Kampuni iliyomshtaki Marioo, meneja wake yalalama hukumu kuchelewa

Dar es Salaam. Kampuni ya Kismaty Advert Media Co. Ltd, iliyomshtaki msanii wa muziki wa kizazi kipya ‘Bongo Fleva’ Omary Mwanga, maarufu Marioo imemuomba Jaji Mkuu wa Tanzania kuingilia kati kesi hiyo kuwezesha hukumu kutolewa.

Kampuni hiyo inayojihusisha na uandaaji wa matamasha na shughuli zinazohusu burudani yenye makao jijini Arusha, ilimshtaki Marioo na meneja wake, Sweetbert Mwinula Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ikimdai malipo ya Sh550 milioni, kwa kuvunja mkataba wa utumbuizaji.

Kesi hiyo ya madai namba 29/2022 ilisikilizwa na Jaji Joachim Tiganga, aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, kwa sasa amehamishiwa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya.

Katika majibu ya utetezi wa maandishi, wadaiwa walikana kuwepo kwa ukiukwaji wa mkataba wa utumbuizaji baina yao na mdai.

Wanadai mdai ndiye alishindwa kutekeleza masharti ya kimkataba kama walivyokubaliana.

Hata hivyo, wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo, Marioo hakutokea mahakamani kujitetea isipokuwa meneja wake pekee.

Mkurugenzi mtendaji ambaye pia ndiye mmiliki wa kampuni hiyo, Mary Emmanuel amelalamikia hatua ya kuahirishwa kwa hukumu mara kwa mara.

“Tangu usikilizwaji umekamilika hukumu imeahirishwa mara nne na wakati mwingine kesi imekuwa ikiahirishwa bila hata kuitwa badala yake karani tu ndio anakutana na mawakili na kuwatajia tarehe, lakini wakati mwingine siambiwi sababu za kuahirishwa,” amedai.

Amedai kesi hiyo imesababisha shughuli zake kusimama na kwa kadri hukumu inavyozidi kuahirishwa ndivyo anavyozidi kupata harasa kubwa, hivyo amemuomba Jaji Mkuu wa Tanzania kuingilia kati aweze kujua hatima ya haki yake.

Kwa mujibu wa Mary, kwa mara ya kwanza hukumu ilipangwa kusomwa Juni 7, 2024 ikaahirishwa na Jaji Tiganga aliyesema kuna kipengele alikuwa bado hajakimalizia, akapanga kutoa hukumu Juni 19, 2024.

Amedai Juni 19, alipokwenda mahakamani wakili wake alikuwa msibani hivyo alielezwa na wakili wa Marioo kuwa hukumu imepangwa kusomwa Julai 19, 2024 na kwamba itasomwa ‘online’ (video conferencing – teknolojia ya mawasiliano kwa njia ya video kupitia kompyuta au runinga).

Anadai pia, alimweleza hukumu itawekwa katika maktaba mtandao ya Mahakama (Tanzlii), hivyo hana haja ya kwenda mahakamani tarehe hiyo.

Mary amedai wakili wake pia alimweleza utaratibu ndivyo ulivyo lakini Julai 19, haikusomwa na wakili wake alimweleza kuwa jaji amehamishwa, hivyo iliahirishwa mbele ya jaji mfawidhi mpya hadi Agosti 2, 2024, siku ambayo pia haikusomwa.

Anadai kesi haikutajwa na hakuna sababu iliyotolewa badala yake karani aliwapa tarehe nyingine kuwa  itasomwa Agosti 12, 2024.

Akizungumza na Mwananchi, Agosti 5, 2024, Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Elia Mrema amesema ingawa Jaji Tiganga amehamishiwa Mbeya, kama ilivyo kawaida akikamilisha kuandika hukumu kwa kesi alizozisikiliza kabla ya kuhamishwa atazituma kwa msajili ambaye ndiye huzisoma.

“Hata juzi nimesoma hukumu zake nyingine alizotuma ambazo amemaliza, lakini hiyo bado haijafika. Maana yake bado anaiandika, lakini hoja ya kuambiwa hukumu ataiona Tanzlii (maktaba mtandaoni), hapana, hukumu inasomwa kwanza,” amesema Mrema.

Kuhusu kesi kuahirishwa bila kuitwa mahakamani na karani kutoa tarehe mpya, Mrema amesema hilo linawezekana kwa kuwa jaji aliyehama na majalada kwa ajili ya kuandika hukumu, anaweza akapanga tarehe lakini ikafika tarehe hiyo akawa hajaikamilisha.

Hivyo, amesema jaji anaweza kumwelekeza karani atafute tarehe nyingine, ndiyo maana wadaiwa wanaweza kupewa tarehe bila kuingia mahakamani.

Amesema anaamini Jaji Tiganga ambaye kwa sasa ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, atatoa hukumu hiyo mapema.

“Nitakachofanya nitamkumbusha ili hiyo hukumu aipe kipaumbele kwa sababu umesema imeshaahirishwa mara kwa mara,” amesema Mrema.

Kwa mujibu wa hati ya madai, mwaka 2021, kampuni ya Kismaty iliandaa shindano la Mr na Miss Vyuo Vikuu Kanda ya Kaskazini na Septemba 23, 2021, iliingia mkataba na wadaiwa (Marioo na meneja wake) kwa ajili ya kutumbuiza kwenye shindano hilo kwa malipo ya Sh15 milioni.

Kwa mujibu wa mkataba huo, shindano lilipangwa kufanyika Septemba 24, 2021 katika Shule ya Kimataifa ya Meru, Arusha na inadaiwa Marioo alikubali kutoa burudani katika shindano hilo tarehe hiyo na katika hafla iliyokuwa imeandaliwa kufanyika Blue Stone Lounge Septemba 25, 2021.

Katika kutekeleza wajibu wa kimkataba, kampuni hiyo inadai Septemba 17, 2021 iliwalipa Marioo na meneja wake Sh8 milioni kupitia akaunti ya Benki ya ABSA, yenye jina la Sweetbert Mwinula (meneja) na kwamba, tarehe ya kusaini mkataba iliwalipa kiasi kilichokuwa kimebakia.

Inadaiwa Septemba 25, 2021 wadaiwa walikiuka masharti ya mkataba kwa kushindwa kutokea kutumbuiza katika hafla ya Blue Stone Lounge kama walivyokubaliana, kitendo ambacho ni cha kiukiukaji mkataba, hivyo kuisababishia kampuni hiyo hasara.

Anadai kampuni ilipata hasara ya Sh500 milioni kutokana na gharama za maandalizi zilizowahusisha na wadau wengine.

Gharama nyingine ambazo kampuni hiyo inadai kuingia ni kiasi cha pesa ilizowalipa wadaiwa kwa ajili ya kutumbuiza, hasara ya kukosa biashara, hasara ya kukosa kipato na hasara ya jumla ya Sh50 milioni.

Kampuni hiyo inadai malipo ya fidia ya hasara hiyo halisi Sh500 milioni, riba ya asilimia 12 ya kiasi hicho kutoka tarehe ya hukumu mpaka tarehe ya kukamilisha malipo yote.

Pia, inaiomba Mahakama iwaamuru wadaiwa wailipe fidia ya hasara ya jumla Sh50 milioni, au kiwango ambacho mahakama itatathmini, gharama za kesi na nafuu nyingine

Related Posts