WAKATI joto la dabi ya Kariakoo likiendelea kupanda, kocha mkuu wa Simba, Fadlu Davies ameandaa sapraizi katika kikosi chake kabla ya kuivaa Yanga Alhamisi, Agosti 8, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Mwanaspoti linajua baada ya Simba kumaliza tamasha la Simba Day lililofanyika Jumamosi iliyopita kocha huyo alitoa mapumziko kwa kikosi hicho huku akiwasihi wachezaji kuangalia mechi ya Yanga dhidi ya Red Arrows iliyopigwa juzi kwenye uwanja wa Mkapa katika kilele cha Wiki ya Wananchi.
Fadlu aliwasisitiza wachezaji kuiangalia vyema Yanga kwani ndiye mpinzani watakayekutana naye katika mchezo ujao wa nusu fainali ya Ngao ja Jamii kesho kutwa Alhamisi.
Wachezaji wa Simba wote walifanya hivyo ambapo baadhi yao walijumuika kwa makundi hususani wale wapya na kutazama mechi kwa pamoja katika hotel moja jijini Dar es Salaam huku wengine wakitazama wakiwa majumbani.
“Tuliambiwa kuangalia mechi, wapo waliokuwa hotelini kwa pamoja lakini wengine tulikuwa majumbani,” amesema mmoja wa wachezaji wa Simba na kuongeza;
“Hadi tunamaliza mechi yetu ya mwisho hakuna mchezaji aliyekuwa na uhakika wa nafasi ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza. Kocha huyu anapenda kila mtu acheze na ana uamuzi mgumu hivyo hadi sasa ukiniambia nikupangie kikosi cha kwanza siwezi.”
Wakati wachezaji wakiitazama mechi ya Yanga kwa namna tofauti, kocha Fadlu na benchi lake zima la ufundi nao waliitazama mechi hiyo kwa pamoja kiufundi zaidi.
Ofisa habari wa Simba, Ahmed Ally alisema wameridhishwa na uwezo wa kikosi chao kipya na sasa wako tayari kuanza mapambano bila kuihofia timu yoyote.
“Tumekamilika na tumeridhika na timu yetu iliyosheheni vijana. Tupo tayari kwa mapambano na hili litathibitishwa Agosti nane tutakapocheza na Yanga, mtaona wenyewe namna timu ya kisasa inavyocheza,” alisema Ahmed.
Simba ilirejea mazoezini jana Jumatatu, na leo itaendelea na programu ya mazoezi katika uwanja wake wa Mo Simba Arena uliopo Bunju Dar es Salaam.