Dosari za kisheria zilivyomuachia huru aliyehukumiwa miaka 20 kwa kudakwa na mirungi

Arusha. Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Manyara, imemuachia huru Shabani Halili, aliyehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kukutwa na dawa za kulevya aina ya mirungi kilo 10.60

Mahakama hiyo imemuachia huru mrufani huyo na kufuta hukumu na adhabu iliyotolewa dhidi yake, baada ya kubaini dosari ya kisheria wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo katika Mahakama ya chini.

Kubatilishwa kwa hukumu hiyo kunatokana na Mahakama hiyo kubaini kuwa Shabani hakuwahi kukiri kosa hilo kama ilivyodaiwa wakati wa mwenendo wa shauri hilo katika Mahakama ya chini na pia hakuwahi kusomewa maelezo yake ya onyo.

Hukumu hiyo imetolewa Agosti mosi, 2024 na Jaji Frank Mirindo, aliyekuwa akisikiliza rufaa hiyo ya jinai namba 11360/2024, ambayo pia imewekwa kwenye mtandao wa Mahakama.

Ilidaiwa katika Mahakama ya chini kuwa Novemba 22, 2022, askari polisi katika kizuizi cha Minjingu wilayani Babati, Mkoa wa Manyara walipokagua gari la abiria, walishuku begi lililokuwa likitoa harufu kwenye buti la basi hilo.

Ilidaiwa kuwa begi hilo lilikuwa na lebo inayoonyesha mmiliki wake alikuwa amekaa kwenye kiti namba 24 kilichokuwa kimekaliwa na Shabani, hivyo aliitwa na kutajwa kuwa ndiye mmiliki wa begi hilo.

Katika Mahakama ya Wilaya ya Babati, Shabani alisomewa shtaka la kusafirisha dawa za kulevya, kinyume na kifungu cha 15A (1) na (2) (c) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya na kuhukumiwa kifungo cha miaka 20 jela.

Hata hivyo, Shabani aliomba kibali cha Mahakama Kuu cha kukata rufaa nje ya muda, alikakubaliwa na aliwasilisha sababu tano za kukata rufaa hiyo.

Katika rufaa hiyo, Shaban aliwakilishwa na wakili Joseph Masanja, huku Jamhuri ikiwakilishwa na wakili Rose Kayumbo.

 Wakili Masanja aliwasilisha hoja hizo kuwa shtaka hilo halikuthibitishwa na upande wa mashtaka bila kuacha shaka na Mahakama haikuthamini ushahidi wa Shabani.

Naye wakili Kayumbo alipinga vikali malalamiko hayo kwamba shtaka hilo halikuthibitishwa bila shaka na kudai Shabani alikamatwa katika Daraja la Ngasere akitokea Moshi kuelekea Dodoma, akiwa kwenye kiti namba 24 akiwa na begi lililowekwa kwenye buti la basi ambalo lilitambulika kwa alama ya kiti.

Akitoa uamuzi katika rufaa hiyo, Jaji alisema katika kushughulikia sababu za kukata rufaa, ni muhimu kupitia upya ushahidi uliotolewa katika Mahakama ya Wilaya ya Babati.

Alieleza kuwa kesi ya upande wa mashtaka inategemea hasa ushahidi wa moja kwa moja wa shahidi wa pili na wa tatu, na kwa kiasi fulani, shahidi wa nne.

Ilidaiwa kuwa alipoitwa na kuulizwa kuhusu begi hilo, shahidi wa tatu wa mashtaka alidai kuwa Shabani alikiri begi hilo ni lake, huku Shabani akakiri kupanda basi hilo, lakini akakana kumiliki begi lililokuwa kwenye buti.

Jaji alieleza kumbukumbu zinaonyesha katika usikilizwaji wa awali, Shabani alidai kuwa polisi walimnyang’anya tiketi ya kielektroniki aliyokuwa nayo, na mahakamani waliwasilisha tiketi ya kawaida iliyojazwa kwa mkono.

