CHINO: Glovu za pilipili zilivunja pambano

WANASEMA kichaa anachekesha akiwa hatoki kwako. Usemi huu umemkumba mmoja wa mabondia wakali wa ngumi za kulipwa, Said Mohamad ‘Said Chino’.

Unajua kwa nini? Ni kwa sababu baada ya kupoteza pambano la mwisho dhidi ya Ibrahim Class wapinzani wake walimbeza kwa kuchukua vipande vya video vya pambano lake hilo kwamba alipigwa kama begi la mazoezi na Class.

Mwanaspoti lilifunga safari kutoka mitaa ya Tabata hadi kwenye makazi ya akademi ya mchezo wa ngumi ya kisasa ikiwa na vifaa vyote muhimu ya Mafia Boxing iliyopo Mbezi Msumi jirani kabisa na Pori la Akiba la Pande.

Chini ya menejimenti ya akademi hiyo iliyo kwenye makazi tulivu yaliyokusanya vijana wenye ndoto za kufika mbali katika mchezo huo huku wakipewa huduma zote muhimu, anafunguka mambo mengi kuhusu kazi yake hiyo ikiwamo pambano lake lijalo.

Hadi sasa ndiye bondia pekee wa Mafia Boxing mwenye rekodi ya kucheza mapambano mengi akiwa amecheza jumla ya mapambano 35 akiwa ameshinda 21, 15 akishinda kwa ‘Knockout’, amepigwa 12 na kati ya hayo ‘Knockout’ zikiwa tatu pekee huku akitoka sare mara mbili.

Jumamosi ya wikiendi hii anatarajia kupanda ulingoni katika pambano la kimataifa litakalopigwa kwa raundi 10 dhidi ya bingwa wa zamani wa dunia wa IBF, Simpiwe Vetyeka kutoka Afrika Kusini huku Chino likiwa pambano lake la pili kimataifa tangu ajiunge menejimenti ya Mafia Boxing.

Bondia huyo amefunguka mambo mengi yaliopitia katika umri mdogo hadi kuingia katika mchezo wa ngumi za kulipwa akiamini ndiyo sehemu pekee itakayoweza kubadili hatua za maisha yake, huku akisisitiza hajawahi kumjua baba yake hadi kufikia leo na hapa analizwa;

Ina maana hujawahi kuonana na baba yako?

Chino: Ni kweli. Mimi na dada yangu hatujawahi kumjua mzee wetu hadi mama anafariki dunia, ila tulielezwa na baba wa kambo ambaye muda mwingi wakati wa uhai wa mama tulijua ndiye baba yetu mzazi.

Mi na dada yangu tuko wawili na hatujapishana sana kuzaliwa, labda mwaka au miezi kadhaa na hata tukiongozana utajua tu hawa ni wa familia moja.

Anasema hilo lilitokea kwa sababu ya maisha ya wazazi wao. Kwa nini waliondoka na mama?

Chino: Nikwambie tu kiasili mimi ni Msukuma upande wa baba. Mama alituambia baba alikuwa ni mfanyabishara wa ng’ombe na waliachana baada ya mzee wetu kuoa mwanamke mwengine ambaye alikuwa binti mdogo, hivyo mama wakati tukiwa wadogo aliamua kuondoka na sisi kurejea Dar es Salaam kutokea Tabora.

Maisha na mama yao yalikuaje?

Chino: Lakini kwa mipango ya Mungu mama alipata mume mwengine Tabora aliyekuwa karani wa mahakama kabla ya kuhamishiwa Arusha na kuwa hakimu wa mahakama ya mwanzo, anaitwa mzee Hassan Habibu. Huyu alikuwa baba mlezi na tulijua ni baba yetu mzazi, ingawa alipata watoto wengine wawili na mama.

Wahamia Arusha, ilikuaje?

