Dar es Salaam. Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Stergomena Tax amesema Serikali haitavumilia uvunjwaji wa aina yoyote wa sheria na yeyote atakayebainika kufanya hivyo atachukuliwa hatua stahiki.
Kauli ya Dk Tax inajibu tukio la kubakwa na kulawitiwa binti mkazi wa Yombo Dovya jijini Dar es Salaam, lililofanywa na kundi la vijana watano.
Video za tukio hilo zilisambazwa juzi Agosti 4, 2024 kwenye mitandao ya kijamii zikionyesha vijana hao wakimbaka na kumlawiti binti huyo kwa kile walichodai ametembea na mume wa mtu.
Katika video hizo, vijana hao wamesikika wakimtaka binti huyo amwombe radhi mtu waliyemtaja kwa jina la Afande.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne Agosti 6, 2024, Waziri Tax amesema Serikali haitavumilia uvunjaji wa sheria, atakayebainika kufanya hivyo atachukuliwa hatua stahiki.
Dk Tax alipoulizwa iwapo waliohusika ni askari wa Jeshi la Wananchi, amesema Jeshi la Polisi ndilo lenye mamlaka ya kufanya uchunguzi na kutoa jawabu la aliyehusika ni nani na wa namna gani.
Kwa sababu jeshi hilo limeshaeleza linaendelea kufanya kazi yake, maswali yote kuhusu nani anahusika yaelekezwe huko.
“Unaponiuliza mimi ni kama unamuuliza mtuhumiwa, anayehusika na uchunguzi wa kubaini mhalifu ni Jeshi la Polisi, uliza Jeshi la Polisi kujua hayo.
“Ukimtaja huyo askari wangu nitasema umetaja mtu, lakini sijathibitisha kwa sababu anayefanya uchunguzi ni mtu mwingine,” amesema.
Kauli ya Waziri Tax imekuja baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni kuthibitisha kukamatwa kwa wahusika wa tukio hilo, ingawa hajaweka wazi ni kina nani wala hatua zinazofuata.
Agosti 4, 2024, Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime alitoa taarifa kwa umma kuhusu tukio hilo, akilaani na kuahidi kulifanyia kazi.
“Jeshi limetoa wito kwa wananchi wote waache kuendelea kusambaza video hiyo, kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria, lakini ni kitendo cha kuendelea kudhalilisha utu wa binadamu mwenzetu.
“Tunatoa wito kwa mwenye taarifa ya kuhakikisha mkono wa sheria unawafikia kwa haraka waliofanya ukatili huu, asisite kutusaidia kwa kutupa taarifa au kumpatia kiongozi yeyote yule wanayemwamini kwamba taarifa ikimfikia watu hao (wahusika) watapatikana haraka iwezekanavyo,” alisema Misime.
Wadau mbalimbali kikiwamo Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), wamelaani tukio hilo wakiitaka Serikali ichukue hatua.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.