Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema Serikali itaendelea kufanya juhudi na kuchukua hatua za makusudi kuhakikisha nchi na wananchi wanakuwa salama, badala ya kuendelea kuwa dampo la bidhaa zisizokuwa na ubora.
Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Jumanne Agosti 6, 2024 alipofungua kituo cha ukaguzi wa vyombo vya moto katika Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS).
Amesema hatua hiyo ni katika juhudi za Serikali kuleta mageuzi makubwa katika sekta za usafiri na kukuza uchumi wa nchi. Kituo hicho kimegharimu Sh1.9 bilioni hadi kukamilika.
Amesema wataendelea kujenga miudombinu imara kuwezesha kufanya shughuli za usimamiaji ubora ziwe za kisasa zaidi kwa kuwapatia majengo, maabara, vifaa vya kisasa na wataalamu wa kutosha.
“Hatua hiyo kwa kiasi kikubwa itasaidia kulinda afya na usalama wa wananchi, kuhifadhi mazingira ya nchi, kuweka ushindani sawa na mazingira wezeshi ya kufanya biashara,” amesema.
Dk Mwinyi amesema pia itaviwezesha viwanda vya ndani kuzalisha bidhaa zenye viwango.
Kupitia mpango huo wa ubora wa bidhaa, amesema Serikali imedhamiria kuziwezesha taasisi zinazohusika ziwe na maabara za kisasa na wataalamu wenye uwezo katika kazi za upimaji bidhaa nchini.
Amesema ili kufikia mpango huo, wanaendelea kuimarisha miundombinu ya ubora ya ZBS na miongoni mwa hatua hizo ni ujenzi wa kituo hicho.
“Hakika hii ni hatua kubwa na muhimu ya kuimarisha taasisi hii ili iweze kufanya kazi zake kwa ufanisi zaidi,” amesema.
Rais Mwinyi amesema katika suala la usalama na ubora wa vyombo vya moto vinavyotumika nchini, kuna umuhimu wa kuhakikisha vinakaguliwa na kuthibitishwa ubora wake kwa matumizi ya barabarani.
“Kama tunavyojua vyombo hivyo vinapokosa ubora husababisha madhara mbalimbali ikiwamo uchafuzi wa hewa unaotokana na moshi, ajali za mara kwa mara ambazo kwa kiasi kikubwa zimechangia kupoteza nguvu kazi ya Taifa,” amesema.
Dk Mwinyi amesema Serikali hulazimika kutumia fedha nyingi kupitia sekta ya afya kwa kutoa huduma za matibabu kwa waathirika wa ajali hizo.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali (OCGS) kwa mwaka 2023 jumla ya ajali 193 zimeripotiwa, huku Wilaya ya Magharibi A, Mkoa wa Mjini Magharibi ukiripotiwa kuwa na ajali zaidi ambazo ni 31 sawa na asilimia 16.6 ikilinganishwa na wilaya nyingine. Idadi hiyo ni sawa na ongezeko la asilimia 12.2 kutoka ajali 172 kwa mwaka 2022.
“Hapa Zanzibar kuna taasisi mbalimbali zinazohusika na ukaguzi na usalama wa vyombo vya moto, ukaguzi unahusisha wa awali baada ya vyambo hivyo kuingia nchini na ukaguzi wa kila mwaka, kwa hiyo lazima tuhakikishe jambo hili linadhibitiwa,” amesema.
Katika eneo hilo amesema kimejengwa kituo jumuishi ambacho mwananchi anaweza kupata bima ya chombo chake, kufanya malipo kupitia benki na kusajili chombo hicho kupitia Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA).
Amezitaka taasisi hizo kushirikiana kuondoa urasimu ili mwananchi anayefika katika kituo hicho akamilishe taratibu zote bila usumbufu na kuokoa muda wa kuzunguka taasisi moja baada ya nyingine.
Amesema kituo hicho kitaongeza uwezo na ukaguzi wa vyombo vya moto utakaosababisha kuwa salama na vinafaa kwa matumizi.
Ametumia fursa hiyo kuwataka watumishi wa mamlaka hiyo kuvitunza vifaa hivyo ili kufikia malengo.
Kabla ya kujenga kituo hicho, Serikali iliunda kamati maalumu iliyopendekeza mfumo wa mageuzi wa ZBS.
Kamati iliundwa kutokana na maagizo aliyoyatoa Rais Mwinyi kuwataka kufanya tathmini ya ufanisi ya utekelezaji wa kazi wa ZBS na kubaini upungufu wa kimuundo na shughuli za kiutendaji.
Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Omar Said Shaaban, bila kutaja idadi kamili, amesema takwimu zinaonyesha uingiaji wa vyombo vya moto umeongezeka kwa kiasi kikubwa kisiwani humo.
Amesema kituo hicho kitatoa huduma za haraka na viwango vya hali ya juu kupunguza upimaji wa kutumia macho.
“Miongoni mwa mambo muhimu yatakayopatikana kutokana na uwepo wa kituo hiki ni pamoja na kulinda usalama, kuogeza ubora na kuepusha ajali za mara kwa mara,” amesema.
Alitumia fursa hiyo kuzitaka mamlaka zinazohusika na upitishaji wa vyombo vya moto kutoa ushirikiano kwa ZBS ili kazi hiyo ifanikiwe.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa ZBS, Yussuph Majid Nassor amesema kituo hicho chenye pande mbili, kina uwezo wa kukagua magari 300 kwa siku, huku kila upande ukiwa na uwezo wa kukagua magari 150.
Amesema kituo hicho kinaendeshwa na mitambo bila kuwapo mtu yeyote anayeingilia, hivyo gari linapobainika kuwa na kasoro inakuwa ya kweli kwani hakuna mtu anaweza kuingilia mtambo huo.
“Iwapo gari likionekana lina shida zile ndogondogo, tunampa mtu siku 14 akatengeneze kisha anarudi kupima hatumtozi gharama zingine, kwa hiyo kuna muda wa kufanya matengenezo wananchi wasiwe na wasiwasi,” amesema.
Mtambo huo utakaofanya kazi kwa saa 24 una uwezo wa kukagua gari moja kati ya dakika saba hadi 10.