“Tuliishi naye Tabora halafu akahamishiwa Arusha, huko nikaanza elimu ya msingi, nimesoma kule hadi darasa la nne kabla ya kuanza kwa misukosuko mwaka 2006 baada ya mama kupata ugonjwa wa kupooza uliosababisha kifo chake mwaka 2007.

Walijuaje mzee Hassan sio baba yao mzazi?

Chino: Nakumbuka wakati mama anaumwa ndiyo nilijua mzee Hassan siyo baba yangu mzazi kwa sababu mama alituambia atafanya kila awezalo atupeleke kwa baba yetu. Hata hivyo haikuweza kutokana na yeye kufariki kwake, hivyo sijawahi kumjua mzee wangu hadi sasa.

Msiba wa mama wabadili maisha, yapi yalimkuta?

Chino: Baada ya msiba mambo yalianza kubadilika kwa sababu mzee Hassan alitaka atuchukue ili niendelee na masomo ila familia iligoma na kuamua kunichukua kuja kuishi Dar huku Mbezi kwa ndugu zangu.

Akili yangu mwanzo ilichofikiria ikawa tofauti na kile ambacho nilikutana nacho, maisha yakawa magumu, asubuhi hata pesa ya kitafunwa cha chai ilikuwa mtihani, ilikuwa inapikwa chai tupu halafu mengine utajua wewe, kifupi mambo yalibadilika sana.

Aanza kuokota vyuma chakavu, nini hatma yake?

Chino: Hali ya maisha ikanifanya nianze kuokota vyuma. Hiyo ilikuwa mwaka 2008 ili maisha yaende, shule ikafia hapo kwa sababu nilikosa usimamizi mzuri, nikawa mtoto wa mtaani ingawa bado nilikuwa naishi kwa ndugu zangu japo kubwa kuna ndugu yangu mwingine alitokea kunisomesha kwenye shule za kulipia nikaishia kidato cha pili baada ya mambo kwenda ovyo kwa mtoa ada.

Alivyoibukia kwenye ngumi, nanai alimpokea?

Chino: Wakati nafanya kazi ya kuokota vyuma chakavu mitaa ya Mbezi, nilipita mahali nikakuta watu wanafanya mazoezi ya ngumi katika Gym ambayo ilikuwa inaitwa Chino Boxing Club, iliyokuwa chini ya kocha Ghafur.

Sasa wakati nafanya mazoezi pale lengo la kwanza ilikuwa ni kwenda jeshini kwa sababu wapo mabondia wengi tuliokuwa nao pale walipata ajira jeshini kupitia ngumi, nikawa nacheza ngumi za ridhaa kabla ya kuja katika ngumi za kulipwa.

Nashukuru Mungu nilikuwa nafanya vizuri na mwenyewe nilikuwa naona kabisa naenda kuwa mwanajeshi na kocha Ghafur Chino ndiye akawa kama mzee wangu, alikuwa ananinulia hadi viatu vya mazoezi, kwa sababu sikuwa na uwezo wowote.

Vyeti vya shule vilivyomzuia kutimiza ndoto yake jeshini, ilikuaje?

Chino: Kweli nilipata nafasi jeshini, lakini kizuizi kilikuwa ni mambo ya kitaaluma kwa maana vyeti vya shule. Kilitakiwa cheti cha darasa la saba na sekondari na mimi upande wangu sikuwa na chochote, safari na ndoto yangu ikaishia hapo. Baada ya hapo, sikuwa na njia nyingine ya kuweza kusogea kimaisha zaidi ya kugeukia ngumi za kulipwa.

Aliwezaje kupata chakula kutokana na ugumu wa maisha?

Chino: Unajua mazoezi yalikuwa jioni, sasa nikitoka mazoezini lazima nipite mitaa kituo cha daladala Mbezi kabla ya kujengwa stendi, kazi yangu kubwa ilikuwa ni kumenya viazi vya chips kwa watu na ujira wangu ni kama 2000 na sahani ya chips kavu, nyumbani ilikuwa kwenda kulala.”