Kuhusu maelezo ya onyo ya Shabani, Jaji alieleza kuwa shahidi wa tatu wa upande wa mashtaka alidai Shabani aliwaonyesha tiketi yake ya basi na shahidi wa pili alidai Shabani alikuwa kwenye kiti namba 24 na walichukua tiketi yake iliyokuwa imeandikwa namba 30.

Jaji alieleza kuwa alikagua tiketi iliyowasilishwa mahakamani ambayo iliandikwa kuwa Shabani alikuwa ameketi kwenye kiti namba 24, na nauli ilikuwa Sh 300.

Hata hivyo, hakukuwa na popote ilipoandikwa tiketi namba 30 kama ilivyodaiwa na shahidi mwingine wa mashtaka.

“Kitendo cha begi linaloshukiwa kubeba mirungi kikiwa na lebo ya kiti namba 24 na mrufani kukaa kwenye kiti hicho ndani ya basi hilo linaibua mashaka makubwa kuhusu umiliki wa mrufani na kusafirisha mirungi, na kanuni ya msingi ya ushahidi wa makosa ya jinai ni kwamba upande wa mashtaka unabeba mzigo wa kuthibitisha kosa bila shaka yoyote,” alisema Jaji.

Huku akinukuu mashauri mbalimbali, Jaji alieleza kuwa bila uthibitisho wa wazi wa tiketi ya basi, tuhuma dhidi ya Shabani kuhusu umiliki wa begi hilo zinatia shaka.

Jaji alieleza swali linalofuata ni nani aliyekuwepo wakati begi hilo lilipokaguliwa. Shahidi wa mashtaka alidai kuwa begi lilikaguliwa mbele ya Shabani, kondakta wa basi, polisi mmoja, na abiria mmoja, huku shahidi wa tatu akidai kuwa begi lilikaguliwa na polisi pekee bila kondakta kuwepo.

“Nimeridhika kwamba upande wa mashtaka ulifeli bila sababu za kutosha kumwita kondakta wa basi ambaye angefafanua mashaka katika kesi yao,” alieleza Jaji.

Jaji alieleza kuhusu maelezo ya onyo na nyaraka nyingine zilizowasilishwa kama vielelezo mahakamani wakati wa usikilizwaji, ikiwemo cheti cha kukamatwa. Wakili wa Shabani alidai kuwa nyaraka hizo hazikuwasilishwa ipasavyo.

Jaji alieleza kuwa kutokana na mzozo kuhusu umiliki wa begi lililokuwa na mirungi, itakuwa ni dhulma kumlaumu Shabani kwa kuzingatia maelezo ya onyo ambayo hayajasomwa kwake.

“Katika kesi hii, hati ya masuala ambayo hayana shaka wala yaliyomo kwenye hati iliyokubaliwa haikusomwa na kuelezewa kwa Shabani. Haijulikani jinsi Mahakama ya awali ilihitimisha kuwa mrufani alikubali mambo mawili.

Maelezo yake binafsi na kukamatwa kwake na maofisa wa polisi bila ya ukweli kusomwa na kuelezwa kwake. Kwa vyovyote vile, mrufani hakuwahi kukiri kutoa maelezo ya onyo, na hayajasomwa kwake,” aliongeza Jaji.

Jaji huyo alisema kwa kuwa Shabani hakuulizwa kama anakubali yaliyomo kwenye maelezo hayo, maelezo hayo yanakosa thamani na Mahakama inayatupilia mbali. Hakuna ushahidi wa kuunga mkono shtaka hilo.

“Kwa uchambuzi uliofanywa hapo juu, nakubali rufaa na si lazima kuzingatia sababu zilizobaki za kukata rufaa. Wala si lazima kushughulikia swali la pili nililouliza wahusika kuhusu uhalali wa hukumu iliyotolewa na Mahakama. Naamuru mrufani aachiliwe mara moja,” alihitimisha Jaji.

Related Posts