Richard Abwao amesema wanaofanya hivyo wakibainika, watashtakiwa kwa kosa la shambulio la aibu.
“Kama kuna watu wanaojulikana kufanya vitendo hivyo ni vema wahusika wakatoa taarifa polisi, ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao,” amesema kamanda huyo.