MABINGWA watetezi wa Ligi ya Kikapu Mkoa wa Mwanza (Marba), Eagles imeanza vibaya katika kampeni ya kutetea ubingwa baada ya kufungwa na Profile kwa pointi 81-72.
Mchezo huo uliokuwa wa ufunguzi ulichezwa katika Uwanja wa Mirongo uliopo mjini humo
Akizungumzia mchezo huo na Mwanasposti, kocha wa kikapu, Benson Nyasebwa alisema timu nane ndizo zitakazoshiriki michuano hiyo.
Alizitaja timu hizo kuwa ni Sengerema Hoopers, CUHAS, Oratorio, Profile, Young Profile, Mwanza Eagles, Planet na CIC.
Nyasebwa alisema mfumo utakaotumika katika ligi hiyo ni kwa kila timu kucheza na nyingine na timu nne za juu zitakazopatikana zitacheza nusu fainali kwa mfumo wa ‘best of three play off.’
“Nusu fainali timu itakayoshika nafasi ya kwanza itacheza na ya nne, ya pili itacheza na ya tatu,” alisema Nyasebwa.
Kocha huyo ambaye pia ni katibu mkuu msaidizi wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), alizipongeza timu zote zilizojitokeza kushiriki mashindano hayo.