Ana soko kubwa nje kuliko ndani ya nchi, ilianzaje?

Chino: Nadhani kwa sababu ya suala zima la ‘connection’ hasa upande wa promota wa ndani kushindwa kunijua mapema ndiyo umechangia lakini ukitoka nje ya mipaka Tanzania, soko langu ni kubwa kutokana kiwango ambacho nimekuwa nakionyesha hasa kwenye mapambano ya nje.

Unajua mimi siyo muongeaji sana wala mtu wa kujichanganya mara nyingi, pia imechangia ingawa sasa nashukuru hata wasiojua ngumi wanamjua Chino na wapinzani wameongezeka hasa upande wa maadui kwa sababu ya mchezo huu. Ni kitu cha kawaida.

Hata hivyo, hata suala mimi kutoka kwenda kuishi Afrika Kusini mwaka 2019 limechangia maana nilipata nafasi ya kufanya kazi na Michael Sediane kupitia gym yake na aliniona na kukubali uwezo wangu ingawa baadae nilirejea Bongo.

Kuna mambo mengi yameumiza kwenye ngumi, ni kipi hatokisahau.

Chino: “Kuna pambano nilipigana mwaka 2022, Botswana na bondia anaitwa Steven Bwagas, lilikuwa la ubingwa wa WBF, sasa jamaa kuna wakati tukawa tumekumbatiana kwenye raundi ya nne. Mwamuzi akasema ‘stop’ akimaanisha tuache kupigana hadi atuachanishe sasa wakati tukio hilo linatokea nilishusha mikono, mpinzani wangu akanipiga ngumi iliyoniangusha chini, ajabu mwamuzi alihesabu kama ‘knockout’ ingawa niliinuka na kuendelea na pambano kwa raundi nyingine ila iliniumiza sana.

Mambo ya ushirikina kwenye masumbwi yapo? Kwani Chino anasemaje?

Chino: Binafsi kwanza siamini kabisa katika hayo mambo ingawa yamekuwa yakisemwa sana ila nakumbuka kuna mwaka nilicheza na bondia (anamtaja jina), sasa siwezi kusema ni ushirikina, lakini katika glovu zake sijui zilikuwa na kitu gani maana zilikuwa zinawasha.

Sasa sijui waliweka pilipili, kiukweli sina uhakika maana ilifanya pambano kuvunjika kwa vurugu za mashabiki na hiyo hali ilichangiwa kwa kiasi kikubwa, halafu siwezi kujua kama ndiyo ulikuwa ushirikiana kwa kuwa nguvu sijaweka huko zaidi ya mazoezi.

Hivi ndivyo alivyojiunga na Mafia Boxing, amtaja kocha wake

Chino: Nadhani mimi mwenyewe ndiyo sababu kujiunga na Mafia Boxing kwa sababu ya mtazamo wangu katika ngumi za kulipwa ingawa kabla ya kujiunga nao niliongea na kocha wangu Ghafur Chino juu ya kutaka kujiunga na Mafia.

Apania pambano la Jumamosi, ataweza?

Chino: Nashukuru mwalimu wangu alinielewa vizuri, nipo hapa kwa baraka zake lakini uongozi wa Mafia wameupokea vizuri. Kwa sasa wananidai mafanikio ya ushindi katika kila pambano watakaloniandalia tukianza na hili la Agosti 10, mwaka huu kwenye Ukumbi wa City Centre, Magomeni dhidi ya Simpiwe Vetyeka kutoka Afrika Kusini.

Kitu cha pekee ninachoweza kusema ni kwamba Mafia kwangu ni sehemu sahihi ambayo naweza nikafikia ndoto zangu kwa sababu ndiyo mejimenti ambayo imefunga vifaa vya kisasa kwa ajili ya mabondia wake kubwa bora.

Related Posts