Bandari ya Tanga mshirikiane na Shirika la Reli la Tanzania (TRC) katika Usafirishaji wa bidhaa -RC Kunenge

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge ameishauri Menejimenti ya Bandari ya Tanga kushirikiana na Shirika la Reli la Tanzania (TRC) katika Usafirishaji wa bidhaa ili kutanua wigo wake katika kutoa huduma kwa wateja.

Mh Kunenge ameyasema hayo wakati alipotembelea banda la Bandari ya Tanga ndani ya Maonesho ya Kimataifa ya Wakulima Nanenane Kanda ya Mashariki yanayofanyika katika uwanja wa Mwalim Jk Nyerere mkoani Morogoro.

Aliendelea kwa kusema kuwa Ushirikiano wa Bandari ya Tanga na Shirika la Reli Tanzania (TRC) katika sekta ya Usafirishaji utazaa matunda mazuri na kuleta tija katika sekta ya usafirishaji nchini.

Kwa upande wake Afisa Masoko wa Bandari ya Tanga, Habiba Godigodi ameeleza kuwa lengo hasa ya kushiriki maonesho haya ni kuwaelimisha watu huduma mbalimbali zinazotolewa na Mamlaka ya Usimamizi wa bandari TPA na kuwahamasisha wakulima kutumia bandari kusafirisha mazao yao kwani njia ya bandari ni nafuu ukilinganisha na njia nyengine ya usafirishaji

“Mkulima anaweza kusafirisha mazao yake kwenda nje ya nchi kwa kutumia usafiri wa bandari kwani tunatumia “Reefer Containers” maalum ambazo zitahifadhi mazao na kufika mahala husika zikiwa salama na ubora ule ule,” amesema Habiba.

Bi Habiba ameongeza kwa kusema kuwa Bandari ya Tanga vilevile Inashiriki maonyesho hayo ili kuwaatarifu wananchi juu ya maboresho yaliofanywa na Serikali ya awamu ya sita chini ya Mh Rais Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa wa shilingi bilioni 429.1 katika Bandari ya Tanga ikiwemo kuongezwa kina kutoka mita 3 hadi 13 na kuiwezesha Bandari hiyo kuhudumia shehena kubwa zaidi kutoka tani 750,000 kwa mwaka hadi tani 3,000,000 kwa mwaka.

Tangu kukabidhiwa baada ya maboresho hayo bandari ya Tanga imehudumia meli 35 kubwa za mizigo zilizotia nanga gatini ambapo awali hazikuweza kutia nanga gatini kutokana na kuwa na kina kifupi

 

Related Posts